Jamvi La Siasa

Kalonzo ashutumu serikali ya Ruto kwa kukita ufisadi katika bajeti

Na PIUS MAUNDU February 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI  wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameshutumu serikali ya Rais William Ruto kwa kukita ufisadi katika bajeti.

Bw Musyoka alidai kwamba kulikuwa na ufisadi mkubwa katika utawala wa sasa unaonyima raia huduma.

Alisema mikataba yenye utata ya Adani kuhusu ukodishaji wa viwanja vya ndege na laini za  umeme, ambayo ilifutwa na Rais mwaka jana baada ya ghasia za umma, ni aina ya ufisadi uliokitwa katika bajeti uliopangwa kuwatajirisha watu wenye mamlaka.

“Kwa nini watu watake kuingia kwenye uongozi na kupata dunia nzima na kupoteza nafsi zao? Ndivyo Biblia inauliza. Tulikataa dili za uwanja wa ndege wa Adani, wakazifuta. Bado tunasubiri kuona kama kweli walifuta dili za Adani kabisa. Walikuwa katika sekta ya nishati, ni Adani huyo huyo ambaye ni sekta ya afya. Pia wameingilia walimu, ambao hawapati bima na watu wetu wanakufa kwa njaa,” Bw Musyoka alisema.

Kundi la Adani, linalomilikiwa na bilionea wa India Gautam Adani, lilikuwa limependekeza kupanua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na  mradi wa usambazaji wa umeme, kabla ya kufutwa na Rais Ruto mnamo Novemba mwaka jana.

Makamu wa rais wa zamani ambaye aliwahi kuwa waziri wa masuala  ya kigeni  alikuwa akiwahutubia waombolezaji wakati wa mazishi ya Mzee James Mwilu katika Kijiji cha Kombe kaunti ya Machakos.

Bw Musyoka alikuwa akimjibu Seneta wa Machakos Agnes Kavindu ambaye alikuwa amelalamika kwamba sekta ya afya nchini imeporomoka.

Kuhusu uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, ambao Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga alishindwa na Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti, Bw Musyoka alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani alifanya vyema.

Alisema mwenyekiti wa tume AUC anafaa kuchukua hatua ili kurejesha amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Tunapozungumza, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepoteza mji wake wa pili, Bukavu, kwa waasi wa M23. Aliyeshinda kinyang’anyiro cha mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika anapaswa kujua kwamba ana kazi ngumu mbele yake ya kurejesha amani kwa kunyamazisha bunduki,” Bw Musyoka alisema.

Wakati huo huo, Bw Musyoka alimkosoa Rais Ruto ambaye alimshutumu kwa utawala mbaya hasa utekaji nyara wa vijana na mauaji ya  kiholela tangu mwaka jana.