Jubilee ya Uhuru itashirikiana na Gachagua kwa masharti, asema Kioni
CHAMA cha Jubilee kinachoongozwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kimedokeza kuwa kiko tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027—ikiwemo kufungua mlango kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, iwapo masharti fulani yatatimizwa.
Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, amesema kuwa chama hicho hakitakubali kubaki nyuma huku vyama vingine vikiendelea kujipanga upya kisiasa, akiongeza kuwa Jubilee itashirikiana na wale walio na maono ya kumzuia Rais William Ruto kupata muhula wa pili kama rais.
Akizungumza na wanahabari Jumatano, Kioni alisema kuwa chama hicho kiko tayari kushirikiana na viongozi wa eneo la Mlima Kenya ili kuzuia kugawanyika kwa kura za eneo hilo, jambo ambalo linaweza kumfaidi Ruto kisiasa.
“Kile kilichosalia kwa William (Ruto) ni kugawanya mlima. Anatamani sana kuona watu wa eneo hilo wakipiga kura kwa misingi tofauti,” alisema Kioni.
Ingawa hakumtaja Gachagua kwa jina moja kwa moja, Kioni alionekana kumlenga aliposema kuwa si rahisi kuuza chama kipya katika eneo la Mlima Kenya kwa sasa.
“Itachukua muda mwingi na kazi kubwa kujenga chama kipya. Sisi tumejenga Jubilee kwa miaka kumi na sasa tuna wanachama 7.1 milioni. Hivyo basi, ukija na wanachama wako sita, tutakupokea lakini masharti yetu yabaki,” aliongeza.
Kioni pia alisisitiza kuwa Jubilee ni chama cha kitaifa ambacho kiko wazi kwa viongozi wanaotafuta jukwaa la kuwania nyadhifa mbalimbali kote nchini.
Alionya wale wanaotaka kujiunga na Jubilee wasije na masharti yao binafsi: “Kama kweli unataka kuondoa utawala huu, njoo kwenye meza ya mazungumzo. Lakini usije kutuletea masharti.”
Kauli hizi zimejiri siku chache kabla ya tangazo linalosubiriwa kutoka kwa Gachagua, ambaye ameahidi kueleza wafuasi wake mwelekeo mpya wa kisiasa mwezi ujao, kufuatia mvutano wake wa wazi na Rais Ruto.
Jubilee imesema kuwa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ndiye mgombeaji wake wa urais katika uchaguzi ujao..
Chama hicho pia kimeilaumu serikali ya Kenya Kwanza kwa hali ngumu ya maisha na kuongezeka kwa visa vya ufisadi, kikisema kuwa uongozi wa sasa umeshindwa kuwajibika kwa wananchi.
Kioni pia alikosoa vikali makanisa, akisema kuwa taasisi hizo zilichangia kuipigia debe serikali ya sasa katika uchaguzi wa 2022. “Kwa makanisa, mliituuza mwaka wa 2022. Mnahitaji kufanya vyema zaidi,” alisema.