Jamvi La Siasa

Mrengo mpya sasa waibuka kumzima Gachagua Mlimani

Na MWANGI MUIRURI July 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

BAADA ya miezi michache ya juhudi kubwa za kujitwika taji la kuwa msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wa kisiasa na washirika wa Rais William Ruto wanaojipanga kumzima.

Tangu alipong’olewa mamlakani mnamo Oktoba 2024, Bw Gachagua amezunguka maeneo mbalimbali ya Mlima Kenya akimkashifu Rais Ruto kwa kudai hafai kuongoza kwa muhula wa pili, huku akieneza kauli ya “wantamu” yaani Ruto anafaa kuongoza muhula mmoja tu.

Bw Gachagua pia ameanzisha chama kipya cha Democracy for Citizens Party (DCP) ambacho anavumisha kama ‘gari’ maalum la kisiasa kwa watu wa Mlima Kenya, akisisitiza kuwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) hakikubaliki tena, licha ya kuwa kilisaidia viongozi wengi wa eneo hilo kuchaguliwa.

Ameanzisha vita wazi dhidi ya viongozi wa Mlima Kenya waliopiga kura kumtimua mamlakani, akiwaita “wasaliti” na kupigia debe kukataliwa kwao debeni mwaka wa 2027.

Pia ameshambulia vyama vingine vya eneo hilo visivyomuunga mkono.Wachambuzi wa kisiasa wanaonya kuwa huenda Gachagua ameanzisha vita vingi vya kisiasa kwa wakati mmoja, hali inayozua mashambulizi ya pamoja kutoka kwa mrengo wa Rais Ruto na viongozi wengine wanaopanga kuunda nguvu mbadala.

“Gachagua hakutarajia kuachiwa uwanja wazi kucheza michezo ya kisiasa ya kiwango hiki bila pingamizi. Ilitarajiwa kuwa mkakati wa kumdhibiti ungejitokeza na sasa tumeuona,” asema mchambuzi wa kisiasa Profesa Macharia Munene.

Anasema kuibuka kwa mrengo wa tatu wa kisiasa ni jambo ambalo lilitarajiwa, kwa kuwa hali ya ushindani ilikuwa bayana.

Baadhi ya wanasiasa mashuhuri ambao hawajaonyesha uaminifu kwa Gachagua ni Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro (ambaye pia ni mkosoaji mkubwa wa Rais Ruto), Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, na aliyekuwa mshauri wa rais, Moses Kuria.

Ingawa Kuria hajatangaza rasmi, amekuwa akimkosoa vikali Gachagua.

Kampeni kubwa pia imeanzishwa kumshawishi aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kugombea urais kupitia chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Jeremiah Kioni aliambia Taifa Jumapili: “Dkt Matiang’i ndiye chaguo bora zaidi dhidi ya Ruto. Tunamuunga kwa sababu tunaamini anaweza kukomboa taifa.”Kioni anasisitiza kuwa hawampingi Gachagua bali wanatoa chaguo mbadala.

“Hatufai kuonekana kama tunampinga. Tunataka kusaidia Mlima Kenya na taifa kwa jumla kufanya uamuzi sahihi za 2027.”

Alipoulizwa iwapo huo ni mrengo wa tatu, alisema: “Inategemea na nguvu zilizo uwanjani. Tunajua adui wetu wa pamoja ni Rais Ruto. Wanaokasirika na chaguo letu kwa Matiang’i wanaweza kuunda miungano yao.”

Wafuasi wa Gachagua hawajakaa kimya. Kiongozi wa Wanawake wa DCP, Bi Cate Waruguru, amedharau miungano mipya inayoibuka.

“Tuna timu ya kiufundi inayofuatilia mienendo ya kisiasa Mlima Kenya. Kuna wanasiasa wanaojifanya wanateswa ili kuvutia huruma. Wengine waliandaa kuondolewa kwao kwenye kamati za Bunge ili waonekane kama waathiriwa,” alisema.

Alidai kuwa kuna mpango unaoendeshwa na wanasiasa wanaomuunga mkono Rais Ruto wa kuwasilisha wagombeaji bandia ili kufifisha nguvu ya Gachagua na baadaye kukubali matokeo ya uchaguzi wa 2027 hata kama yatakuwa ya utata, na kuunda serikali ya pamoja kati ya 2027 na 2032.

“Tunajua njama hii. Kazi yetu ni kuwaelimisha wananchi na kufichua mipango hii,” akaongeza.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini, James Gakuya, mshirika wa karibu wa Gachagua, anasema hakuna siasa ya maana ya Mlima Kenya inayoweza kufanyika pasipo idhini ya Gachagua.

“Wanaotaka kufanya biashara ya kisiasa na Mlima Kenya lazima wapitie kwa Gachagua. Ukijaribu njia nyingine, tutakuchukulia kama adui,” alisema.

“Na kama kweli unampinga Ruto, basi taja jina lake moja kwa moja na sema makosa yake yote.”

Kiongozi wa The Service Party (TSP), Bw Mwangi Kiunjuri, ambaye aliwahi kuwa mshirika wa karibu wa Uhuru na Ruto, sasa anaongoza kundi linalompinga vikali Gachagua.

“Mradi wa Gachagua wa kikabila hautanasa Mlima Kenya. Tukiona mrengo wa tatu hautoshi, tuko tayari kuunda hadi mirengo 10,” alisema.

Alifichua kuwa wamekuwa wakifanya mikutano ya kila wiki, na tayari wamewavutia baadhi ya wafuasi wa Gachagua, marafiki wa karibu wa Uhuru na viongozi waliokuwa bado wakisitasita kuamua upande wa kujiunga nao.

“Hatuwezi kuruhusu mtu mmoja ajitangaze kuwa ndiye msemaji wa eneo lote. Gachagua atazungukwa na miungano mingi – mingine ikiunga mkono muhula wa pili wa Rais Ruto,” alisema Kiunjuri.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Bw Wachira Kiago, aliambia Taifa Jumapili kwamba baraza lao linafuatilia hali kwa lengo la kusaidia kufikia mwafaka kati ya wagombeaji wote wa Mlima Kenya.

“Tunajua hisia za watu kuhusu 2027. Lengo letu kama wazee ni kuhakikisha makundi yote yanavumiliana lakini bado tunakuwa na mwelekeo mmoja utakaunganishwa na mwelekeo wa kitaifa,” alisema.