Jamvi La Siasa

KINAYA: Tusulubishe nani, Zakayo au Riggy G?

Na DOUGLAS MUTUA September 29th, 2024 2 min read

‘KUFA dereva, kufa makanga!’ Usiniambie hujasikia kaulimbiu hii. Inakaririwa na Wakenya wasiojali masaibu yanayowasibu wanasiasa wote.

Hao ni Wakenya wanaoamini kwamba mbuzi na ng’ombe wamoja, kondoo mtu wa kando. Hivyo? Wanashikilia kuwa hakuna haja ya kumwokoa ng’ombe wala mbuzi kwa kuwa hatimaye hatamfaa kondoo kwa chochote.

Hayo ni katika muktadha wa jaribio la kumwondoa mamlakani ‘Msema Kweli’ wa Mathira, ama ukipenda Riggy G. Nasikia siku hizi pia anaitwa Riggy Big G. Watu wanachekesha kweli!

Ni vigumu kuamini kwamba ni takriban miaka miwili tu tangu Uchaguzi Mkuu uliopita. Waliokuwa washirika wakuu, Riggy G na Zakayo, leo hawapikwi kwa chungu kimoja wakapikika.

Wanaotangaza kifo cha dereva na manamba wanasema wawili hawa hawana tofauti, hivyo kumwokoa moja na kumwacha mwingine ni sawa na kutoboa jipu juujuu ila ukaacha usaha wote ndani.

Hebu tafakari kuhusu usaha na uchafu mwingineo uniambie kati ya wawili hao, nani usaha. Nani anayenuka? Jipu halinukii!

Msimamo wa kuwaua dereva na manamba kwa mpigo unashikiliwa na Wakenya wachache mno. Siasa zetu ni za kikabila, hivyo kila eneo linakufa na mbaya wao.

Washirika wa Zakayo wamerejea vijijini kuwahakikishia wafuasi wao kwamba hakuna atakayemgusa mtu wao, naye Riggy G na watu wake wamejitokeza kadamnasi na kumwambia Zakayo akiwa tayari kuzichapa atangaze siku!

Zamani tulipotaka kupigana kwa raha zetu tu au kukosana kikweli, tukiambiana hakuna aliyebeba mtoto. Huko ni kutangaza kwamba vita vianze wakati wowote, mpinzani haogopwi.

Je, kati ya Riggy G na Zakayo, ni nani aliyebeba mtoto? Hakika simuoni, wote ni wapenzi wa siasa za makabiliano.

Nyembe hazikatani eti, kwa busara za wakazi wa janibu za Mlima Kenya. Nao Wakambodia husema marafiki hawachezi kamari pamoja.

Inaonekana Riggy G ameshikilia msimamo wa dawa ya puto ni sindano, yaani likidungwa tu linatoboka. Haikosi unajiuliza puto ni nani hapa.

Ni huyo-huyo Zakayo, kigogo wa siasa za Kenya. Watu wake watakwambia kuwa yeye ni bahari isiyotikiswa na vishindo vya mashua.

Ukweli ni kwamba kati yao hakuna kifaranga wala tembe, wote majogoo jeuri. Wanawakilisha jamii kubwa, hivyo hata hilo la kuondoana mamlakani likijiri kitakuwa kibarua kigumu mno.

Riggy G na watu wake wanasema Zakayo hana wabunge 233 wanaohitajika kumtimua ofisini, na ndiyo maana wanamwita puto lililojaa hewa tu, eti itabidi Zakayo azoee sauti na sura hiyo kati ya sasa na mwaka 2027.

Zakayo, mjanja wa siasa aliyemchenga mtangulizi wake, Ouru, na aliyekuwa waziri mkuu, ‘Babaman’, akaingia Ikulu, anaogopwa na wengi. Haya anayachukuliaje?

Langu jicho tu. Lako pia.

[email protected]