Jamvi La Siasa

Kinaya Raila ‘akibariki’ washirika wake waponde serikali

Na BENSON MATHEKA May 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

HATUA ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kumshauri Katibu Mkuu Edwin Sifuna kupunguza mashambulizi yake dhidi ya Serikali Jumuishi huku akisisitiza seneta huyo wa Nairobi anawakilisha msimamo wa chama yanaibua maswali kuhusu iwapo huwa anawatuma washirika wake kuponda serikali.

Raila alikubali kuwa Sifuna ana haki ya kuzungumza kwa niaba ya chama kutokana na nafasi yake kama Katibu Mkuu, lakini akamtaka kupunguza makali ya kauli zake hasa za kushambulia wanachama wa ODM ambao ni mawaziri.

Hii ilikuwa baada ya Sifuna kutofautiana na Waziri wa Fedha John Mbadi.

“Msemaji wa chama mara nyingi ni katibu mkuu, hivyo, Bw Sifuna anapozungumza, anazungumza kwa niaba ya chama. Lakini Bw Sifuna, wakati mwingine punguza kidogo,” alisema Raila wakati wa mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kaspul, Charles Ong’odo Were.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kukiri kwa Raila kwamba Sifuna na viongozi wengine wa ODM washirika wake wanaokosoa serikali wanasisitiza msimamo wa chama kunaonyesha kauli zao huwa zina baraka zake.

“Amewahi kutetea Gavana wa Siaya James Orengo na mwenzake wa Kisumu Peter Anyang Nyong’o kwa kauli zao za kushambulia serikali ambayo ODM inaunga. Akiwa kiongozi wa chama, ingetarajiwa awakemee iwapo wangekuwa wameenda kinyume na msimamo wake ila sasa kuwaunga mkono kunatoa taswira kwamba huwa wanapata baraka zake,” asema mchambuzi wa siasa Derrick Otieno.

Anasema Raila anaonekana kuwa na njama fiche kwa wenzake au kwa mshirika wake katika Serikali Jumuishi Rais William Ruto.

“Inashangaza anaweza kuunga kauli za Sifuna kama ODM itamfanya Ruto kuwa rais wa muhula mmoja na wakati huo huo anashinda Ikulu na Rais wakijadiliana masuala tofauti. Anamshauri atulize boli kushambulia wanachama wa ODM ambao ni mawaziri huku akioenekana kumruhusu kuponda Rais,” asema.

Mnamo Alhamisi Sifuna ambaye ni seneta wa Nairobi alisema ODM ina nia ya kumfanya Dkt Wiliam Ruto rais wa muhula mmoja.

“ODM inapigana kutwaa mamlaka kupitia mchakato wa kidemokrasia. Bado tunakusudia, na hatujakata tamaa katika nia yetu ya kuongoza nchi hii. Tutakuwa pale kukabiliana na kila mtu, hata William Ruto. Na matokeo ya kawaida ya hilo ni kwamba tutamfanya awe rais wa muhula mmoja kwa sababu tunataka kuchukua mamlaka kutoka kwake ili tutekeleze yale tunayoyasema.”

Ni kauli kama hii ambayo Bw Odinga alionekana kuunga.

“Wanachama wa ODM, lazima tuwe imara na kujenga ODM kuwa chama imara cha kisiasa. Katika chama cha kisiasa, kuna tofauti za maoni kuhusu masuala fulani, lakini chama lazima kiwe na msimamo thabiti kuhusu masuala hayo, watu wanapaswa kusema, lakini mwishowe kuna msimamo rasmi utakaotolewa na chama,” aliongeza Raila.

Raila pia amewahi kuwatetea Orengo na Nyongo kwa kauli zao za kushambulia serikali akisema wanaeleza misimamo ya chama. Wawili hao wanaendelea kusimama kidete.

“Orengo hajafanya kosa lolote la kiuhalifu na ana haki ya kuzungumza kwa sababu tuko katika taifa la kidemokrasia. Hakuna makosa akizungumza kuhusu maelewano na ushirikiano wetu na UDA. Profesa Nyongó’o akiongea kuhusu ugatuzi anaongea kwa niaba ya ODM. Ugatuzi ndio muhimu zaidi katika Katiba hii ambayo tuliandaa katika ukumbi wa Bomas,” akasema waziri huyo mkuu wa zamani wakati wa mazishi katika Kaunti ya Homa Bay mwezi Aprili.

Mnamo Ijumaa, Gavana Nyong’o alikanusha ripoti za mgawanyiko kati yake na Raila Odinga, hasa kuhusu mpango wa kukodisha viwanda vya sukari.

Kupitia taarifa, Nyong’o alisisitiza kuwa msimamo wake kuhusu suala hilo ni sawa wa Raila.Gavana huyo aliongeza, “Msimamo wetu wa pamoja ni wazi: serikali lazima ijiondoe katika usimamizi wa viwanda hivi na badala yake vikodishwe kwa wawekezaji wa kibinafsi kupitia mchakato wa ushindani na uwazi.”

Raila ameunga mkono mpango wa serikali wa kukodisha viwanda vya sukari, akisema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa ukuaji wa kiuchumi.Hata hivyo, msimamo wa Raila ulionekana tofauti na Nyong’o, ambaye alitaja hatua hiyo mapinduzi ya kiuchumi dhidi ya wakulima na watu wa Magharibi mwa Kenya.

Dkt Otieno anasema japo kauli za Raila zinaonyesha kuwa anatilia shaka ndoa yake ya kisiasa na Rais Ruto.

“Ukichunguza makubaliano yao, ni ndoa ya muda na ndio sababu anatuma majemedari wake kuishambulia au kushinikiza ajenda na maslahi yake. Wengine wakishambulia akina Sifuna na Orengo, anawaunga mkono ili mshirika wake katika serikali jumuishi aingiwe na mchecheto na kukubali matakwa yake,” asema.