Kuria aona mwanga, akiri dhambi za Mlima kwa Raila na babake
KIONGOZI wa Chama cha Kazi ambaye alikuwa Mshauri Mkuu wa masuala ya uchumi wa Rais William Ruto, Moses Kuria, anaonekana kuona mwanga mpya uliomwezesha kuomba msamaha wakazi wa eneo la Nyanza kwa dhambi za kisiasa za Mlima Kenya.
Kwa niaba ya eneo la Mlima Kenya, Bw Kuria alimaliza mwaka jana kwa kuomba msamaha wakazi wa Nyanza kutokana na mashambulizi ya kisiasa yaliyodumu kwa miongo kadhaa na hadithi zilizogawanya wakazi wa maeneo hayo zilizolenga Marehemu Jaramogi Oginga Odinga na mwanawe, marehemu Raila Odinga.
Kuria alielezea hisia zake kupitia akaunti yake rasmi ya X mnamo Jumatano wiki hii akijikita katika historia ya kisiasa ambayo ilifanya familia ya Odinga ionekane kama maadui wa Mlima Kenya katika kampeni za kisiasa.
“Kwa miaka 60, Wakikuyu walikuwa wakiuziwa picha ya shetani kwa jina la Jaramogi Oginga Odinga na Raila Odinga. Hii ilifaulu kama silaha ya kisiasa. Baada ya yote, kanisa linaweza kuishi bila malaika lakini haliwezi kuishi bila shetani wa kupigana vita. Lilikuwa kosa,” alisema Kuria.
Alisisitiza kuwa alitoa msamaha huo kwa nia njema, akisema kuwa uhasama wa zamani wa kisiasa haupaswi kuendelea kugawanya jamii.
“Kwa niaba ya jamii ya Wakikuyu na watu wa Mlima Kenya kwa jumla, ninaomba radhi kwa jamii ya Waluo.
“Wakati huo huo, makosa mawili hayawezi kurekebisha hali. Uhuru Kenyatta na Wakikuyu si maadui wa Waluo. Msiruhusu tutumike kama chombo cha kisiasa. Hatufai kudumisha hadithi hii ya kishetani kwa miaka mingine 60,” aliongeza Bw Kuria.