Gachagua ajigeuza ‘mhubiri’ kujijenga
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa anaonekana kubadili mkakati wake wa kisiasa kwa kulenga kudumisha umaarufu wake katika ngome yake ya Mlima Kenya siku chache baada ya kuondolewa mamlakani.
Bw Gachagua ameacha hulka yake ya kutoa matamshi makali katika majukwaa ya umma na badala yake amekumbatia siasa za maridhiano akiwashauri wafuasi wake na wakazi wa eneo hilo, lenye watu wengi, kusalia watulivu na wadumishe amani baada ya kung’atuliwa kwake afisini.
Tangu alipotimuliwa, Gachagua amekoma kabisa kuandaa mikutano ya hadhara kuwahutubia wafuasi wake, badala yake amehiari kuhudhuria hafla za mazishi na ibada makanisani. Ametumia majukwaa haya kuhubiri amani na utulivu.
Mbunge huyo wa zamani wa Mathira amehudhuria angalau hafla tatu za mazishi na kutumia majukwaa hayo kuwatuliza wafuasi wake, akiwahimiza kukubali kutimuliwa kwake na wasubiri kulipiza kisasi debeni katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Bw Gachagua amechelea kabisa kuikosoa serikali na badala yake kuwataka wafuasi wake wampe Rais William Ruto muda awahudumie.
“Hatuna shida na Rais. Tunataka tumpe nafasi katika miaka hii mitatu iliyosalia atimize ahadi alizotoa kwa Wakenya,” Gachagua alisema Jumamosi, Novemba 2, 2024, wiki iliyopita alipohudhuria ibada ya wafu katika Kanisa la Kianglikana (ACK) la Kiamwathi eneobunge la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga.
Ibada hiyo iliandaliwa kumuaga Mama Anna Wanjiru, nyanyake Diwani wa Wadi ya Baragwi David Mathenge.
Aidha, Bw Gachagua alitumia jukwaa hilo kutoa wito kwa wabunge haswa kutoka eneo la Mlima Kenya kuharakisha kupitishwa kwa Mswada wa Kahawa unaolenga kufaidi wakulima wa zao hilo.
“Kila mtu apewe nafasi ya kufanya kazi yake, Rais apewe nafasi ya kutimiza ahadi alizotoa kwa raia na wabunge, haswa wa hapa kwetu, nao wapitishe Mswada wa Kahawa haraka kama walivyopitisha hoja ya kunitimua ili wakulima wetu wapate faida. Vilevile, waisukume serikali itoe Sh5 bilioni zilizotengwa kugharimia madeni ya wakulima wa kahawa,” akaeleza.
Wengi walitarajia kwamba baada ya kuondolewa kwake afisini Bw Gachagua angeanzisha kampeni kali ya kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza na bosi wake wa zamani Rais Ruto.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema mwanasiasa huyo ameamua kukuza ushawishi wake katika ngome yake ya Mlima Kenya kwa manufaa yake kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
“Ingawa kisheria Bw Gachagua hataruhusiwa kuwania kiti chochote katika uchaguzi huo kwa sababu alitumuliwa afisini kwa ukiukaji wa Katiba na maadili, anafanya hivyo kwa manufaa ya mgombea urais atakayeamua kumuunga mkono. Pili, Bw Gachagua anachelea kuishambulia serikali ili kuepuka kuandamwa kwake na vyombo vya dola na hatimaye kufunguliwa mashtaka kwa baadhi ya makosa 11 yaliyoorodheshwa kwenye hoja ya kumtimua afisini,” asema Bw Martin Andati.
Kwa mujibu wa mchanganuzi huyo wa masuala ya siasa na uongozi, Gachagua anaendeleza mchakato wa kujijenga kisiasa, chini kwa chini bila kuonekana kuwa anapiga vita moja kwa moja, serikali ya Rais Ruto.
“Bw Gachagua anafahamu kwamba wakazi wa Mlima Kenya, haswa Mlima Kenya Magharibi wamekerwa kutokana na masaibu aliyopitia. Anataka kutumia hasira hizo kujijenga kisiasa na kushirikiana na wanasiasa wengine kubuni muungano mwingine wa kisiasa kwa uchaguzi mkuu wa 2027,” Bw Andati anaeleza.