Jamvi La Siasa

Hofu ya Upinzani kuhusu njama ya Ruto kukwamilia Ikulu

Na CHARLES WASONGA July 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

VIONGOZI wa upinzani sasa wameelezea hofu kwamba kauli zinazotolewa na Rais William Ruto pamoja na wandani wake zinaashiria njama ya kiongozi huyo kukwamilia mamlakani endapo atashindwa katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka vinara hao wanaonya kuwa hatua hiyo inakiuka katiba na inaweza kutumbukiza taifa hili kwenye machafuko.

Naye Naibu Kiongozi wa chama cha Safina Willis Otieno anadai kuwa uamuzi wa Rais Ruto wa kujenga Kanisa kubwa katika Ikulu, ni sehemu ya mipango yake ya kukwamilia mamlakani.

Mabw Gachagua na Musyoka, wakiwa kwenye ziara ya kukutana na raia katika eneo la Magharibi mwa Kenya, viongozi hao waliwataka Wakenya kukataa njama hizo na wajitokeze kwa wingi kupiga kura kumwondoa afisini 2027.

“Hatuwezi kukubali Ruto na watu wake kuvuruga uthabiti nchini. Katiba imesema wazi kwamba Rais akishindwa anaondoka afisini mara moja kumpisha aliyeshinda. Lakini juzi alikuwa hapa Magharibi akidai kuwa hawezi kutupokeza mamlaka tukimshinda 2027 eti hatuna mpango wa kuendeleza taifa hili. Huo ni upuzi mtupu,” akasema Bw Gachagua Alhamisi katika mji wa Luanda Kaunti ya Vihiga.

Aidha, walikerwa na kauli ya Mshauri Mkuu wa Rais kuhusu masuala ya Kiuchumi Moses Kuria kwamba hakutakuwa na uchaguzi mkuu 2027.Mbunge huyo wa zamani wa Gatundu Kusini alidai kwamba “wazee wataketi chini na kukubaliana” kwani Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haitakuwa na muda tosha wa kutayarisha na kusimamia uchaguzi mkuu.

Isitoshe, wandani wa Rais kama vile wabunge William Kamket (Tiaty) na Oscar Sudi (Kapseret) wamenukuliwa wakisema kuwa ni sharti Dkt Ruto ahudumu kama rais kwa mihula miwili.

“Wasilete mchezo, wajue kwamba ninatoka kaunti ya Baringo, kaunti ya miaka 24. Tunajua kutengeneza raia anayehudumu kwa miaka 24. Wakicheza tutamwambia Rais atawale kwa zaidi ya mihula miwili,” Bw Kamket akasema.

Rais wa Pili nchini Hayati Daniel Moi, mzaliwa wa Baringo, anashikilia rekodi ya kuongoza kwa miaka 24; kuanzia Agosti 23, 1978 hadi Desemba 30, 2002.

Hata hivyo, kulingana na katiba ya sasa iliyozinduliwa mwaka wa 2010, Rais anaruhusiwa kuhudumu kwa mihula miwili pekee.Lakini mnamo Juni 15, mwaka huu, akiwa ziarani Magharibi mwa Kenya, Dkt Ruto aliapa kutowapokeza mamlaka viongozi wa sasa wa upinzani, kwani, kwa mtazamo wake, hawana mpango wa maendeleo kwa taifa hilo.Ajenda yao kuu ni ‘Ruto Must Go’

“Hawana mpango wowote. Ajenda yao kuu ni “Ruto Must Go”(Sharti Ruto aondoke). Hamna nyingi.Hii Ruto Must Go inatatua vipi changamoto zinazokumba sekta za afya, elimu, miongoni mwa matatizo mengine?. Siwezi kupokeza mamlaka kwa viongozi kama hawa kwa sababu Wakenya walinipa kazi ya kuhakikisha taifa hili linapata maendeleo,” akasema alipohudhuria ibada katika Kanisa la Friends Quakers katika eneobunge la Lugari.

Kiongozi wa taifa aliwataja Mabw Musyoka, Gachagua, Eugene Wamalwa, Fred Matiang’i na Martha Karua kama kama viongozi waliochanganyikiwa na wasio na mpango wa “kubuni nafasi za ajira kwa vijana wa taifa hili, kufadhili elimu katika vyuo vikuu, kuendeleza kilimo na kufanikisha mpango wa afya kwa wote.”

Lakini kwenye mahojiano na runinga ya NTV juzi, Bw Gachagua alijibu kauli hii ya Rais Ruto akisema wao kama upinzani wanazo ajenda kadhaa za kuboresha maisha ya Wakenya.

“Ajenda yetu ya kwanza ni kumwondoa mamlakani, sio sasa, bali akikamilisha muhula wake. Hii ndio maana tunavumisha kauli mbiu ya “One Term” (Muhula Mmoja). Baada ya kumng’oa tutaweza kutekeleza ajenda zingine kama vile kukomboa mishahara ya wafanyakazi kwa kufutilia mbali ushuru wa nyumba, kuondoa sheria ya Hazina ya NSSF inayofanikisha kiasi cha juu cha makato kwani uwekaji akiba sio jambo la lazima bali la hiari.

Aidha, tunao mpango wa kuondoa hii Bima ya SHA na kuweka bima bora,” akaeleza kiongozi huyo wa chama cha Democracy for the Citizens’ Party (DCP).

Wakili na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa James Mwamu, anaonya kwamba kauli za Rais Ruto na wandani wake zinazoashiria kuwa anapania kukiuka Katiba kwa kukwamilia afisini zinaweza kuleta hofu na taharuki nchini na kuogofya wawekezaji kuanzia mwaka ujao.

“Katiba inaelezea wazi kuwa Rais, magavana, maseneta, wabunge na madiwani wanaruhusiwa kuhudumu muhula moja wa miaka mitano. Baadaye uchaguzi ukifanywa, na Rais na magavana wanaweza kuhudumu muhula wa pili na wa mwisho. Maseneta, Wabunge na madiwani wanaweza kuhudumu kwa mihula zaidi ya mbili.Hakuna kipengele cha katiba kunachompa Rais kibali cha kukataa kuondoka afisini,” anaeleza.

Kulingana na mtaalamu huyo katiba inatoa mwanya wa siku 60 pekee kwa Rais kuendelea kutopokezana mamlaka, endapo nchi imetumbukia kwenye machafuko.