Jamvi La Siasa

Mikakati ya Karua kuvutia Gen Z baada ya kubadili jina la Narc-Kenya

Na CHARLES WASONGA February 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Narc-Kenya sasa kitajulikana kama People’s Liberation Party (PLP) baada ya kupokea cheti cha kubadili jina lake kutoka kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Hatua ya kubadilisha jina la chama chake ni mojawapo ya juhudi za kiongozi wa chama Martha Karua za kuvutia vijana wa kizazi cha Gen Z ambao wanaaminiwa wataamua mshindi wa kura za urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Mnamo Ijumaa, Januari 31, 2025, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu alimpokeza Bi Karua stakabadhi zote za kisheria za kuhalalisha kubalishwa  jina kwa Narc Kenya.

Bi Nderitu alipongeza Narc Kenya kwa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria kufanikisha kubadilishwa kwa jina lake, kulingana na Sehemu ya 20 ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011.

“Ninatoa wito kwa chama hiki kuendeleza uzalendo na kuzingatia haki za kisiasa kama zilivyoorodheshwa katika kipengele cha 38 cha Katiba ya Kenya,” Bi Nderitu akasema.

Kubadili jina ni mojawapo ya mageuzi manne makuu yaliyotekelezwa na Narc-Kenya  inapolenga kubadili sura yake na kuvutia ufuasi, haswa miongoni mwa vijana, kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kando na kubadili jina, Narc Kenya pia imebadili nembo yake, rangi zake rasmi na kauli mbiu.

Badala ya rangi zake za zamani zilizokuwa nyekundu na nyeupe sasa chama cha People’s Liberation Party (PLP) kitatambuliwa kwa rangi, nyeupe na zambarau.

Alama yake sasa ni ua la waridi lenye rangi ya zambarau wala sio ua la waridi la rangi nyekundu lililotumika kutambua Narc-Kenya.

Kauli mbiu ya PLP ni “Ungana” na “Komboa” ikichukua mahala pa ile ya zamani ya “Kenya Moja, Taifa Moja, Watu Wamoja”.

Hatua hii ya kukipa chama chake sura na jina mpya inajiri siku chake baada ya Bi Karua na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuonyesha dalili ya kujitolea kwao kufanya kazi pamoja.

Wiki moja iliyopita Bw Gachagua alimtembelea Bi Karua nyumbani kwake katika kijiji cha Kimunye, eneo bunge la Gichugu, kaunti ya Kirinyaga ambako walitangaza kuwa watashirikiana kisiasa kuelekea 2027.

Wawili hao waliwasifia zaidi vijana wa Gen Z na kuwarai kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kuwa wapiga kura.

Kulingana na Baraza la Kitaifa la Idadi ya Watu na Maendeleo (KNPC), sensa iliyoendeshwa mwaka wa 2019 ilionyesha asilimia 75.1 ya Idadi jumla ya watu nchini ni walio na umri wa chini ya miaka 35.

Hii ni sawa na watu 35.7 milioni au Wakenya watatu kati ya Wakenya wanne, wengi wao sasa wakionekana kupigania ukombozi wa kisiasa na kiuchumi.

Bi Karua amesisitiza kuwa kubadilishwa kwa jina la chama chake cha Narc-Kenya kunaashiria mabadiliko ya uongozi katika chama ambacho sasa kitakumbatia na kuendeleza matakwa ya Wakenya wenye umri mdogo.

Aliongeza kuwa chama cha PLP kinalenga kubadili katiba yake ambapo kati ya mambo mengi kitaanzisha mtindo wa viongozi kuhudumu kwa muhula mahsusi.

“Hii ina maana kuwa katika uchaguzi ujao wa chama, sitaruhusiwa kuwania kiti cha uongozi wa chama,” Bi Karua akasema.

Jina kamili la Narc-Kenya ni National Rainbow Coalition-Kenya.

Chama hicho kiliundwa mnamo 2005 baada kura ya maamuzi kuhusu rasimu ya Katiba ambako serikali ya Rais Mwai Kibaki, iliyounga rasimu hiyo, ilishindwa na upinzani ulioongozwa na Raila Odinga.

Kiliundwa na wanachama wa uliokuwa Muungano wa Narc (National Rainbow Coalition) waliokuwa waaminifu kwa serikali hiyo ya Rais Kibaki.

Bi Karua aliwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2013 kwa tiketi ya chama cha Narc-Kenya, baada ya kutwaa uongozi wake punde tu alipojiuzulu kutoka serikali ya Kibaki.