Jamvi La Siasa

ODM wataka minofu zaidi kwa kusaidia kutimua Gachagua

Na CECIL ODONGO October 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha ODM imebainika sasa kinaotea minofu zaidi ndani ya utawala wa Kenya Kwanza huku mabadiliko yakitarajiwa serikalini kufuatia kungátuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye bado anapambana kujinusuru mahakamani.

Iwapo mchakato wa kungátuliwa kwa Bw Gachagua utafaulu mahakamani, basi inakisiwa Rais atatekeleza mabadiliko kwenye baraza la mawaziri na kuwatema wandani wa Bw Gachagua, hatua ambayo itaifaa ODM.

Ushirikiano wa Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga ambao ulianza wakati wa maandamano ya Gen Z nchini miezi mitatu iliyopita, tayari ulichangia baadhi ya wanachama wa ODM kuteuliwa mawaziri kama malipo ya ‘hisani’ yao.

Walionufaikia uteuzi kama mawaziri ni Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo), Opiyo Wandayi (Kawi), Beatrice Askul (Jamuiya ya Afrika Mashariki) na John Mbadi (Fedha).

Masaibu ya Bw Gachagua na ushirikiano ambao wabunge wa ODM walizua na wenzao kutoka UDA kumngóa kwenye Bunge la Kitaifa na pia Seneti, sasa inaashirikia kuwa chama hicho cha upinzani kinatarajiwa kuvuna katika mabadiliko yajayo ya mawaziri pia kama malipo kutokana na ‘wema’wao.

Mnamo Jumamosi, Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed alilazimika kukanusha madai yaliyoenea mitandaono kuwa kuna mpango wa kumteua kwenye Baraza la Mawazi kuhudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani.

Bw Mohamed hakukataa wadhifa huo ila alisema yupo tayari kuwahudumia Wakenya kwenye wadhifa wowote ule japo akakanusha kuwa kuna mpango wa kumpokeza uwaziri.

Wizara ya Usalama wa Ndani imebakia wazi baada ya mshikilizi wake Profesa Kithure Kindiki kuteuliwa naibu wa rais japo bado hajachukua wadhifa huo rasmi kutokana na kesi ya Bw Gachagua mahakamani.

Hata hivyo, duru zinaarifu kuwa ODM imeanza mchakato wa kuunda mkataba wa kisiasa na Kenya Kwanza huku ikinyemelea hasa wadhifa wa Spika wa Bunge la Kitaifa unaoshikiliwa na Moses Wetangúla na Wizara ya Usalama wa Ndani.

Hapo jana, Mbunge wa Homa Bay mjini Opondo Kaluma na Seneta wa Migori Eddy Oketch waliandamana na Rais katika ibada ya kanisa kule Uasin Gishu ambapo walisema kuwa ODM itaendelea kuwa ndani ya serikali na kumuunga.

“ODM haiendi mahali na ipo ndani ya serikali hii kwa sababu tuko tayari kusaidia katika kuunganishwa Wakenya kwa ajili ya amani,” akasema Bw Kaluma, mwandani wa Raila akihitubu kwenye ibada hiyo jijini Eldoret.

Mbunge wa Makadara George Aladwa jana alisema kuwa hafahamu iwapo kuna mazungumzo ya wanachama zaidi wa ODM kuingia serikali ila wapo tayari kumsaidia Rais akiwaomba tena.

“Tulimfaa Rais na mawaziri na iwapo ataomba msaada tena, tupo tayari kwa sababu hata Junet ambaye madai yametanda kuwa atateuliwa waziri, anatosha kuhudumu katika nafasi hiyo,” Bw Aladwa akaambia Taifa Leo.

“ODM haijafunga milango yake kwa Rais mradi tu kinachofanyika kinawaunganisha Wakenya na tunashirikiana. Tukiombwa majina kama kutakuwa na mabadiliko, basi tutakuwa tayari kwa sababu sasa tuko serikalini,” akaongeza.

Kwa mujibu wa Mchanganuzi wa Kisiasa Martin Andati ambaye yupo katika kambi ya Raila, kuna mkataba ambao unasukwa kati ya ODM na UDA ili kugawa nyadhifa serikalini ili kuhakikisha udhabiti wa nchi na kwa ajili ya ushirikiano wa 2027.

“Kila upande una washirika wake na ODM inatarajiwa itanufaikia uteuzi zaidi. Mazungumzo hayalengi nyadhifa za uwaziri tu bali ule wa Spika, na Wizara ya Usalama wa Ndani,” akasema Andati.

Mchanganuzi Javas Bigambo anasema kuwa ODM ilitoa idadi ya kumngátua Bw Gachagua lazima kuwe na malipo na huenda kuna mkataba wa kisiri kati ya Raila na Rais ambapo hata wandani wa wanasiasa hao hawaujui.

“Kama kulikuwa na malipo kwa kumwokoa rais dhidi ya maandamano ya Gen Z basi hata hii ya Bw Gachagua lazima kuwe na malipo. Atakayeumia zaidi huenda akawa ni Wetangúla au Kingi kwa sababu ni wazi ODM inataka wadhifa wa juu zaidi ya uwaziri,” akasema Bw Bigambo.