Makala

GEORGE KIGURU: Nilimeza dawa ya panya kutokana na matokeo duni darasani

December 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

‘MGAAGAA na upwa hali wali mkavu,’ ni methali inayohimiza wanadamu wasiwahi vunjika moyo kwenye jitihada za kutaka kutimiza malengo fulani maishani mwao. Pia imethibitishwa na wengi wanaozidi kushangamkia shughuli tofauti kwenye juhudi za kusaka riziki.

Miongoni mwao ni mwigizaji chipukizi, George Kiguru ambaye amejaa imani kuwa anacho kipaji cha kufanya vizuri katika sekta hiyo na kufikia upeo wa kimataifa miaka ijayo.

”Hakika sitawahi kuweka katika kaburi la sahau kuwa mwaka 2018 nilipofikia uamuzi wa kujitoa uhai ambapo nilikunywa dawa ya panya ili nife nilipogundua siwezi kufanya vizuri darasani,” anasema na kuongeza kuwa kwa sasa amejielewa wala hawezi rudia kitendo hicho tena.

Katika mpango mzima anataka kukuza talanta yake akilenga kufikia kiwango cha waigizaji mahiri duniani kama Michael Gerard Tyson maarufu Mike Tyson ambaye wakati mmoja alikuwa bingwa wa masumbwi duniani.

Bingwa huyo ameshiriki filamu kama ‘The Hangover (2017),’ na ‘Grudge Match,’ kati ya zingine.

Chipukizi huyu anasema ametambua talanta yake imo katika burudani ya maigizo wala sio elimu.

”Nilifikiria kujitoa uhai baada ya wazazi wangu kuibuka kero hasa kunitupia cheche za maneno kwa kutofanya vyema shuleni. Lakini kwa sasa ninapania kuwadhihirishia kuwa bali na masomo naweza kufanya vizuri katika tasnia ya uigizaji.”

Chipukizi huyu amegundua ana talanta katika uigizaji mapema mwaka huu baada ya kushiriki filamu iitwayo ‘Game Changer’ ambayo hupeperushwa kupitia UTV kila wiki.

Chipukizi huyu ni miongoni mwa waigizaji katika filamu hiyo ambayo huzalishwa na kampuni ya Heart Media Services inayomilikiwa na Caroline Njoroge maarufu ‘Ladyheart.

Katika uhusika wake kwenye filamu hiyo yeye ni muuzaji bangi ingawa anasema alikuwa mtumiaji ila aliamua kuacha mapema mwaka huu alipogundua haina msaada kwa maisha yake.

Anaongeza kuwa analenga kuwa mfano mwema kwa wenzie ambao wamekuwa wakishirikiana pamoja kutumia bangi na pombe kati ya maovu mengine katika eneo hilo.

Ingawa ni mwanafunzi wa kidato cha tatu kwenye Shule ya St Joseph’s Riabai inayopatikana katika Kaunti ya Kiambu anasema analenga kusaidia vijana wenzake eneo hilo wabadilike.

”Nataka kukuza talanta yangu ili miaka ijayo nisaidie chipukizi wenzangu wajihepushe dhidi ya matumizi ya mihadarati,” alisema na kuongeza kuwa bangi imefanya apoteze marafiki wake tisa baada ya kuuawa kwa mtutu wa bunduki.

Anadokeza kuwa analenga kuanzisha makundi ya kutoa mafunzo kwa vijana chipukizi (wavulana na wasichana) wenye talanta mbali mbali ikiwamo uigizaji kati ya zingine eneo hilo.

Anashauri chipukizi wenzake wajiamini kwa talanta zao pia wajitume bila kulegeza kamba kwenye jitihada za kupapalia vipaji vyao.