Makala

FUNGUKA: 'Paka wazee ndio shibe yangu'

February 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULIN EONGAJI

Ikiwa umewahi tembelea Pwani ya Kenya na hasa maeneo ya Malindi na Nyali, basi bila shaka utaelewa kuwa ni kawaida kukutana na mabinti wa Kiafrika wakiandamana na wanaume wa kizungu ambao mara nyingi huwa ni paka wazee.

Kwa mara nyingi mabinti hawa huchukuliwa kuwa wavivu na wengi husemekana kuwa na kiwango duni cha masomo, hawana ujuzi na huwa wanalenga kunufaika maishani.

Lilly ni mmoja wa mabinti hawa lakini yeye ni tofauti kabisa. Kwanza kabisa binti huyu anayetarajia kuhitimu miaka 35 mwezi Aprili, ni msomi. Amesomea uhandisi na ameajiriwa na mojawapo ya kampuni kubwa za ujenzi mjini Mombasa.

Ni ajira ambayo inamhakikishia donge nono kila mwezi kiasi cha kwamba mapato yake yanamwezesha hata kununua gari la kifahari pasi kuomba mkopo wa benki.

Lakini uwezo wake wa kifedha haujamzuia kusaka senti kutoka kwa hawa mababu ambapo tayari ana watoto sita kati ya miaka 10 na 2 kutoka kwa vikongwe tofauti.

Binti huyu anavutiwa na madume haya yaliyojaa mvi kichwani. Tangu alipokamilisha chuo zaidi ya mwongo mmoja uliopita, amekuwa akisaka wazee wa kizungu, na hafichi kwamba pesa zao ndizo anazovizia kiasi cha kwamba yuko tayari kuwazalia mradi tu kila mwisho wa mwezi anahakikishiwa kitita cha fedha.

 

Picha zinaninasia wanaume

“Kwa kawaida mawindo yangu mimi huyapata mtandaoni. Kutokana na picha zangu za kishua lazima madume wataingia mtegoni.

Kuna sifa ambazo mimi huangalia kabla ya kumpa sikio langu. Ili kunasa jicho langu sharti uwe angaa miaka sitini au zaidi. Pili lazima uwe na mfuko mzito na tayari kuhamia humu nchini kunigharimikia na wanangu na kutuhakikishia maisha ya raha mstarehe.

Lazima anionyeshe stakabadhi kuwa anamiliki nyumba na magari ya kifahari huko kwao, huku pia akiwa tayari kunifichulia taarifa za akaunti yake ya benki.

Nami niko tayari kumpa penzi na hata kumzalia mtoto mmoja, mradi ahakikishe kuwa kisima chake cha fedha hakikauki.

Ni mkataba ambao sisi huingia kabla ya kuanza uhusiano na hutiwa saini na wakili.

 

Sh200,000 kila mwezi

Kila mwezi nakusanya angaa laki mbili kutoka kwa kila mwanamume, fedha zinazohakikisha kuwa maisha yetu ni mazuri. Unapaswa kukumbuka kuwa mimi na wanangu tunahakikishiwa maisha haya ya starehe hata bila kugusa mshahara wangu.

Baba za watoto wangu wanatoka katika mataifa sita tofauti ikiwa ni pamoja na Uingereza, Amerika, Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji na Uswidi ambapo hakuna kati yao anayejua kuhusu watoto wa mwanamume mwingine.

Hakuna aliye na ruhusa ya kunitembelea kabla ya kuniarifu wiki mbili mapema.

Nina majumba mawili ambapo zamu ya mmoja wao ya kuja ikifika, wanangu wataishi katika nyumba tofauti na nitakayoishi na mhusika pamoja na mwanawe katika muda aliopanga kunitembelea. Kauli mbiu yangu ni, kwa nini nitumie pesa zangu ikiwa naweza kutumia za wengine?”