Gavana Kahiga amemruka Gachagua?
DALILI zinaashiria huenda Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga amemgeuka kisiasa mwandani wake, aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.
Hii ni kutokana na hatua ya Bw Kahiga kushiriki mikutano ya Rais William Ruto kwenye ziara yake kikazi eneo la Mlima Kenya.
Mwalimu Kahiga, kama anavyofahamika Nyeri, amekuwa rafiki wa karibu wa Gachagua, na alipobanduliwa 2024 Gavana huyo wa ngome yake kisiasa alinukuliwa akirusha cheche za maneno mazito.
Hata hivyo, kwenye ziara ya Rais Ruto Mlima Kenya siku ya kwanza, Jumanne, Aprili 1, 2025, Bw Kahiga aliungana na kiongozi wa nchi na alipopewa mikrofoni eneo la Naromoru, Nyeri kuhutubia umma, Gavana huyo alielezea kuridhishwa kwake na hatua ya Rais kurejea kwa mapochopocho ya maendeleo eneo lililomsaidia kuingia Ikulu 2022.
“Mheshimiwa Rais, tulikukosa kidogo (missed you), tulikuwa tunajiuliza tulikufanyia nini? Hata hivyo, tuna furaha umerejea na mazuri,” Kahiga akasema.
Wiki hii, Rais Ruto ameamba ngoma na hema Mlimani akiahidi kuzindua mseto wa maendeleo, kuanzia miundomsingi, barabara, ujenzi wa nyumba za bei nafuu, hospitali, masoko, kati ya maendeleo mengine.
Gachagua alipoondolewa mamlakani Oktoba 2024 na Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kutia muhuri, Kahiga alinukuliwa akimkashifu Rais Ruto kwa ‘kutumia jamii ya Mlima Kenya vibaya kisiasa.’
Si kisa kimoja, viwili au vitatu, Gavana huyo ameskika akitumia maneno kama “kama mbaya mbaya”, kauli zilizoonekana kuelekezewa kiongozi wa nchi.
Hata hivyo, kwenye ziara ya Ruto eneo la Kati, hii ikiwa ni mara ya kwanza anatua humo baada ya Gachagua kubanduliwa, Kahiga alikiri kupotoka ila sasa amerejea laini baada ya kuona Rais ameukumbuka Mlima kimaendeleo.
“Wajua Mheshimiwa Rais kuna siku ‘inasema kama mbaya mbaya’, lakini tukiona maendeleo, tunasema ni vizuri,” Gavana Kahiga alimwambia Ruto, matamshi yanayofasiriwa kama ishara ya Gachagua kurukwa na mwandani wake.
Akiskika kumrai Rais kukumbuka Mlima Kenya, Kahiga alisema ni haki ya eneo hilo kupata maendeleo sawa na sehemu zingine za nchi, hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi wa 2022 lilimchagua kwa wingi.
“Sisi ndio tulichagua hii serikali na lazima tunufaike nayo,” Kahiga alielezea.
Kati ya kura 7.1 milioni ambazo Ruto alipata kumrithi mtangulizi wake Bw Uhuru Kenyatta, 3.5 milioni zilitoka Mlima Kenya kwa mujibu wa takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Dkt Ruto (Kenya Kwanza) alimenyana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, aliyewania urais kwa tiketi ya Azimio, na ambaye kwa sasa anashirikiana na Ruto sako kwa bako baada ya wawili hao majuzi kutia saini mkataba wa makubaliano, na vilevile kutangaza kuzika tofauti zao kisiasa 2024.
Aidha, Bw Kahiga anamtaka Rais Ruto endapo ana nafasi za hadhi ya juu za ajira serikalini zinazoelea, azielekeze Mlimani.
Kwenye ziara ya Naromoru, Rais Ruto aliandamana na baadhi ya viongozi kutoka Mlima Kenya, akiwemo Naibu wa Rais Profesa Kithure Kindiki, ambaye alimrithi Bw Gachagua, wengine wakiwa; kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichungwah, mbunge wa Nyeri, Anthony Wainaina Njoroge, miongoni mwa wengine.
Wengine walikuwa Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe na mwenzake wa ICT, William Kabogo, ambao waliteuliwa na Rais Ruto Desemba 2024.
Jumatatu jioni, Machi 31, 2025 kwenye mahojiano na vituo vya runinga na redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu, Rais Ruto alidai kuwa Gachagua alitemwa na wabunge kwa sababu ya kuwahangaisha.
Vilevile, kiongozi wa nchi alihoji kuwa wakati mmoja naibu rais huyo wa pili wa Kenya chini ya Katiba ya 2010, alimshinikiza Rais ampe kima cha Sh10 bilioni ili amfanyie kampeni Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, hasa baada ya maandamano ya Gen Z Juni 2024 yaliyotikisa utawala wa Serikali ya Kenya Kwanza.
Vijana walishiriki maandamano ya kitaifa kupinga Mswada tata wa Fedha 2024, ambao baadaye Dkt Ruto aliufuta kutokana na ghadhabu za wananchi.