Jamvi La Siasa

Niliondoka mikono mitupu kutoka handisheki yangu na Uhuru, asema Raila

Na JUSTUS OCHIENG July 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa ODM Raila Odinga amepuuza madai kuwa alinufaika kutokana na ushirikiano kati yake na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, akisema hakupokezwa nafasi yoyote serikalini au kupata manufaa ya kibinafsi.

Bw Odinga alikanusha dhana kuwa alishiriki handisheki na Bw Kenyatta mnamo 2018 kwa nia ya kujitajirisha, akisema malengo yao yalikuwa kushinikiza mageuzi.

Waziri huyo mkuu wa zamani alisisitiza kuwa hakuna manufaa yoyote aliyopata kibinafsi au kupitia wandani wake kwenye serikali ya handisheki jinsi wengine wanavyodai au kufikiria.

“Sikufaulisha uteuzi wa mtu yeyote kwenye serikali ya Uhuru. Nilipata nini? Sikupata chochote,” akasema Bw Odinga katika mahojiano.

Alifafanua kuwa uungwaji kutoka kwa Bw Uhuru ulikuja wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 akisema hiyo ilikuwa hadharani.

“Uhuru alikuwa anaondoka. Alisema ataniunga mkono, ahadi ambayo alitimiza. Kwa hivyo, nilimshawishi Uhuru kivipi ninufaike na utawala wake? Sikufanya hivyo,” akasema Bw Odinga.

Mbunge huyo wa zamani wa Lang’ata alisema ‘handisheki’ iliyozaa Jopo la Maridhiano (BBI) ililenga tu kushughulikia masuala ya uongozi na uwazi wakati wa uchaguzi mkuu.

Bw Odinga alisema BBI iliporomoka kwa sababu ya uamuzi wa mahakama na hawafai kubebeshwa zigo hilo.

“Ni mahakama ilikataa BBI na lau ingepita, yaliyotokea 2022 hayangefanyika hivyo,” akasema.

Alisisitiza kuwa kutofaulu kwa BBI ndiko kulichangia uchaguzi wa 2022 kukosa uwazi na pia mgawanyiko ulioshuhudiwa kati ya makamishina wa Tume ya Uchaguzi (IEBC).

“Chebukati angeondolewa kutoka IEBC. Ukikumbuka Chebukati na makamishna watatu walisema kitu tofauti na wengine wanne,” akasema akikumbuka mgawanyiko ulioshuhudiwa kwenye tume hiyo wakati wa matangazo ya matokeo ya kura za urais.

Kwenye mahojiano, Bw Odinga pia alikosoa uamuzi wa Mahakama ya Juu ukiongozwa na Jaji Martha Koome ambao ulidumisha ushindi wa Rais William Ruto, akisema haukuzingatia sheria.


“Kwa mara ya kwanza Mahakama ya Juu ilikubali kuwa watatu ni wengi kuliko wanne. Mbona watu hawazungumzi kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Juu. Wanazungumza tu kuhusu Raila,” akalalamika.

Kiongozi huyo alisema baada ya uamuzi huo wa mahakama hakuwa na jingine ila kukubali uongozi wa Rais William Ruto.

“Baada ya uamuzi huo, ningefanya kipi kingine? Ni mahakama ilikosea, si mimi,” akasema.

Matamshi yake yanakuja baada ya kufufuliwa kwa mjadala kuhusu handisheki ya 2018, uhalali wa kura za 2022 na ushirikiano ambao anao sasa na Rais Ruto kwenye Serikali Jumuishi.

Raila alisema kuwa taifa bado linapambana na changamoto tele ndiposa ODM iliamua kushirikiana na utawala wa Rais Ruto.

Uamuzi wa kufanya hivyo, ulisukumwa na haja ya kuwa na taifa lenye udhabiti.

“Tumesema tuko ndani ya Serikali Jumuishi hadi 2027. Hatua itakayofuata ni masuala ambayo tutayajadili wakati ukifika na uamuzi utafanywa na wanachama wa ODM si Raila Odinga pekee,” akasema kiongozi huyo.

Ushirikiano na Rais Ruto, Bw Odinga alisema ulitokana na wimbi la maandamano lililoongozwa na vijana wa Gen Z, maasi hayo yakitishia kusambaratisha umoja wa taifa.

Bw Odinga alisema iwapo hangechukua hatua ya kuungana na Rais Ruto, Kenya saa hii ingetumbukia kwenye ukosefu wa udhabiti kama Somalia, Haiti na Sudan.

Ushirikiano wa Ruto-Raila ulichangia uteuzi wa wandani wa kiongozi huyo wa ODM serikalini.


Walioteuliwa mawaziri kutoka ODM ni Opiyo Wandayi (Kawi), John Mbadi (Hazina ya Fedha), Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika) na Beatrice Askul (Jumuiya ya Afrika Mashariki).