MakalaSiasa

JAMVI: Kibarua kigumu kwa Ruto kuokoa jahazi la Jubilee linalozama

March 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto huenda akawa na kibarua kigumu ‘kufufua’ chama cha Jubilee ambacho kinaonekana kutelekezwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Chama cha Jubilee kimeanza kuonyesha dalili za kusambaratika licha ya viongozi wake kushikilia kuwa kingali imara.

Wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Naibu wa Rais wamekuwa wakishinikiza kujiuzulu kwa viongozi wa sasa wa Jubilee, akiwemo Katibu Mkuu Raphael Tuju.

Wandani wa Dkt Ruto wanadai kuwa viongozi wa sasa wa Jubilee wanahujumu juhudi za naibu wa rais kutaka kuingia Ikulu baada ya Rais Kenyatta kustaafu 2022.

Mzozo unaoendelea kutokota ndani ya Jubilee imesababisha chama hicho kusitisha mpango wake wa kufungua afisi za chama katika kaunti zote 47.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa pia wanaonya kuwa uchaguzi wa viongozi wote kuanzia mashinani hadi ngazi ya kitaifa mwaka ujao huenda ukagonga mwamba iwapo mvutano uliomo chamani hautatafutiwa ufumbuzi upesi.

Chama cha Jubilee kinapanga kuandaa uchaguzi wa viongozi wake, muda wa kuhudumu wa viongozi wa muda utakapokamilika 2020.

Dkt Ruto, hata hivyo, ameshikilia kwamba chama cha Jubilee kingali imara na atakitumia katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Alipokuwa akimpokea mwaniaji wa ubunge wa Wajir Magharibi Ahmed Kolosh aliyegura ODM na kujiunga na Jubilee, Naibu wa Rais Ruto alionnekana kudokeza kwamba angali na nia ya kuhakikisha kuwa chama cha Jubilee kinaendelea kuwa imara.

Dkt Ruto aliyekuwa ameandamana na Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale na Bw Tuju alisema kuwa chama cha Jubilee kimejitolea kwa hali na mali kushinda kiti cha Wajir Magharibi.

“Chama cha Jubilee kitashiriki katika uchaguzi wa Wajir Magharibi kwa kutumia sera na masuala yanayohusu wananchi,” akasema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais anatarajia kutumia chama cha Jubilee kuwania urais 2022 licha ya kuwepo na shinikizo za kumtaka kuuunda chama kipya.

Kulingana na Felix Otieno, ikiwa Dkt Ruto ataunda chama kipya sasa huenda akapoteza kiti cha unaibu rais kwa sababu alichaguliwa pamoja na Rais Kenyatta kwa kutumia .

“Mbali na kuwepo na shinikizo za kumtaka kujiuzulu, itakuwa vigumu kwa chama hicho kipya kupata uungwaji mkono kabla ya 2022,” anasema Bw Otieno.

Hata hivyo, Bw Otieno anasema kuwa Naibu wa Rais atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha kuwa chama cha Jubilee kinaendelea kuwa na ushawishi nchini hadi 2022.

Tangu kuchaguliwa kwa muhula wa pili mwaka jana, Rais Kenyatta amesalia kimya kuhusu hatima ya Jubilee, hatua ambayo imezua hali ya hofu miongoni mwa wanachama.

Kadhalika, Rais Kenyatta haijaitisha kikao na wanachama wa Jubilee ili kuwaelezea kuhusu hatua yake ya kutia mkataba wa ushirikiano na kinara wa ODM Raila Odinga.

Kongamano la viongozi wa Jubilee lilofaa kufanyika Naivasha mnamo Julai mwaka jana mjini Naivasha liliahirishwa na kulingana na Bw Tuju halitafanyika hivi karibuni.

Naibu wa Rais pia anakabiliwa na upinzani na baadhi ya viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya, haswa wanasiasa waliopoteza katika uchaguzi uliopita.

Mwezi uliopita kundi la viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na Maina Kamanda (Maalumu), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Paul Koinange (Kiambaa), Muturi Kigano (Kangema), Naomi Shaban (Taveta) waliwataka wanasiasa wanaompigia debe Dkt Ruto kuhama Jubilee.

Kulingana na wabunge hao, wanasiasa hao hawana heshima kwa Rais Kenyatta ambaye amewataka wanasiasa wa Jubilee kujiepusha na kampeni za mapema za uchaguzi ujao wa 2022.

“Ikiwa wanasiasa hao wanaotembea na naibu wa rais wanadhani kwamba anaweza kuwasaidia wajiuzulu kutoka Jubilee na wawanie tena kwa kutumia vyama tofauti,” akasema aliyekuwa mbunge wa Dagoreti Kusini Dennis Waweru.

Kulingana na mhadhiri wa siasa Prof Macharia Munene, endapo kutakuwa na kura ya maamuzi basi vyama vipya huenda vikajitokeza na huo huenda ukawa mwisho wa Jubilee.

Rais Kenyatta na Bw Odinga wanataka kufanywa kwa kura ya maamuzi ili kupanua serikali na kujumuisha jamii zote.

Dkt Ruto, hata hivyo, anapinga vikali kwa kusema kuwa hataruhusu katiba kufanyiwa mabadiliko ili kuongeza vyeo.

“Naibu wa Rais amejitokeza na kusema kuwa atapinga rasimu ya katiba endapo vipengee vya kubuni nyadhifa zaidi vitaingizwa. Hiyo inamaanisha kwamba huenda akawa upande tofauti na Rais Kenyatta,” anasema Prof Munene.

“Ikiwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto watakuwa katika mirengo tofauti wakati wa kampeni za kutaka kubadilisha katiba, basi huo utakuwa mwisho wa Jubilee,” anaongezea.