JAMVI: Ishara huenda Uhuru asiondoke mamlakani 2022
Na WANDERI KAMAU
HUENDA Rais Uhuru Kenyatta akakosa kung’atuka uongozini hata baada ya mwaka 2022, wachanganuzi wakitaja ukosefu wa kiongozi ambaye atajaza pengo lake la kisiasa kitaifa na ukanda wa Mlima Kenya.
Miongoni mwa sababu zinazotajwa ni hatua ya Rais kutomtaja mrithi wake maalum wa kisiasa kutoka familia yake na miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliopo wanaoonekana kupigania nafasi ya kumrithi baada ya kipindi chake kukamilika.
Baadhi ya viongozi wa kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya wamekuwa wakiendesha juhudi za kichinichini kujinadi kama warithi wa Bw Kenyatta, ila hilo limeonekana kutombabaisha hata kidogo.
Wale wanaopigiwa upatu kuwa warithi wa Bw Kenyatta ni magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Mwangi wa Iria (Murang’a), Francis Kimemia (Nyandarua), Peter Kenneth kati ya wengine.
Hata hivyo, wachanganuzi wanasema kuwa kimya cha Rais kuhusu siasa za urithi na agizo kwa viongozi wa Jubilee kuacha siasa za urithi ni ishara tosha kwamba hayuko tayari kung’atuka.
“Kimya cha Rais Kenyatta kuhusu hatima yake baada ya 2022 kinaashiria mengi, moja likiwa hajapata mrithi maalum anayeweza kujaza pengo atakaloliacha ikiwa atastaafu kutoka ulingo wa kisiasa. Hii ni dalili ya wazi inayoonyesha uwezekano mkubwa wake kuendelea kuhudumu serikalini hata ikiwa hatawania urais,” asema Ndegwa Njiru, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Kulingana na wachanganuzi, anayeonekana kuwa mrithi wa Rais katika familia ya Kenyatta ni mwanawe, Muhoho Kenyatta, ila wakimkosoa kuwa “ana ulimbukeni mkubwa katika ulingo wa kisiasa.”
“Dalili zote zimeonyesha Rais anampendelea Muhoho kama mrithi wake, ila kilicho wazi ni kwamba hana baadhi ya sifa kama ufahamu kamili wa lugha ya Gikuyu, kwani amelelewa katika mazingira ambayo hakushuhudia wala kuingiliana na Wakenya wa kawaida. Hii ni kinyume na Rais mwenyewe ambaye ana ufahamu mpevu wa lugha hiyo na Kiswahili,” asema Bw Njiru.
Mnamo 2017, Muhoho alikumbwa na ugumu kujieleza kwa lugha ya Kiswahili, alipozuru katika Kaunti ya Uasin-Gishu akiwa ameandamana na Naibu Rais William Ruto. Ilibidi awahutubie wananchi kwa kusoma ujumbe ulioandikwa kwenye simu yake kwa lugha ya Kiswahili.
Kwa hayo, Bw Oscar Plato, ambaye ni mchanganuzi anasema kuwa licha ya dalili zote kuonyesha kwamba Rais Kenyatta anampendelea Muhoho, “anahitaji mafunzo mengi ya kisiasa”.
“Mojawapo ya dalili za Rais kutoonyesha ishara za kutong’atuka ni mbinu ya kumtayarisha mwanawe kwa nafasi kubwa zaidi, wakati ambapo hatimaye atajiondoa uongozini,” asema.
Wanasema kwamba Rais Kenyatta analenga kutumia mbinu aliyotumia Rais Mstaafu Daniel Moi kumwandaa kwa uongozi wa kitaifa, alipompendekeza kama mwaniaji urais wa KANU mnamo 2001.
“Baada ya kumtangaza Bw Kenyatta kama mwaniaji wa Kanu, Moi aliwashtua wengi. Hata hivyo, walilosahau ni kwamba Mzee Moi alikuwa akimwaandaa Bw Kenyatta kutwaa nafasi hiyo kwa muda mrefu,” asema Bw Plato. Sawa na hivyo, anatabiri kwamba huenda Bw Kenyatta akamtangaza Muhoho kama mrithi wake katika muda ambao atawaacha wengi kwa mshangao.
Mbali na hayo, wachanganuzi wanataja midahalo ya maandalizi ya kura ya maoni kama ishara nyingine inayoonyesha kwamba huenda Rais Kenyatta akaendelea kuhudumu hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Kulingana nao, agizo la Rais kwa viongozi wote kukoma kuendeleza siasa za 2022 ni ishara kwamba kuna mikakati ya kichinichini inayoendelea kuandaliwa ili kugeuza mfumo wa utawala nchini.
Hatua yake ya kubuni muafaka wa kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga inatajwa kama mkakati wake wa kutoa mazingira matulivu ya kuandaa mikakati ya urithi wake kwa njia itakayohakikisha kwamba bado anaendeleza ushawishi wake serikalini hata ikiwa atakuwa nje.
“Tamko la Rais kwamba uamuzi wake ‘utawashangaza wengi mnamo 2022 linapaswa kuchukuliwa kwa uzito. Ni tamko ambalo limejaa fasiri nyingi ambazo zingali siri kwa wengi. Ni kauli ambayo haiondoi uwezekano wa Rais mwenyewe kuendelea kuhudumu au kumtaja mrithi atakeyewaacha wengi kwa mshangao,” asema Kiprotich Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Kumekuwa na midahalo inayomtaja Peter Kenneth kama mrithi anayeandaliwa kumrithi Rais, ila wachanganuzi wanaeleza kuwa mapema kutoa utabiri huo.
“Kufikia sasa, ingekuwa dhahiri ni nani ambaye Rais Kenyatta anapendelea kuwa mrithi wake wa kisiasa. Hata hivyo, ni fumbo ambalo lingali kufumbuliwa hadi sasa,” asema Bw Mutai.
Baadhi ya wataalamu wa kisiasa wamekuwa wakieleza kwamba mpango wa Rais Kenyatta ni kushinikiza mageuzi ya kikatiba ambayo yatabuni nafasi zaidi ambapo atahudumu kama Waziri Mkuu ama Naibu Rais, ama jinsi Rais Vladimir Puttni wa Urusi, ambaye awali alihudumu kama Waziri Mkuu chini ya Rais Dmitri Medvedev.
“Hili ni fumbo kuu ambalo atakayetoa jibu ni Rais Kenyatta mwenyewe. Ila ilivyo kwa sasa, hakuna dalili zozote za yeye kung’atuka uongozini vivi hivi tu,” asema Bw Mutai.