FBI yamtaja kijana wa umri wa miaka 20 aliyefyatulia risasi Trump
IDARA ya ujasusi Amerika (FBI) imemtaja mshukiwa aliyemshambulia Rais wa zamani wa Amerika Donald Trump.
FBI inasema kuwa Thomas Matthew Crooks, 20, alinuia kumuua Bw Trump.
Vile vile, Shirika la habari la AP limepekua sajili ya wapigakura na kubaini kuwa Crooks alikuwa amesajiliwa katika chama cha Republican eneo la Pennsylvania, chama ambacho Trump atatumia kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Novemba.
Mfyatuaji alikuwa mita 100 kutoka kwa Trump
Mshukiwa alikuwa umbali wa kati ya mita 120 – 150 kutoka alipokuwa Trump wakati alifyatua risasi kwa mkutano wa siasa. Hii ni kulingana na uchunguzi wa Shirika la habari la CNN.
Kulingana na FBI, mshambuliaji alilenga shabaha akiwa ‘eneo la juu ya nyumba’ nje ya mhadhara kabla ya kupigwa risasi na makachero hao.
Vurugu kutumia bunduki
Vurugu na vifo kupitia mtutu wa bunduki vimekuwa donda sugu kwa mamlaka za Amerika kwa muda mrefu.
Kulingana na takwimu kamili ya hivi karibuni zaidi, watu 48,830 walifariki kutokana na risasi mwaka wa 2021 nchini Amerika.
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kimeainisha vifo hivi katika misingi mitatu: bila kusudi, maafisa wa usalama na vifo ambavyo vyanzo vyao havikubainika.
Takwimu ya 2021 ndiyo kubwa zaidi tangu miaka ya 90 baada ya visa kuongezeka sana wakati wa janga la Corona duniani.
Mfumo wenye matatizo
Mwaniaji urais wa chama cha Green Party Jill Stein amesema ‘jaribio la kumuua Trump’ linatoa mwanga kwa mgogoro mpana wa mfumo wa kijamii na uongozi unaoathiri Amerika.
“Kilichofanyika leo kwa Trump, ninafikiri ni dalili ya mfumo wenye matatizo mengi. Yaani, ni mfumo wa kisiasa wenye matatizo ndani ya jamii yenye matatizo mengi,” mwaniaji mara tatu wa urais aliambia Shirika la habari la AP.
“Inasikitisha sana na ni muhimu kwetu kubaini kuwa hakuna aliye salama dhidi ya madhara ya matukio haya,” aliongeza.
Sera na umiliki wa bunduki
Angalau watu wazima 4 kati ya 10 wamekiri kuwa wanaishi katika nyumba ambayo ina bunduki nchini Amerika. Hii inajumuisha asilimia 32 ambao wanasema wao binafsi wanamiliki bunduki.
Hii ni kulingana na utafiti uliofanywa na kituo cha utafiti cha Pew Research Centre mnamo Juni 2023.
Sehemu ya utafiti huu inaeleza kuwa karibu nusu ya wasiomiliki bunduki wana nia ya kuwa nayo siku za usoni kwa sababu za kiusalama.
Licha ya wengi kutaja wanamiliki bunduki ili kujilinda na fahari, wengine wanasema wanazitumia katika uwindaji na michezo.
Republican wengi wanamiliki bunduki
Utafiti huu umenakili kuwa wengi wa wapigakura wa Chama cha Republican na wenye mwegemeo huo waliripoti kumiliki bunduki (45%) ikilinganishwa na wale wa Democrat (20%).
Katiba ya Amerika inawahakikishia Waamerika haki ya kubeba silaha – takriban thuluthi moja ya watu wazima nchini humo wanamiliki bunduki.
Ili kuangazia matukio ya kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na bunduki, Rais Joe Biden alipendekeza sheria za sera ya bunduki ili kupanua sheria ya usalama wa bunduki.
Sheria hii ilipitishwa na bunge mwaka jana kwa ushirikiano wa pande zote.