Jamvi La Siasa

Fahamu kwa nini kujiuzulu kwa balozi Meg Whitman si habari njema kwa Kenya

Na CHARLES WASONGA November 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUJIUZULU kwa Balozi wa Amerika nchini Meg Whitman wiki moja tu baada ya Donald Trump kuibuka mshindi katika uchaguzi wa urais sio habari njema kwa Kenya.

Wadadisi wanasema kuwa hatua hiyo ni kiashirio kuwa manufaa ambayo Kenya imepata kutokana na ukuruba kati ya Rais wa Amerika anayeondoka Joe Biden na Rais William Ruto yamo hatarini.

“Kwanza, hatua hii inaonekana kama kura ya kutokuwa na imani ya uhusiano kati ya Ruto na Biden kwani kimsingi kama balozi wa Amerika nchini, Whitman ni mwakilishi na mtekelezaji wa sera za Biden hapa Kenya. Kwa kujiuzulu, amejiondoa kwa jukumu ambalo linapasa kukamilika rasmi Januari 20, 2025, Biden atakapomkabidhi Trump mkoba wa uongozi wa Amerika,” anasema Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi.

“Kwa hivyo, kujiuzulu kwake hata kabla ya Trump kuapishwa rasmi, kunaashiria kuwa anajitenga na sera za Biden mapema,” anaongeza Bw Mwangangi ambaye pia ni mtaalamu katika nyanja ya Mahusiano ya Kimataifa.

Isitoshe, japo aliteuliwa na Biden (Rais wa chama cha Democratic) kuwa balozi wa Kenya, Bi Whitman ni mwanachama wa chama cha Republican, chake Trump. Mnamo 2010 aliwania ugavana wa California kwa tiketi ya chama hicho lakini akafeli.

Hata hivyo, kwenye taarifa ya kutangaza kujiuzulu Jumatano, Whitman alionekana kuondoa hofu kama hiyo na kuelezea imani kuwa uhusiano kati ya Kenya na Amerika utaendelea kuwa mzuri chini ya utawala mpya wa Trump.

“Sina shaka kuwa ushirikiano wetu uliodumu kwa miaka 60 utaendelea kuimarika kwa manufaa ya Waamerika na Wakenya huku tukilenga kujenga mataifa yenye ufanisi, salama na inayoheshimu demokrasia,” akaeleza.

Bi Whitman pia alitaja mafanikio yake tangu ateuliwe balozi wa Amerika Kenya. Hayo ni pamoja na mikataba kadhaa ya kibiashara, kiafya na kuisalama ambayo Kenya imetia saini na Amerika kama vile kupandishwa hadhi kwa Kenya kama mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO barani Afrika.

“Ni fahari yangu kwamba nimeongoza ajenda ya kuokoa maisha, kuimarisha usalama na kubuni nafasi za kuwawezesha Wakenya na Waamerika kujistawisha kiuchumi.

“Kuanzia kutoa ufadhili wa kupunguza janga la mafuriko mnamo 2023 hadi vita vinavyoendelezwa dhidi ya malaria, Ukimwi na Mpox, kielelezo kuwa Amerika inayapa kipaumbele afya na masilahi ya marafiki zetu nchini Kenya,” Bi Whitman akaeleza.

Wakati wa ziara ya Rais Ruto nchini Amerika mnamo Mei mwaka huu, Rais Biden alitoa ahadi chungu nzima kwa Kenya. Aidha, Kenya na Amerika ilitia saini mikataba mbalimbali ya thamani ya mabiliano ya fedha katika kadhaa za kiuchumi.

Kwa mfano, utawala wa Biden uliiahidi Kenya usaidizi wa thamani ya Sh52 bilioni katika nyanja za uendelezaji wa misingi ya demokrasia, Haki za Kibinadamu, Uongozi na Afya.

Aidha, Amerika iliahidi kuipiga jeki Kenya katika mipango ya kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, na ile ya kustawisha biashara na uwekezaji, uchumi wa kidijitali, vita dhidi ya ugaidi miongoni mwa mingine.

Lakini kuna hofu kwamba huenda Amerika ikapunguza ufadhili kwa shughuli za kuleta amani nchini Haiti chini ya kikosi cha walinda usalama kutoka mataifa mbalimbali chini ya uongozi wa Kenya.

Sababu ni kwamba Bw Trump ameonyesha wazi wakati wa kampeni zake kwamba chini ya utawala wake Amerika haitafadhili kwa ukamilifu shughuli zozote za kuleta amani katika mataifa ya nje.

Kulingana na kiongozi huyo shughuli kama hizo pia zinapasa kufadhiliwa na mataifa mengine ya ulimwengu.