Kivuli cha Uhuru kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027
Licha ya kuwa kimya na kujitokeza hadharani mara chache, kivuli cha Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kinaendelea kutanda katika ulingo wa siasa nchini Kenya, huku dalili zikionyesha kuwa anaweza kuwa na ushawishi mkubwa katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Ingawa hajaonekana kushiriki moja kwa moja kisiasa, Bw Kenyatta bado anavutia wafuasi wengi kisiasa, akiwakaribisha wageni katika makazi yake ya Ichaweri, Gatundu Kusini (Kaunti ya Kiambu), kutoa jumbe fiche za kisiasa, na kuripotiwa kuwa anashiriki mipango ya kisiasa nyuma ya pazia kuwasaidia washirika wake kuelekea uchaguzi ujao.
Mmoja wa wageni wake wa kushangaza mwezi Desemba mwaka jana alikuwa Rais William Ruto, ambaye walifanya mazungumzo naye. Miezi michache baadaye, baadhi ya washirika wa Bw Kenyatta waliteuliwa katika baraza la mawaziri.
Katika Uchaguzi wa 2022, Bw Kenyatta alimuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga dhidi ya naibu wake wa wakati huo, Dkt Ruto.Katika mahojiano maalum yanayotarajiwa kurushwa na runinga ya NTV usiku huu, Bw Odinga alifichua kuwa Bw Kenyatta alichangia pakubwa katika mkataba aliotia saini na Rais Ruto kufuatia maandamano ya vijana wa Gen Z mwaka jana.
“Wakati maandamano yalipokuwa yamefikia kilele, Uhuru alinipigia simu akiwa Amerika na kusisitiza umuhimu wa kutuliza nchi. Alinishauri nizungumze na Rais Ruto ili tupate suluhu ya kudumu. Nilishirikiana na viongozi wenzangu wa Azimio, tukajadili kama chama (ODM), ndipo tukakubaliana kuwa hatuwezi kuruhusu nchi izame katika machafuko,” alisema Bw Odinga.
Kauli hiyo iliangazia jinsi ambavyo Bw Kenyatta bado ana ushawishi mkubwa katika masuala ya kitaifa, hata baada ya kustaafu.Kwa sasa, kutoka siasa za Mlima Kenya hadi mageuzi ya upinzani na hata harakati za Gen Z, inaonekana wazi kuwa Bw Kenyatta anasuka mikakati nyuma ya pazia, hali inayozua maswali ikiwa anapanga kurudi katika siasa si kwa ajili yake binafsi, bali kwa niaba ya wale anaamini wanafaa kuongoza taifa.
Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, amesema kuwa chama hicho, kinachoongozwa na Bw Kenyatta, kinamtazama aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kama mgombea wa urais mwaka 2027. Kauli hiyo haijawahi kupingwa hadharani na Bw Kenyatta.
“Watu wanakumbuka jinsi alivyowaonya dhidi ya kumchagua Ruto. Anachotaka ni uongozi bora kwa sababu aliwahi kuwa rais na akafanya kazi nzuri. Watu wanatazamia awaonyeshe mwelekeo,” alisema Bw Kioni.
Licha ya kutangaza kustaafu siasa, mienendo ya Bw Kenyatta inaendelea kuibua hisia kali. Anaendelea kuathiri mazungumzo ya kisiasa na kubadilisha mizani ya siasa kuelekea 2027.
Prof Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia anasema kuwa ushawishi wa Uhuru una nguvu kubwa kisiasa.“Uhuru anamiliki uwezo mkubwa wa kifedha kutokana na utajiri wa familia yake. Katika siasa, pesa ni kila kitu. Kampeni ni ghali mno, na kuwa na mfadhili kama Uhuru ni faida kubwa kisiasa,” anasema Prof Naituli.
Lakini anasema kuwa ushawishi wake hauishii kwa fedha pekee.“Ana nguvu katika nyanja tatu: kiuchumi, kisiasa, na kidiplomasia. Urais wake ulimwezesha kujenga mahusiano na viongozi wa bara Afrika na mataifa mengine. Diplomasia hiyo bado inafanya kazi kwani viongozi wa kimataifa wanaendelea kumtembelea Gatundu, wakimheshimu kama mzee wa taifa.”
Mchanganuzi wa siasa, Javas Bigambo, anasema Uhuru hajatoka kabisa katika jukwaa la siasa.“Ushawishi wake bado ni mkubwa, hasa katika eneo la Mlima Kenya. Anaonekana bado anajali chama cha Jubilee na huenda bado ana machungu kuhusu ushindi wa Ruto 2022.
”Bw Wambugu Ngunjiri, aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini, anakiri kuwa kivuli cha Kenyatta bado kinatanda nchini.“Alihudumu kwa miaka karibu 30 serikalini, akihudumu kama Rais kwa miaka 10. Hii inafafanua kwa nini kila hatua yake inazua hisia kote nchini.”
Kulingana na Bw Ngunjiri, huku Mlima Kenya ukikumbwa na migawanyiko, wapiga kura wa kawaida wanamtazama Kenyatta kwa mwelekeo.
“Anaweza kuathiri pakubwa siasa za 2027 kwa sababu ya uzoefu wake, hata kama atafanya hivyo kwa njia ya kisiri. Tusisahau pia kuwa Uhuru ni mpenda taifa, hawezi kufurahia juhudi za kuigawanya Kenya kwa misingi ya kikabila,” alisema.
Wakati huo huo, Bw Kioni anadai kuwa juhudi za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuunganisha Mlima Kenya kupitia chama cha DCP zinaonekana kugonga mwamba kwa sababu ya uaminifu unaoendelea kwa Bw Kenyatta na chama cha Jubilee, ambacho kimekataa kuvunjwa.