Jamvi La Siasa

KINAYA: Zakayo ni wetu sote, tuache kumkimbia

Na DOUGLAS MUTUA October 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HIVI unadhani Zakayo aliingia mamlakani kutokana na maombi ya waumini, au ni mbinu ya mwenyezi Mungu kutuadhibu kwa utundu wetu Wakenya?

Kuna hadithi kuhusu mganga aliyepata umaarufu kwa kupiga bao njiani walipopitia waumini wakielekea kanisani.

Aliudhi sana eti kwani alifanya vituko vyake hivyo kila Jumapili asubuhi, waumini wakielekea kanisani. Aliwashtua na kuwaogofya si haba!

Viongozi wa kanisa lile walikasirika mno, wakawatuma wazee wa Nyumba Kumi wamkanye hasidi yule, lakini mganga wa watu hakujali wala kubali.

Kutokana na jeuri yake – pamoja na sarakasi za kula na kutapika moto kwa wepesi – baadhi ya waumini walianza kupita njia ya mbali kuelekea kanisani. Wapo walioacha kwenda kanisani kabisa.

Maudhi hayo yaliwafika kileleni viongozi wa kanisa hilo, wakaandaa mfungo na maombi kwa juma zima, ili hasidi wao ashindwe.

Hata kabla ya mfungo kuisha, nyumba ya mganga, pamoja na zana zake vya kazi, viliungua! Haikujulikana mara moja moto huo ulitokana na nini kwa sababu hakuwa na nguvu za umeme.

Mganga mjanja, baada ya kupata habari kwamba kanisa tayari lilikuwa kwenye mfungo kwa ajili ya kumtia adabu, alikimbia mahakamani na kulishtaki.

Shtaka lilisema: “Kutokana na maombi ya washtakiwa, moto uliteketeza kila kitu alichomiliki mlalamishi na kumsababishia hasara ya mali na msongo wa mawazo usiomithilika.”

Mganga aliiomba mahakama ilikute kanisa hilo na hatia, iliagize limlipe fidia ya mamilioni ya pesa, tena likome kutia dua dhidi yake, akaongeza na liagizwe liache kumpigia kelele anapofanya vituko vyake. Kazi zote mbili ziheshimiane eti.

Walipopandishwa kizimbani kujitetea, viongozi wa kanisa hilo pamoja na waumini wao walikanusha mashtaka! Walisema maombi yao hayakusababisha hasara waliyoshtakiwa.

Jaji alibaki kinywa wazi. Alijipata kwenye njia-panda hasa: Mbele yake palikuwa na waumini wasioamini maombi yao yalijibiwa, na vile-vile mganga kafiri aliyeamini maombi ya waumini yalijibiwa! Amwamini nani?

Katika muktadha wa siasa za Kenya, sasa watu waliodai kumwombea Zakayo hadi akachaguliwa kiongozi wa nchi, na wakasisitiza kuwa ‘si uchawi, ni maombi’, wamekuwa wajanja.

Hawataki kujinasibisha naye tena, ilhali waliomwona mbwa mwitu aliyevalia ngozi ya kondoo wamemkumbatia na kumbusu. Sasa anapendeza eti.

Kwa vyovyote vile, naamini kati ya makundi hayo mawili, lipo linalosema kweli. Hayawezi kuwa yanasema uongo tu, lazima pana ukweli hata ikiwa ni asilimia ndogo namna gani.

Biblia Takatifu inasema Wanaisraeli walipomsumbua Mungu sana awateulie mfalme, alichoshwa na maudhi yao akawapa Sauli shingo-upande ili awatese kikweli.

Ikiwa Wakenya walioomba bila kukoma walimuudhi Mungu, akatupa Zakayo ili atutese, basi wanapaswa kutubu dhambi zao.

Vile-vile, waliomchukia Zakayo, na sasa wanampiga pambaja, wanapaswa kutukoma pia! Hii Kenya si ya Zakayo.

[email protected]