MakalaSiasa

JAMVI: Ishara Uhuru atamrithisha Raila urais wala si naibu wake Ruto

June 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

HUKU kauli moja kuu ya kisiasa ikiwa ni kuwa “yote yawezekana bora tu yapangwe vizuri”, kuna wasiwasi mkuu kuwa Rais Uhuru Kenyatta amezindua njama kali ya kumshinikiza Naibu wa Rais William Ruto ang’atuke na badala yake, Raila Odinga ateuliwe katika wadhifa huo.

Mhadhiri wa somo la kisiasa, Gasper Odhiambo anasema kuwa uwezekano wa kuwapo kwa njama hii unatokana na ushahidi wa kiusemi wa Rais mwenyewe.

“Rais Kenyatta amesikika hadharani akimsuta naibu wake kama aliye na mazoea ya kutangatanga. Amesikika si mara moja akisema kuwa mpango wake wa sasa kuhusu 2022 utashtua wandani wake ndani ya Jubilee aliokuwa amewaelekeza mbeleni kuwa atahudumu kwa miaka 10 na kisha amkabidhi Dkt Ruto miaka 10. Hali ya kushtua inawezekana tu kwa kumpa Ruto talaka,” asema.

Aidha, anasema kuwa hivi majuzi akiwa katika kongamano la dhehebu la Akorino ambapo Rais alitangaza kuwa “hamtanizuia kufuata ile barabara mimi nimejitengenezea ya kupeleka watu wetu (Jamii za Mlima Kenya) kwa manufaa halisi ya amani kwa miaka 50 ijayo,” Odhiambo akisema kuwa hii ni ishara tosha kuwa Ruto hayuko katika hesabu ya Rais kuhusu 2022.

Aidha, hatua ya Rais Kenyatta kutangaza kuwa “sio ninyi mlinisaidia kutwaa urais bali mimi ndimi niliyewasaidia kupata nyadhifa hizo ina maana kuwa Naibu Rais alipata wadhifa huo kwa kuwa Rais alimkubali awe mgombezi mwenza.”

Matamshi ambayo Bw Odhiambo anashikilia kuwa ni msumari wa mwisho kwa jeneza la Dkt Ruto ni kuwa “Mimi nimechoka na hii takataka mnayoita wanasiasa na nitawang’oa kutoka nyadhifa hizo mlizonazo.”

Masaibu haya yote kwa Ruto yalitokana na hatua ya Rais Kenyatta kusalimiana na Odinga katika hali ya Hendisheki na inasemwa kuwa yamezua kila aina ya changamoto kwa Dkt Ruto na ndiyo sababu anapambana kufa kupona kujinusuru, kiasi cha kutangaza kuwa kuna njama ya kumuua.

Ni hali ambayo imempata Dkt Ruto akisemwa kwa idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) na katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Bw Karanja Kibicho, hali ambayo inazidisha presha katika maisha yake kama msaidizi wa Rais Kenyata.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa “katika somo la siasa, uvumi huwa sio wa ukweli hadi wakati ule utakapokanushwa na walio ndani ya uvumi huo.”

Katika hali hiyo, kuwa wanaosemwa kupanga kumuua Naibu Rais, mawaziri Peter Munya, Sicily Kariuki, Joe Mucheru na James Macharia, wakiwa wamekanusha, wadadisi wanasema kuwa inaweza kuwa sio mauti kwa Ruto yanayopangwa bali ni mauti kwa unaibu wake wa urais.

Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro anasema kuwa “kuna habari za kuaminika kuwa kuna njama ya kumng’atua Dkt Ruto kutoka unaibu wa urais lakini wanaopanga njama hizo wanalemewa kwa kuwa katiba itazua utata na pia kutakuwa na athari mbaya za kisiasa kutoka kwa wafuasi wa Ruto.”

Anasema mbinu ambayo inatumiwa ni ya “kumdunisha Ruto kama mtu fisadi, asiye wa kuaminika na ambaye hana uwezo wa kuongoza taifa ambalo linasaka umoja wa kijamii.”

Bw Nyoro anasema kuwa “njama hizo zote zimezinduliwa huku Naibu Rais akizitibua kutokana na weledi wake wa kisiasa na wa kuwa na mitandao ya kina ya kumkusanyia ujasusi wa yale yanayopangwa.”

Mbunge wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri anasema Bw Raila alikuwa, mwaka jana, amedokeza kuwa alikuwa na nia ya kumng’atua Ruto kutoka ushawishi wa kurithi Ikulu 2022.

“Alionya kuwa Ruto hakuwa na uwezo wa kurithi ikulu bila mchango wake (Odinga). Alionya kuwa alikuwa ameandaa mbinu ya kuingia katika hesabu ya urithi ndani ya serikali na ndipo salamu hizo za maridhiano zilishikishwa kasi na kuanzia wakati huo Rais akaonekana kujitenga na afisi ya naibu wake,” asema Bw Ngunjiri.

Anasema kuwa hadi sasa “hizi salamu kati ya Rais na Odinga zimekuwa za kupiga vita wote ambao walikuwa viungo muhimu katika ushindani wa kisiasa na kuishia kumuidhinisha Uhuru kutwaa mamlaka ya uongozi.”

Asema, “Tangu salamu hizi ziingie, Rais anaonekana waziwazi kuongoza njama kali za kumzima Ruto. Amekuwa akitangaza sera zinazoonyesha waziwazi kuwa zinamlenga Ruto. Inaonekana kuwa kuna mwanya unaosakwa kwa hila na njama ya ama Ruto ahujumiwe hadi ajiuzulu au kuzuke msingi thabiti wa kumng’atua au kupitia jopo maalum au kufutwa kazi moja kwa moja.”

Bw Ngunjiri anasema shida kubwa ni kuwa “ndani ya bunge kuna wingi wa ufuasi kwa Ruto na pia katika jumuia ya wapiga-kura, anabakia akiwa na ufuasi mkuu na ambao unatatiza njama hizo kutimizika.”

Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu anasema kuwa “nimekuwa nikiandamwa na wandani wa upinzani kwa Ruto nikiahidiwa kulegezewa presha za kuandamwa na kesi na shutuma katika kaunti yangu ikiwa nitaachana na mrengo wa urithi wa Ruto 2022.

Anasema “wale ambao wamekuwa wakinifuatafuata wakinipa shinikizo hizo ni wakuu katika serikali na ambao nia yao hawaifichi kwa kuwa wananiambia waziwazi kuwa masaibu yangu yanatokana na ufuasi kwa Ruto.”

Anadai kuwa amepewa mfano wa mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria “ambaye baada ya kuhama mrengo wa Ruto na kutangaza kuwa alikuwa amejitenga na kampeni za 2022 kwa manufaa ya DP, basi kesi yake mahakamani kuhusu uchochezi ilifutiliwa mbali.”