Jamvi La Siasa

Gachagua amsifu Raila, amtakia kila la heri uchaguzi AUC

Na BENSON MATHEKA February 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amemtakia kila la heri aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) huku akimshehenezea sifa kemkem.

Katika taarifa yake fupi Ijumaa asubuhi, Bw Gachagua alimsifu Odinga, akimtaja kama mgombea bora wa uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika.

Huku akionyesha matumaini kuwa Bw Odinga atatwaa wadhifa wa bara, Gachagua alisema kwamba hakuna shaka Raila amejitolea kutetea watu wa Afrika.

“Mwaniaji bora zaidi wa Kenya, Mheshimiwa Raila Odinga, bila shaka ndiye mgombea bora wa uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika. Afrika inastahili kilicho bora zaidi. Hakuna shaka kuhusu mtazamo wa kimataifa wa Raila na kujitolea kwake kutetea watu wa Afrika.”

Alkiyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwa na Kinara wa ODM Raila Odinga na wake zao, awali. Picha|Maktaba

Kulingana naye, Afrika, kama bara, inamhitaji Raila, ambaye ana uwezo wa kuunganisha kanda za mbili zinazozungumza Kiingereza na Kifaranza kuunda mustakabali wa bara hili.

Gachagua alibainisha kuwa ushindi wa kiongozi huyo wa Azimio mjini Addis Ababa, Ethiopia, utaimarisha kujitolea kwake kwa muda mrefu kuunganisha Afrika, ambayo ameutetea kwa miaka mingi.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisisitiza kwamba ushindi wa Odinga utakuwa mzuri na wa maendeleo kwa Afrika na kwamba ushindi wake utakuwa ushindi kwa Kenya.

Maoni ya Gachagua kuhusu ugombeaji wa AUC wa Odinga unakuja siku moja tu kabla ya uchaguzi ambao umepangwa kufanyika Jumamosi, Februari 15.

Waziri Mkuu huyo wa zamani anashindana na wagombea wengine wawili; Mohamoud Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar.

Viongozi wa  nchi 55 wanachama wa Muungano wa Afrika akiwemo Rais William Ruto, walianza kuwasili Adis Ababa, Ethiopia Alhamisi  uchaguzi huo.