KINAYA: Hivi kuna ithibati kwamba wahubiri wamemrejeshea Zakayo sadaka?
HIVI Kenya hii ya shida, watu wanawezaje kukataa hela? Wachungaji, hasa wa kanisa Katoliki, wanatoa wapi nguvu na ujasiri wa kukataa sadaka ya rais?
Hebu na watoe ithibati kwamba wamerejesha pesa hizo zote ili tuwaamini! Si kwamba tunawashuku, la hasha! Tunataka tu kujua, katika nchi yetu hii ya walafi wasio na aibu wala adabu, wanawezaje kupewa mamilioni ya pesa kisha wakarejesha.
Mtu akikataa zawadi nono ya kiongozi wa nchi humrejeshea vipi? Ni kupitia sanduku la posta, kampuni za usalama, maafisa wa utawala, au hiyo ya kuzirejesha ni hadithi tu?
Ondoa kampuni za usalama; nyingi zina tamaa ya pesa, zikipewa zimrejeshee Zakayo haziwezi kufikisha. Zinajua hawezi kujitokeza hadharani na kusema hakurejeshewa pesa.
Hata wachungaji wanaodai kumrejeshea pesa hizo wanajua hawezi kujitokeza hadharani kusema hawakurejesha, kwa hivyo hata nao wanaweza kucheza na akili zetu kisha wakatia pesa vibindoni.
Kenya yetu ya ajabu huwezi kumwamini yeyote, ndio maana nasisitiza tuonyeshwe ithibati kwamba kwa hakika zimerejeshwa hadi kwa aliyezitoa.
Wala usijitie udarai wa kuniambia kuwa kuzirejesha ni rahisi, eti mtu anaweza kuandika hundi tu na basi. Labda hujui masuala ya hela kubwa; sheria zetu hazimruhusu yeyote kuandika hundi ya zaidi ya Sh999,999.
Kimsingi, ili kurejesha Sh7 milioni, unahitaji hundi saba na ushei. Halahala na tuonyeshwe nakala za hundi walizoandika wachungaji wapendwa ili tuwaamini!
Hata Tomaso wa Biblia hakuamini mara moja kwamba Yesu amefufuka, hadi pale alipogusa alama za misumari, ndipo akaamini hakika huyu ndiye aliyeangikwa msalabani.
Yesu hakukasirishwa na dukuduku la Tomaso na msisitizo kwamba angeamini tu baada ya kuthibitisha, hivyo wachungaji msinikasirikie, igeni mfano wa Yesu Kristo.
Nasikia kuna mmoja wenu, asiye Mkatoliki lakini, ambaye amekalia Sh7 milioni na kukaa kimya, hataki mjadala unaoendelea kuhusu hela na siasa kanisani. Labda kwake yeye sadaka hairejeshwi.
Siku hizi inabidi tuambizane ukweli kwa kuwa Wakenya wengi walishawishika wakamchagua Zakayo baada ya wachungaji kusema kuwa ndiye mteule wa Mungu.
Sina shaka na hilo, hasa kwa kuwa ninajua kuwa, sawa na mui anavyokuwa mwema, mwema naye anaweza kuwa mui, na hilo si jambo tukizi nchini Kenya.
Watu hubadilika ghafla na kukushangaza, ukabaki kinywa wazi, hivyo labda hata viongozi hao wameshtuliwa na mienendo mipya ya Zakayo.
Mungu naye pia anaweza kuwapa watu kiongozi ili awatie adabu, wajutie dhambi za kumsumbua eti wanamtaka fulani awaongoze. Labda tulimkasirisha Mungu akatutupia Zakayo atutese?
Inawezekana pia kwamba Wakenya ni binadamu waliovimba vichwa, wasiojua maana ya uzalendo, wanaomsumbua Zakayo bure bilashi.
Haijalishi! Akitafuta kazi ya kuwaongoza alijua ni watu wa aina gani, hivyo abebe msalaba wake, lau sivyo ajiengue kimya-kimya na kurejea kwao kijijini Sugoi.