GLADYS MUSAU: Nilianza kuigiza kimzaha lakini sasa mimi ni staa
Na JOHN KIMWERE
MWAKA 2019 aliwika kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutaja kuwa anataka mpenzi ambaye kila siku atakuwa tayari kumpa Sh50,000.
Gladys Mumbi Musau ambaye ni mwigizaji anayeibukia alitaja hayo kwenye kipindi cha Hello Mr Right ambacho hupeperushwa kupitia Rembo TV.
Anaelekea kutimiza ndoto yake maanake tangu akiwa mdogo alitamani kuhitimu kuwa mwalimu, kwani yuko mwaka wa kwanza anakosomea kuhitimu katika taaluma hiyo kwa shahada ya digrii kwenye Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU).
Kando na hayo binti huyu ni afisa wa matangazo wa kampuni ya Debenham ya nchini India ambayo hujihusisha na bidhaa za urembo.
Katika mpango mzima kisura huyu anasema kuwa anatamani sana kuwa mtangazaji mahiri pia mtayarishaji wa kipindi cha burudani kwenye runinga.
”Masuala ya maigizo nilianza kama mzaha muda mchache baada ya kukamilisha masomo ya kidato cha nne mwaka 2018 ambapo nilipata nafasi kushiriki filamu tukitumia mwongozo wa vitabu za riwaya , anasema na kuongeza kuwa baadaye wengi walimshawishi kukamatia uigizaji alionekana ana kipaji.
Binti huyu anayeonekana mwenye umbo la kuvutia anasema alinatamani zaidi kujiunga na masuala ya maigizo alipotazama filamu ya Hollywood, iitwayo ‘Empire’ aliyoshiriki mwigizaji mashuhuri Taraji P. Henson mzawa wa Marekani.
Musau aliyeanza kushiriki uigizaji chini ya kundi la Watamaduni Production anajivunia kushiriki filamu kadhaa chini mwaka mmoja ikiwamo ‘Selina’, ‘The next Superstar,’ ‘Njoro wa Uber,’ ‘Maempress,’ bila kuweka katika kaburi la sahau filamu fupi kwa jina ‘Why you hate,’ ambazo zimepata mpenyo kupeperushwa kupitia Maisha Magic East.
Kadhalika amebahatika kushiriki picha za kutangaza biashara mara mbili na benki ya Equity pia kampuni ya Velvex.
Afrika angependa kushirikiana na wanamaigizo kama Lupita Nyong’o aliye mzawa wa hapa nchini anayetamba kwenye filamu za Hollywood.
Lupita ni kati ya wasanii walioshiriki filamu iliyozoa umaarufu mkubwa iitwayo Black Panther. Duniani bila shaka anasema Taraji P Henson ndiyo nambari wani kabla ya wengine kufuatia.
”Uigizaji unalipa maana wengi wanahutimia kama kitega uchumi na bila shaka serikali inastahili kuhushirikisha katika mtaala wa elimu,” alisema.
Anadokeza kuwa jukwaa la maigizo limefurika changamoto nyingi tu ambazo hufanya baadhi yao wakose ajira. Binafsi anasema maprodusa wengine husema hawezi kuigiza vizuri kutokana na maumbile yake.
Anahimiza wasanii wanaoibukia kwenye gemu kuwa uigizaji siyo mteremko unahitaji nidhamu, kujitolea na kujituma bila kulegeza kamba pia kumtegemea Mungu zaidi.
Pia anawaambia kamwe wasipuuze masomo maana ndiyo msingi wa kila jambo wanalofanya. Anahimiza wanawake wenzake kuwa wanastahili kuvaa vizuri na kujiheshimu ili kujihepusha na wanaume ambao hupenda kushusha wanawake hadhi.