Jamvi La Siasa

ODM yaibuka mchumba mjeuri, ikosoa serikali inayounga

Na  JUSTUS OCHIENG January 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MAZINGIRA ya kisiasa nchini Kenya yanashuhudia mabadiliko ya kipekee ambayo yanavunja mipaka kati ya serikali na upinzani, huku chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga kikidhihirisha sifa za undumakuwili – kupinga serikali huku kikiwa ndani ya Serikali Jumuishi.

Katika wiki moja iliyopita, chama hicho kilizidisha ukosoaji wake dhidi ya utawala wa Rais William Ruto, huku Bw Odinga na kaimu kiongozi wa chama Prof Anyang’ Nyong’o wakiionya serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya ‘siasa za ukandamizaji,’ kufuatia visa vya utekaji nyara.

Msimamo mkali dhidi ya serikali umewaacha wafuasi wa ODM wakikisia hatua inayofuata ya uongozi wa chama, huku wanachama wake watano wakiwa mawaziri na wengine wakinufaika kwa kuteuliwa kushikilia nyadhifa za juu serikalini wakiwemo washauri wa rais.

Mawaziri ambao ni wanachama wa ODM ni waliokuwa naibu viongozi wa chama cha ODM Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Majini) na Wycliffe Oparanya ( Ushirika), aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM John Mbadi (Wizara ya Fedha), aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi (Kawi na Petroli), na mwanachama wa zamani wa bodi ya uchaguzi ya chama hicho Bi Beatrice Askul ( Jumuiya ya Afrika Mashariki).

Zaidi ya hayo, Rais Ruto hivi majuzi aliteua washirika zaidi wa Bw Odinga katika nyadhifa kuu serikalini. Prof Adams Oloo, Bw Joe Ager na Dkt Sylvester Kasuku – washirika wote wa Bw Odinga – sasa ni sehemu ya Baraza la Washauri wa Kiuchumi la Rais Ruto.

Rais William Ruto (kulia) akiwa na Raila Odinga Homa Bay kwa hafla ya michezo. Picha|Hisani

Lakini hata viongozi hao wanaposhughulikia sera za Rais Ruto serikalini, na wakati huo huo kukumbatiwa na uongozi wa ODM, msimamo mkali wa hivi majuzi wa Bw Odinga na Prof Nyong’o dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza unaibua hisia.Mnamo Jumanne, Prof Nyong’o alilaani kukamatwa kwa waandamanaji wanaopinga utekaji nyara siku ya Jumatatu, akitaja hatua hiyo kama ‘ya kishenzi.’

Prof Nyong’o ambaye pia ni Gavana wa Kisumu alisema kukamatwa kwa Seneta wa Busia Okiya Omtatah pamoja na mamia ya waandamanaji hakuwezi kuvumiliwa.”Huu ni ukatili kabisa. Nilichoona kikitokea kwa Seneta Omtatah na wale waliokuwa wakifanya maandamano Nairobi hakiwezi, narudia hakiwezi kuvumiliwa Kenya leo,” Prof Nyong’o aliambia Taifa Leo.

Alikuwa akizungumza siku moja tu baada ya kutishia kuwa chama hicho kitaongoza maasi dhidi ya utawala wa Rais Ruto ikiwa utaendelea kuendeleza ‘siasa za ukandamizaji.’

Katika hotuba yake kwa taifa baada ya maandamano ya Jumatatu, Prof Nyong’o alisema:

“Ninamuomba Rais Ruto akomeshe aina hii ya ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji kwa amani na utekaji nyara wa Wakenya ambao kosa lao pekee ni kupinga kuvurugwa kwa demokrasia na Serikali.”

Bw Omtatah ni miongoni mwa waandamanaji wengine waliokamatwa Jumatatu, Desemba 30, pamoja na wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu wakati wa maandamano jijini Nairobi kupinga madai ya utekaji nyara.

“Tuko tayari kuongoza maasi dhidi ya siasa za kidikteta na dhuluma ambazo zinajaribu kulazimisha utawala dhalimu na usio wa kidemokrasia kwa watu kupitia mambo kama vile utekaji nyara na vitisho vya kisiasa,'”Prof Nyong’o alidai.

Aliendelea: “Kwa hiyo tunaionya sana serikali kukomesha utekaji nyara huu wa uoga wa wale wanaokosoa sera zisizo za kidemokrasia.”

Bw Odinga awali alikuwa ameonya kwamba, Wakenya hawawezi kuvumilia hali ya ujambazi, akitaka kukomeshwa kwa utekaji nyara ambao ulisababisha maandamano nchini kote Jumatatu.

“Haya ni matukio hatari sana. Ni kama Serikali ya mafia ambapo watu wanaofanana na maafisa wa polisi huwateka nyara Wakenya mchana peupe. Wanafanana na genge la jenerali Papa Doc Duvalier na kikosi chake cha wanamgambo wa Tonton Macoute ambao walikuwa wakiteka nyara watu na kuwatesa. Kwa hivyo hili si jambo ambalo tunaweza kuvumilia katika nchi yetu,” alisema.

Kinara wa ODM, Raila Odinga, akihutubia Baraza la Kitaifa la Usimamizi wa Chama (NGC) katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, hapo Aprili 18, 2024. PICHA | WILFRED NYANGARESI

Kauli ya Prof Nyong’o ilijiri huku Bw Odinga akijitenga na madai ya kuwa na handisheki na Rais Ruto.Bw Odinga alisisitiza kuwa chama cha ODM kilisaidia tu kuzuia nchi kutumbukia katika machafuko kufuatia maandamano makubwa ya Gen Z yaliyosababisha umwagikaji wa damu.

.Bw Odinga anamezea mate uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), azma ambayo imeidhinishwa kikamilifu na Rais Ruto.Kumekuwa na wasiwasi kuhusu msimamo wa chama cha ODM, huku afisa mmoja mkuu wa chama hicho akiambia Taifa Leo kwamba, wako katika ‘hali ya kuchanganyikiwa.

“Tulichonacho ni chama kinachokumbwa na mgawanyiko mkubwa; tuna ODM Serikalini (ODM-IG) na ODM katika upinzani (ODM-IO) na wakati fulani hatujui hata la kuwaambia wafuasi wetu ambao wanatutazamia kupata mwelekeo,” afisa huyo alifichua.

Naibu Katibu Mratibu wa ODM Caleb Amisi amemuonya Rais Ruto kuwaachilia vijana waliotekwa nyara la sivyo ajihatarishe kubeba msalaba pekee, akiongeza kuwa Bw Odinga na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye ana uhusiano mzuri naye hawatamuokoa.’

“Hili si ombi. Tafadhali watoeni hawa vijana kutoka mikononi mwa watekaji na muombe radhi taifa. Mimi ndiye pekee kutoka chama cha ODM mwenye ujasiri wa kukuambia ukweli,” akasema Bw Amisi ambaye pia ni Mbunge wa Saboti.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA