Makala

Hizi ndizo kaunti kidedea kwa maendeleo

Na  ERIC MATARA September 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Ni kaunti 12 kati ya 47 pekee zilizorekodi utendaji bora kwa kuwekeza zaidi ya asilimia 70 ya bajeti katika miradi ya maendeleo mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Kwa jumla, kaunti hizo 12 zilitumia Sh 35.2 bilioni kati ya Sh 123.76 bilioni zilizotumiwa na kaunti zote katika shughuli za maendeleoKulingana na Ripoti ya Utekelezaji ya Serikali za Kaunti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 iliyotolewa na Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang’o, kaunti za Nandi, Trans Nzoia, Narok, Meru, Kericho, Mandera, Kirinyaga, Makueni, Marsabit, Murang’a, Samburu na Wajir ndizo zilizo na viwango vya juu kabisa vya matumizi ya fedha za maendeleo.
Ripoti ya hivi karibuni inaonyesha kuwa Nandi iliongoza kwa asilimia 90, Trans Nzoia (asilimia 77), Narok (asilimia 74), Meru (asilimia 73), wakati Kericho, Mandera na Kirinyaga zote zilikuwa na asilimia 72. Kaunti za Makueni, Marsabit, Murang’a, Samburu na Wajir pia zilimaliza orodha na asilimia 71 kila moja.
“Katika kipindi kilichochunguzwa, serikali zote za kaunti zilitumia Sh 123.76 bilioni kwa shughuli za maendeleo, kikiwakilisha kiwango cha asilimia 57 ya bajeti ya maendeleo ya  mwaka ya Sh 218.99 bilioni,” sehemu ya ripoti hiyo inasema.
Hii ina maana kaunti zilitumia Sh 346.98 bilioni (asilimia 74), ya jumla ya Sh 470.74 bilioni zilizotengwa kwa matumizi ya mara kwa mara — na kutumia tu Sh 123.76 bilioni (asilimia 26) kwa maendeleo, kwa mwaka mzima.
Kwa kulinganisha na mwaka uliopita, 2023/2024, matumizi ya shughuli mara kwa mara yalipanda kwa Sh 10.98 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Ripoti inaonyesha pia kuwa Nandi ilitumia Sh 3.3 bilioni kwa maendeleo kati ya bajeti ya maendeleo ya Sh 3.6 bilioni, wakati Trans Nzoia ilitumia Sh 3.4 bilioni kati ya bajeti ya maendeleo ya Sh 4.34 bilioni.
Kwa upande wake, Narok ilitumia Sh 3.96 bilioni kati ya Sh 5.3 bilioni zilizotengwa kwa maendeleo mwaka huo, Meru ilitumia Sh 2.8 bilioni, Kericho (Sh 2.6 bilioni), Mandera (Sh 4 bilioni), Kirinyaga (Sh 2.1 bilioni), Makueni (Sh 2.6 bilioni), Marsabit (Sh 3 bilioni), Murang’a (Sh 2.3 bilioni), Samburu (Sh 1.5 bilioni) na Wajir (Sh 3.6 bilioni). Hizi ndizo kaunti zilizomaliza orodha ya zile zilizotumia pesa zaidi kwa maendeleo katika kipindi hicho.
Kinyume chake, kaunti zilizotumia kiwango cha chini kwa  maendeleo zilikuwa Kisii (asilimia 40), Elgeyo Marakwet (39), Kiambu na Nyamira (37), na Kisumu na Jiji la Nairobi kwa asilimia 29.
Kwa mfano, utawala wa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja; ulitumia Sh 4 bilioni tu kwa maendeleo kati ya bajeti ya maendeleo ya Sh 14.2 bilioni, huku Gavana Simba Arati akitumia Sh 2.4 bilioni kati ya bajeti ya maendeleo ya Sh 6.1 bilioni.
Hata hivyo, Sh 4 bilioni zilizotumia na Gavana Sakaja kwenye miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2024/25 ilikuwa ongezeko ikilinganishwa na Sh 2.72 bilioni katika mwaka wa 2023/24 — ikionyesha ongezeko la asilimia 50.6.
“Jumla ya matumizi na serikali za kaunti katika mwaka wa fedha 2024/2025 ilikuwa Sh 470.74 bilioni, ikiwakilisha kiwango cha jumla cha utumiaji cha asilimia 78 ya bajeti ya serikali za kaunti ya Sh 601.69 bilioni,” ripoti inaendelea.