Jinsi kamari ya Gachagua inamzalia matunda maeneo ya Mlimani
ILIKUWA ni kamari ngumu kwa aliyekuwa naibu Rais Rigathi Gachagua alipokataa presha za kujiuzulu wakati wa hoja ya kumtimua ofisini na badala yake akaamua kuwakabili waliomshtaki.
Zaidi ya mwezi mmoja baada ya Bw Gachagua kuondolewa ofisini na nafasi yake kuchukuliwa na Prof Kithure Kindiki kama naibu wa rais, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kisiasa kwa wahusika hao wawili.
Rais Ruto ameimarisha serikali yake kwa kuungwa mkono na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ushirikiano unaomruhusu kupenya kwa urahisi maeneo ya upinzani ambako amezuru mara kadhaa hivi majuzi.
Lakini kutimuliwa kwa Bw Gachagua kumeibua msukosuko katika eneo la Mlima Kenya, ambapo rais, naibu wake na washirika wao eneo hilo wanazidi kupata mapokezi baridi.
Kumkumbatia Gachagua
Eneo hilo linaonekana kumkumbatia Bw Gachagua ambaye hata hivyo hana budi kustahimili fedheha inayotokana na kukabili serikali akiwa nje ya mamlaka.
Lakini kwa nini Bw Gachagua alikataa kujiuzulu na kujiweka katika hatari hadi akatimuliwa Oktoba 17, jambo ambalo linaweza kuzima maisha yake ya kisiasa isipokuwa kama ataokolewa na mahakama?
Mnamo Novemba 25, 2024, katibu wa kibinafsi wa Bw Gachagua, Bw Munene wa Mumbi aliambia Taifa Leo jinsi Oktoba 7 — siku moja kabla ya Bunge la Kitaifa kupiga kura ya kumtimua naibu wa rais — Rais alijaribu kumshinikiza Bw Gachagua ajiuzulu.
“(Rais) alimpigia simu bosi (Gachagua) akimtaka aache kuthubutu kupigana badala yake ajiuzulu na kwenda nyumbani kwa amani kama alivyoingia serikalini. Aliahidi kumwachia usalama na manufaa yake. Alimwambia kwamba alikuwa tayari kufanya chochote kumuondoa serikalini,” Bw Munene alisema akimnukuu Bw Gachagua akisimulia mazungumzo na bosi wake.
Kamari ya Bw Gachagua inaibuka ilikuwa hesabu hatari kwamba ikiwa angekubali kubeba msalaba, watu wake wangeona mateso yake na kumhurumia.
Baada ya huruma, upendo wafuata
“Hii ilifaulu, baada ya huruma, imefuata upendo. Jambo ambalo hatuna uhakika nalo ni jinsi upendo huu utamsaidia Bw Gachagua iwapo atakosa kupata afueni mahakamani kuweza kugombea 2027,” akaeleza mchanganuzi wa kisiasa na msomi Prof Peter Kagwanja.
Msaidizi wa Bw Gachagua Bw Ngunjiri Wambugu, Jumanne iliyopita, aliambia Kogi’s Corner TV kwamba ‘kujiuzulu kungemfanya Bw Gachagua kuonekana mwoga jambo ambalo wapiga kura wa Mlima Kenya wanachukia.
“Iwapo Bw Gachagua angejiuzulu, aliongeza, ingewapa waliomshtaki silaha ya kumwangamiza zaidi kwa kudai kuwa walio na hatia huwa waoga. Sasa imedhihirika kuwa uamuzi wa Bw Gachagua kukabiliana na mchakato wa kumuondoa ana kwa ana badala ya kujiuzulu ulikuwa kamari ambayo ililenga kuibua wimbi la upinzani katika eneo la Mlima Kenya.”
“Tulijua kuwa rais alikuwa amedhamiria kumfukuza Bw Gachagua kutoka serikalini. Ilikuwa imeamuliwa na ujasusi wetu ulitudokeza hivyo.
“Tulikaa chini na kutoa ushauri wetu na kuamua kukabiliana na kesi hiyo kulikuwa ya manufaa zaidi katika kumkabili kiongozi wa nchi 2027,’ alisema mshirika wa Bw Gachagua kaunti ya Murang’a Bw Mwangi Kifeeti.
Bw Kifeeti alisema shtuma ambazo zililimbikiziwa Bw Gachagua zilionekana kuwa makombora mazuri ya kisiasa ambayo yangeweza kumjenga iwapo kweli angetimuliwa “na imekuwa hivyo”.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA