Jamvi La Siasa

Masharti ya Raila kwa Ruto

Na  RUSHDIE OUDIA March 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKATABA mpya wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ukitekelezwa kikamilifu, utafanya Waziri Mkuu huyo wa zamani kudhibiti hadi asilimia 50 ya Baraza la Mawaziri na nyadhifa zaidi za serikali.

Hii itakuwa sawa na serikali ya muungano mkuu wa 2008 alipogawana mamlaka na Rais Mwai Kibaki baada ya uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata mwaka mmoja mapema.

Mkataba uliopendekezwa—uliokubaliwa katika Ikulu ya Mombasa siku ya Jumatatu na mbele ya naibu rais Kithure Kindiki, kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah na mwenzake wa walio wachache Junet Mohamed miongoni mwa viongozi wengine mashuhuri—unaweza kutekelezwa mapema wiki ijayo.

Bw Odinga ameahidi tangazo kuu wakati huo.

Bw Ichung’wah na Bw Mohamed tayari wameagizwa kuharakisha miswada husika itakapowasilishwa Bungeni.

Bw Odinga, ingawa anasemekana kusitasita kujiunga na serikali kama Waziri Mkuu au katika nafasi sawa kwa jina tofauti, pia anaweza kuidhinishwa kwa muda mfupi ikiwa atabadilisha mawazo yake, chanzo kilisema.

Mpangilio huo, kulingana na wanaofahamu maelezo, huenda ukaipa ODM nafasi tatu zaidi za Baraza la Mawaziri juu ya tano za sasa.

Chama cha Bw Odinga pia kinatarajiwa kupata angalau nafasi 10 za Makatibu wa wizara.

Rais Ruto wiki jana alipokea orodha ya waliofaulu kwa nyadhifa za makatibu baada ya wiki moja ya mahojiano.

“Kutakuwa na uteuzi wa makatibu, idadi haijakubaliwa lakini Rais Ruto amekuwa tayari kwa hilo tangu mwanzo. Pia kuna viti vya kamati za bunge ambazo Ruto ametoa, angalau vitano vilivyokuwa vya Kenya Kwanza.

Mabadiliko ya kina ya sera kuhusu ufadhili wa elimu, ufadhili wa afya, sera za kiuchumi na fedha. Baadhi ya nyadhifa za  mawaziri pia zinatarajiwa,” alisema mshirika wa karibu wa Bw Odinga kwa sharti tubane jina kwa kuwa haruhusiwi kujadili maelezo ya mpango huo kwa sasa.

Tume ya Utumishi wa Umma, inayoongozwa na Anthony Muchiri, iliwahoji jumla ya watu 109 waliotuma maombi kuwa makatibu wa wizara katika mchakato uliokamilika Januari 31.

Tayari, hofu imewakumba mawaziri na makatibu kwani  mabadiliko yanayotarajiwa yatawafanya wengi wao kukosa kazi.

Ili kuandaa mazingira hayo, Bw Odinga alianzisha misururu ya mikutano katika ngome zake za Nyanza na Magharibi ili kushawishi wafuasi wamuunge mkono  ]kufanya kazi na serikali ya Dkt Ruto akisema ni kwa manufaa ya taifa kwa sasa.

Mawaziri Opiyo Wandayi (Nishati na Petroli), Bw John Mbadi (Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Kiuchumi), Bw Hassan Joho (Uchumi wa Madini na Bluu), Bw Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika na MSMEs) na Bi Beatrice Askul Moe (Jumuiya ya Afrika Mashariki) wote ni viongozi wakuu wa zamani wa ODM.

Gavana wa Siaya James Orengo amesisitiza kwa muda mrefu kuwa chama hicho lazima kiwe na ushirikiano uliopangwa na serikali.

“Uongozi wa Siaya umekubali kwamba Baba (Bw Odinga) ashiriki mashauriano ambayo hatimaye yataleta uhusiano uliopangwa ambapo kuna usawa, haki na uhuru katika nchi yetu ya Kenya.

Nina hakika Baba hawezi kukosea ikiwa anataka kufanya kazi kwa ajili ya watu na ambapo kuna uhusiano uliopangwa tunaposhirikiana na vyama vingine ikiwa ni pamoja na watu walio ndani na nje ya serikali,” alisema Gavana Orengo.

Makubaliano hayo pia yanaweza kumaanisha kuwa Odinga atastaafu kisiasa baada ya uchaguzi wa 2027.

Wandani wake wanasema hajali kuunga azima ya  Rais Ruto ya kugombea muhula wa pili.

Bw Odinga, walio karibu naye wanasema, pia anafahamu kwamba wakati huenda usiwe upande wake, ikizingatiwa kuwa atakuwa na umri wa miaka 82 uchaguzi ujao wa urais utakapofanyika.

Katika umri wake, hayuko tayari kwa kampeni za uchaguzi wa urais.