Mikakati ya Kindiki kupenya kwa Muturi, Gachagua
NAIBU Rais Kithure Kindiki sasa anaonekana kulenga ngome ya Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi huku akiendeleza azma yake ya kutwaa udhibiti wa eneo la Mlima Kenya kutoka kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Jana, Prof Kindiki alifanya mkutano na ujumbe wa viongozi kutoka Embu katika makazi yake Nairobi Karen, ishara kwamba amedhamiria kudhibiti eneo hilo kuelekea 2027.
Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na viongozi wa kisiasa wenye ushawishi katika kaunti hiyo akiwemo Gavana Cecily Mbarire, Seneta Alexander Mundigi na Mbunge Geoffrey Ruku (Mbeere Kaskazini) na Nebart Muriuki (Mbeere Kusini).
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Spika wa Bunge la Kaunti ya Embu Josiah Thiriku, Kiongozi wa Wengi Bungeni Peter Muriithi pamoja na viongozi wa kidini.Mkutano huo unakuja siku tatu tu baada ya Prof Kindiki kukutana na viongozi wa Meru na Tharaka.
Prof Kindiki yuko mbioni kujijenga katika Mlima Kenya kwa sababu sasa ndiye kiongozi mkuu wa kisiasa katika eneo hilo kufuatia kutimuliwa kwa mtangulizi wake Rigathi Gachagua.
Anataka kutwaa udhibiti wa eneo hilo kutoka kwa Bw Gachagua ambaye amekuwa akijigamba kuwa yeye ni mfalme wa eneo hilo na hata kuwaambia wakazi kuwa atawapa mwelekeo wa kisiasa mwezi huu.”Nitawapa mwelekeo wa kisiasa,” Bw Gachagua alisema hivi majuzi wakati wa ibada ya mazishi huko Mbeere Kaskazini.
Viongozi walimhakikishia Prof Kindiki kwamba walikuwa nyuma yake. “Ni kweli tulikutana na Kindiki na tukaahidi kuungana tena katika azma yake ya kuunganisha eneo letu,” mmoja wa wabunge aliambia Taifa Leo.
Akiwahutubia viongozi hao, Prof Kindiki alisema ana uwezo wa kuunganisha wakazi wa Mlima Kenya wamuunge Rais. “Mtu fulani aliniuliza kama ninaweza kuunganisha Mlima Kenya nyuma ya Rais William Ruto na jibu langu lilikuwa rahisi. Nitaunganisha Mlima Kenya kwa ukamilifu kwa kuwa hii ni sehemu ya Kenya,” alisema.
Prof Kindiki alisema dhamira yake ni kuhakikisha kuwa Rais Ruto anafaulu katika kazi yake kama kiongozi wa nchi na serikali.“Nitafanya chochote kuhakikisha kuwa ajenda ya mabadiliko ya utawala wa Kenya Kwanza inafanikiwa,” alisema.
Aliahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inakamilika na mingine mingi inaanzishwa na Rais ataenda kuizindua.
“Tunataka kurejea Embu na kaunti zote 46 tukiwa na matokeo yanayoonekana,” alisema. Alimsuta mtangulizi wake akisema aliamua kutumia afisi yake kuendeleza siasa badala ya ujenzi wa taifa.
Prof Kindiki alishauri viongozi kutojihusisha na siasa za kikabila katika mikutano yao na kuzingatia umoja wa Wakenya wote.Alisema hakuna sehemu yoyote ya nchi itakayonyimwa maendeleo, na kuongeza kuwa lazima Wakenya wote wanufaike na rasilimali za nchi.
“Kila sehemu ya nchi itanufaika na miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya Wakenya wote,” akaongeza.
Mkutano huo unajiri huku viongozi wa serikali wakimshambulia Waziri Muturi anayetoka Embu kwa kukosoa serikali kuhusu utekaji nyara wakiashiria huenda akavuliwa uwaziri.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA