Raila ang’ang’aniwa Mlima Kenya kama mpira wa kona
BAADA ya mwaniaji wa Kenya, Raila Odinga katika uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kushindwa, sasa mirengo mbalimbali pinzani imeanza kumng’ang’ania.
Waziri huyo mkuu wa zamani sasa anang’ang’aniwa na wandani wa Rais William Ruto, kwa upande mmoja na wale wa aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua, kwa upande mwingine.
Wafuasi wa Bw Gachagua wamekuwa wakimtaka Bw Odinga arejelee siasa za kupigana na utawala mbaya na “kurekebisha hali inayoshuhudiwa nchini.”
Lakini wafuasi wa Rais Ruto wanapuuzilia mbali wito huo, wakisema kiongozi wa taifa pamoja na Bw Odinga wanafaa kuendelea kufanya kazi pamoja “kwa ustawi na umoja wa taifa”.
Naibu wa Rais, Prof Kithure Kindiki amemtaka Bw Odinga kuendelea kushirikiana kwa karibu na Rais Ruto na kumsaidia kustawisha umoja nchini, akisema kuwa licha ya kiongozi huyo wa ODM kupoteza wadhifa wa AUC alipata uungwaji mkono kutoka kwa mataifa 22.
“Tunamhimiza Rais na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kuendelea kufanya kazi pamoja katika kuunganisha nchi hii jinsi walivyoshirikiana kupigania kiti cha Umoja wa Afrika (AU),” Prof Kindiki akasema.
Alisema hayo Jumapili katika eneobunge la Imenti Kusini, Meru wakati wa hafla ya kumtawaza Askofu wa Kanisa la Kimethodisti, Jimbo la Nkubu, Stephen Mawira.
Lakini akimwelekezea ‘pongezi’ Bw Odinga kwa kuwa nambari mbili katika uchaguzi huo wa Jumamosi, Bw Gachagua alisema japo Afrika ilihitaji mchango wake, anahitajika zaidi nyumbani.
“Afrika ilikuhitaji lakini Mungu kwa hekima yake aliamua kwamba Kenya, na hasa Wakenya hawakuwa ‘wamemalizana’ nawe kama mwana wao mpendwa, hususan wakati huu tunapopania kulikomboa taifa hili katika utawala mbaya,” akasema katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook
Hata hivyo, akimjibu, Mbunge wa Mathira, Eric Wamumbi, ambaye ni mwandani wa Rais Ruto alisema “tumerejea nyumbani na tuna wajibu wa kutunza nchi hii. Sasa tunalenga kuwahudumia wananchi. Tuna kazi nyingi ya kufanya kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” akaambia Taifa Leo, kupitia ujumbe mfupi.
Akaendelea, “Katika kila uchaguzi huwa kuna mshindi na aliyeshindwa. Raila alishindwa lakini huo sio mwisho wa maisha. Kuna watu fulani kutoka kijijini mwetu (Gachagua) wanaotamani kwamba Raila arejee na aungane nao kuivuruga serikali. Kamwe hawatafaulu.”
“Raila na Ruto wataendelea kushirikiana kuiwezesha nchi hii kupiga hatua kubwa kimaendeleo. Wale wanaolenga siasa watafanya hivyo pekee yao huku viongozi hawa wawili wakishirikiana kuwahudumia Wakenya.”
Naye Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba, ambaye ni mwandani wa Gachagua, alikosoa jinsi kampeni za Bw Odinga zilivyoendeshwa.
Alisema kuwa kushindwa kwa kiongozi huyo wa ODM ni ishara kwamba marais wa mataifa ya Afrika hawana imani na Rais Ruto. Aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Laikipia, Cate Waruguru pia aliunga mkono kauli ya Bi Wamuchomba.
“Niling’amua kwamba Raila angepoteza nilipowaona zaidi ya wabunge, maseneta na magavana 100 wakijazana katika mkahawa wakiimba “Bado Mapambano”.
Hii iliwaogofya marais wa AU na wanadiplomasia wengine. Mchakato kama huo ni wa kidiplomasia na unahitaji upole wala sio mayowe,” akaeleza Bi Waruguru ambaye pia ni mshirika wa karibu wa Bw Gachagua.
Kwa upande wake, Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang’wa, mwandani mwingine wa Gachagua, alisema Bw Odinga alijitahidi kabisa lakini ushirikiano wake na Rais Ruto ndio ulimkosesha ushindi.
Mbunge wa Belgut, Nelson Koech naye alisema serikali ina mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa ushirikiano wa Rais Ruto na Bw Raila unadumu.
“Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Bw Raila anabaki na Rais Ruto, hata ikibidi turejee katika ripoti ya Nadco (Mazungumzo ya Mapatano baina ya Raila na Rais Ruto).”