Barua isiyo ya kawaida ya Raila kwa Ruto
WAZIRI Mkuu wa zamani, Raila Odinga, amethibitisha dhamira yake ya kushirikiana kisiasa na Rais William Ruto katika barua mpya ambayo inaashiria mabadiliko makubwa katika siasa za Kenya.
Barua hiyo aliyoandika Machi 3 – ambayo Taifa Leo iliipata jana – inaeleza kwa kina juhudi za kipekee ambazo Rais na serikali yake walifanya katika jaribio la kumwezesha Odinga kupata uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), ambao alishindwa na Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti mnamo Februari 15. Barua hiyo iliwasilishwa rasmi Machi 4.
Upekee wa barua hiyo unaashiria umuhimu wake kama msingi wa maridhiano yao, ambayo yalihalalishwa Machi 8 wakati chama cha Odinga cha ODM kilipotangaza kuunga mkono shughuli za serikali.
“Mheshimiwa Rais, natambua kuwa sasa unashikilia wadhifa ndani ya Tume ya Muungano wa Afrika ukihusika kuifanyia mageuzi taasisi hiyo. Nina imani kwamba utakabiliana na changamoto zilizopo na ninakuhakikishia msaada wangu wa dhati. Ninaahidi kushirikiana nawe na uongozi mpya wa Muungano wa Afrika ili kutimiza ndoto za waasisi wetu,” aliandika Odinga, akisema kushindwa kwake kama fursa ya mshikamano badala ya pigo la kisiasa.
Ahadi hii ya Odinga ya “uaminifu” kwa Ruto, ambayo imewakera baadhi ya wafuasi wake, pamoja na umri wake mkubwa, imesababisha uvumi kuwa huenda anaweka mazingira ya kumsaidia Rais Ruto kuelekea uchaguzi wa urais wa 2027.
Muungano mpya wa upinzani unamhimiza Odinga kujiondoa kwenye makubaliano yake na Rais Ruto ili kulazimisha mabadiliko ya utawala. Hata hivyo, chama chake cha ODM kinajiepusha na msimamo wa wazi kuhusu jambo hilo, kikisema kuwa kitaamua hatma yake uchaguzi ukikaribia, na kwamba maamuzi makubwa kama hayo lazima yaidhinishwe na vyombo vya chama. Vyombo hivyo- kamati kuu za chama, hufuata matakwa ya Odinga kila wakati.
Katika siku ambayo walitia saini makubaliano ya kushirikiana, Rais Ruto alimpongeza Odinga – mtu ambaye walikuwa wapinzani wakubwa katika kampeni za uchaguzi uliopita.
“Watu wachache sana wanaweza kuweka maslahi ya wananchi mbele ya maslahi yao binafsi. Kaka yangu Raila, historia itakutendea haki. Miezi michache iliyopita, nilimpigia Raila simu nikamwambia: Umewahi kuwa kiongozi wangu wa chama, na leo, kwa neema ya Mungu, mimi ni Rais. Nataka uheshimiwe Kenya,” alisema Rais Ruto kuhusu Odinga.
“Na nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba unaheshimiwa. Mchango wako kwa Kenya unastahili heshima na msaada.”
Viongozi hao wawili, waliokuwa mahasimu wakubwa katika uchaguzi wa urais wa 2022 uliogawanya Kenya kwa misingi ya kikabila na kimaeneo, sasa wamesimama kama washirika wa kushangaza, makubaliano yao yakiwa jaribio la kuthubutu kuponya taifa ambalo bado linapona majeraha ya maandamano makali ya kupinga ushuru mnamo Juni 2024.
Barua hiyo inatoa mtazamo wa nadra kuhusu kampeni ya hali ya juu ya Ruto kusaidia Raila kunyakua wadhifa wa AUC, ambayo ilikuwa mojawapo ya mikakati yake mikuu ya utawala baada ya mgogoro wa mwaka jana, kwa lengo la kurejesha utulivu nchini.
Katika kampeni yake ya AUC, Ruto alihusisha maafisa wa serikali wa kiwango cha juu, alifanya ushawishi binafsi kwa viongozi wa mataifa ya Afrika, na kuwatumia maafisa wake wakuu— Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Wizara ya Masuala ya Nje, na mkuu wa idara ya ujasusi Noordin Haji kwa mawasiliano ya siri.

Ushirikiano wa Ruto na Odinga ni sehemu ya mkakati mpana wa baada ya mgogoro wa Juni ili kuhakikisha uthabiti wa kitaifa, mkakati ambao pia unajumuisha juhudi za kumshirikisha aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, ishara ya upatanisho wa viongozi wa juu ili kuzima joto la kisiasa nchini.
“Msaada wako wa mapema na wa dhati kwa azma yangu uliniwezesha kuendeleza kampeni yangu kwa nguvu. Uliweka Serikali ya Kenya nyuma yangu. Usaidizi wa kimaadili na kifedha ulionipa ulinipa motisha kubwa,” anaandika Odinga.
Odinga pia anakiri, rasmi, kuwa Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ilihusika moja kwa moja katika kampeni yake ya AUC, labda akisisitiza jinsi serikali ilivyokuwa makini kuhusu nafasi hiyo ya bara Afrika.
“Mheshimiwa Rais, ulitembelea marais wengi wa Afrika na ukapiga simu nyingi kwa niaba yangu. Uliniwekea maafisa wa juu wa serikali, wakiwemo Mkuu wa Mawaziri, Mheshimiwa Musalia Mudavadi, na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kitaifa ya Ujasusi, Bw Noordin Haji,” Odinga anaandika, akionyesha juhudi za Ruto za kutafuta uungwaji mkono.
Lakini kushindwa kwake AUC, ambako wakosoaji kama Kalonzo Musyoka wanautaja kama matokeo ya makosa ya kidiplomasia ya Ruto, kunaweza kuonekana kama pigo la kisiasa. Hata hivyo barua ya Odinga inajaribu kubadilisha kuwa wito wa mshikamano kwa ushirikiano wao mpya, kama daraja la kuziba ufa wa uchaguzi wa 2022 na athari za maandamano ya Juni 2024 ambayo yalisababisha vifo vya watu kadhaa na kufichua udhaifu wa utawala wa Ruto.
Nguvu ya Odinga katika siasa za Kenya inamfanya kuwa sehemu muhimu ya mpango huu wa uthabiti wa kitaifa, jambo lililoangaziwa na rekodi yake ndefu ya kisiasa na mtazamo wa matumaini wa barua hiyo. Tayari, anafaidika na ushirikiano huu, kwani Rais ameteua washirika wake kadhaa kuwa Makatibu, wakisubiri kuidhinishwa na Bunge.
Hata hivyo, ushirikiano huu unakabiliwa na upinzani mkubwa: Wafuasi wa Odinga wanahisi amewasaliti kwa kumuunga mkono adui wa zamani, huku washirika wa Ruto ndani ya Kenya Kwanza wakihofia kudhoofika kwa ajenda yao.
Hatima ya ushirikiano huu itategemea iwapo utazaa matunda halisi kwa wananchi au utaishia kuwa mkataba wa kisiasa usio na maana.