Jamvi La Siasa

Dalili upinzani unatupa nyota ya 2027

Na BENSON MATHEKA December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MIKUTANO miwili ya makundi tofauti ya vinara wa upinzani Alhamisi wiki hii imetoa taswira kwamba muungano wanaosuka kumkabili Rais William Ruto 2027 huenda ukawa hewa, huku dalili za mpasuko zikiwa wazi licha ya kauli zao zinazosisitiza umoja.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka aliongoza mkutano wa vinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua, Eugene Wamalwa wa DAP- Kenya na Justin Muturi wa DP uliofanyika katika Chui House, Nairobi, huku naibu kiongozi wa Jubillee Dkt Fred Matiang’i na Martha Karua wa PLP wakiongoza kikao kingine cha faragha walichosema ni kupanga mikakati na kutia nguvu upinzani.

Kikao hicho cha Matiangi pia kilihudhuriwa na Peter Munya, Ukur Yatani, Lenny Kivuti, James Magara na msemaji wa muungano wa upinzani Mukhisa Kituyi.

Ingawa vinara hao wa upinzani wamekuwa wakikanusha madai ya mgawanyiko, mfululizo wa matukio na matamshi yao wenyewe katika siku za hivi majuzi hasa baada ya chaguzi ndogo za Novemba 26 yamefanya wafuasi wao kutilia shaka umoja wao.

Kikao cha kundi la Bw Musyoka katika makao ya DAP-K, Chui House, kilitarajiwa kuonyesha umoja wa vinara wa upinzani katika kukosoa serikali. Kundi hilo lilionya kwamba utawala wa sasa unahatarisha uhuru na taasisi za taifa na kushambulia kwa ukali mwenendo wa Tume Huru ya Uchaguzi, wakisema chaguzi ndogo za Novemba 26 “zilikuwa za aibu.”

Ingawa walipuuza tetesi kwamba kukosekana kwa Dkt Matiangi na wenzake kuliashiria mgawanyiko katika muungano wao, Dkt Kituyi ambaye ni msemaji wao alinukuliwa akisema kwamba baadhi ya vinara “waliamua kukwepa mkutano bila hata kuomba radhi.”

Kauli hii inatofautiana na ya Bw Wamalwa, aliyesoma taarifa rasmi katika Chui House akisema baadhi ya wenzao waliokosa kuhudhuria waliomba radhi na kutuma wawakilishi.

“Chukulia hayo kama uvumi. Tumeungama na tuko na lengo moja. Mtakumbuka tulipoanza Januari 27, baadhi hawakuwa—lakini walituma wawakilishi. Leo pia wametuma wawakilishi. Tuko imara,” alisema. alisema.

Dkt Matiang’i alisema mkutano wa faragha wa kundi lake ulikuwa wa kuimarisha umoja, muundo na mkakati wa upinzani.

Kupitia ujumbe wake katika X, alisema Dkt Matiangi alisema majadiliano yao yalilenga kuimarisha upinzani kwa kuzingatia azma yao thabiti ya kurejesha uongozi bora nchini.

Bi Karua aliongeza maneno ambayo yalizua maswali zaidi akionekana kuunga kauli za Dkt Kituyi. “Huu ulikuwa mkutano uliopangwa kwa pamoja na kukubalika na wote, tafadhali tambua hilo,” alisema kupitia X.

Wachanganuzi wa siasa wanaona dalili zote za muungano huo kuporomoka hata kabla ya safari ya 2027 kuanza.

Mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema licha ya kauli za viongozi hao wa upinzani kuonyesha wangali wameungana, ishara wanazowasilisha kwa umma ni kuwa kuna mvutano kati yao. “Hauwezi kujenga muungano kwa taarifa mbili zinazotoka siku moja kutoka sehemu tofauti. Huo ni mgawanyiko,” alisema.

Naye Bi Dolly Ndirangu, mchambuzi wa utawala na miungano ya siasa, anasema tatizo ni ubabe katika kusaka mgombea mkuu anayeungwa mkono na wote.

“Hakuna kinara anayeonekana kuwa ‘nyota’ au chaguo la wote. Hiki ndicho chanzo cha misuguano midogo midogo inayojitokeza. Bila mwelekeo mmoja, upinzani unaweza kuyeyuka kabla ya 2027,” Ndirangu anaeleza.

Anasema kuwa kundi la Kalonzo linaonekana kuwa sura ya muungano; wakati Karua na Matiang’i wanaonekana kuunda mrengo mbadala unaotaka kuamua mwelekeo wa upinzani.

Hii, anasema, itawakosesha nguvu za kukabiliana na Rais Willam Ruto ambaye amejipanga kushinda atawale kwa muhula wa pili 2027.

“Watakuwa wametupa nyota ya kumshinda Rais Ruto ambaye akiwa mamlakani ana nguvu na mikakati bora. Tofauti za nani atapeperusha bendera au ni nani atakuwa nini hazifai kwa sasa. Ni wakati wa kuamua kuunga mmoja na kuweka nguvu na rasilmali za pamoja iwapo wanataka kuondoa utawala wa sasa debeni 2027,” alisema Ndirangu.

Dkt Gichuki anasema mvutano huu unaweza kuwa umezidishwa na kauli zao baadhi ya vinara baada ya chaguzi ndogo zilizoashiria wana misimamo kuhusu mgombea urais na kukubaliana kutengea vyama maeneo fulani katika uchaguzi mkuu wa 2027.