Jamvi La Siasa

Ruto awateua marafiki wake aliofuta awali kurudisha ushawishi

Na MOSES NYAMORI, BENSON MATHEKA April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Rais William Ruto anaonekana kugeukia viongozi waliowahi kuhudumu serikalini, wakiwemo wale aliowafuta kazi kwa madai ya kutokuwa na uwezo, pamoja na wale waliohudumu katika serikali ya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, kama mkakati wa kuhakikisha anachaguliwa tena mwaka wa 2027.

Ahadi yake kwa wakazi wa Meru kwamba anapanga kumrejesha aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi, ni mwelekeo unaoonekana kulenga kuwaweka karibu baadhi ya washirika wake katika kampeni ya 2022 pamoja na kuwavutia mahasimu wake wa kisiasa.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi. Picha|Maktaba

Wachambuzi na wanasiasa wanasema kwamba hatua hiyo huenda ni mkakati wa kuzuia hali ambapo washirika wake wa karibu wa 2022 watajiunga na wapinzani wake kumkabili kwenye uchaguzi wa 2027.

Kwa kuwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua tayari anaongoza kampeni ya kumpinga Ruto katika eneo la Mlima Kenya lililomsaidia kushinda urais, kujiunga kwao na mrengo pinzani kunachukuliwa kama tishio kwa mipango ya rais ya kuchaguliwa tena.

Wakati wa ziara yake ya siku tano katika eneo la Mlima Kenya, Rais Ruto alifichua kuwa tayari anazungumza na Linturi na Peter Munya, wote waliowahi kuwa Mawaziri wa Kilimo.

“Peter Munya na rafiki yangu Mithika Linturi; tayari ninazungumza na viongozi hao wawili, na tuna mpango. Tulieni, kila kitu kiko sawa,” alisema Rais Ruto.

Baada ya maandamano ya vijana mwezi Juni 2024, Rais Ruto aliwafuta kazi mawaziri 12. Lakini ndani ya kipindi cha miezi minane tu, tayari ameajiri tena nusu yao, huku akiashiria kuwa wengine zaidi watarejeshwa kupitia nyadhifa mbalimbali za serikali.

Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria. PICHA | MAKTABA

Aliofuta kazi ni Prof Njuguna Ndung’u (Hazina na Mipango), Ezekiel Machogu (Elimu), Aisha Jumwa (Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi), Zachariah Mwangi Njeru (Maji), Eliud Owalo (Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali), Moses Kuria (Utumishi wa Umma,) na Mithika Linturi (Kilimo ).Wengine waliotemwa ni Ababu Namwamba (Vijana na Michezo), Simon Chelugui (Vyama vya Ushirika), Florence Bore (Kazi na Ulinzi wa Jamii), na Susan Nakhumicha Wafula (Afya).

Mnamo Agosti 23, 2024, Rais alimrejesha Bw Kuria kama Mshauri Mkuu katika Baraza lake la washauri wa Kiuchumi, na Bw Owalo kama Naibu Mkuu wa Wafanyakazi wa Ikulu anayesimamia Utekelezaji na Utoaji Huduma.Katika tangazo la gazeti rasmi la serikali Januari 17, 2025, Rais pia alimteua Bi Jumwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara Kenya kwa kipindi cha miaka mitatu.

Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu Eliud Owalo kwenye hafla ya awali. Picha|Hisani

Mnamo Januari pia aliwateua Namwamba (Mwakilishi wa Kenya katika UNEP) na Dkt Andrew Karanja, aliyehudumu kwa miezi mitatu tu kama Waziri wa Kilimo, kuwa Balozi wa Kenya nchini Brazil. Bi Margaret Nyambura, aliyehudumu pia kwa muda mfupi, alikataa uteuzi wake kama Balozi wa Kenya nchini Ghana.

Bi Nakhumicha ndiye wa hivi karibuni kurushiwa mnofu baada ya Rais Ruto kumteua kuwa Mwakilishi wa Kenya katika Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) lililoko Nairobi.

Mabadiliko ya hivi karibuni ambapo Rais aliteua watu 14 kuwa makatibu wa wizara pia yalionyesha mtindo wa kutumia tena maafisa wa serikali waliotemwa kwa kuwapa kazi za ubalozi.

 

Bw Alfred K’Ombudo, aliyekuwa Katibu wa Biashara, aliteuliwa kuwa Naibu wa Ubalozi wa Kenya mjini Brussels, Ubelgiji, huku mwenzake wa Michezo, Mhandisi Peter Tum, akitumwa Ubalozi wa Kenya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 

Prof Edward Kisiangani (Katibu wa Utangazaji na Mawasiliano) aliteuliwa kuwa Mshauri Mkuu na Mwanachama wa Baraza la Rais la Ushauri wa Kiuchumi, huku Geoffrey Kaituko, aliyewahi kuwa Katibu wa Masuala ya uchukuzi Baharini, akitumwa Ubalozi wa Kenya mjini Roma, Italia.Katika mahojiano ya hivi karibuni, Dkt Ruto alisema kuwa anaamini katika kuwapa watu nafasi ya pili.

Alitoa mfano wa aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi, ambaye alisema “hakuwa na uwezo wa kutosha” alipohudumu kama Mwanasheria Mkuu.

“Mimi ni mtu ninayeamini katika nafasi ya pili. Hata kama viongozi wengi hawakumpenda rafiki yangu Gachagua, bado nilimpa nafasi. Ninaamini kwamba ukiwa na marafiki, huwatupi kirahisi. Hii inamhusu pia JB Muturi. Hata kama ilikuwa vigumu kwake kufanya kazi kama Mwanasheria Mkuu, tulifanya kazi pamoja, tulifanya kampeni pamoja, nilikuwa tayari kumpa nafasi ya pili. Nilimpa nafasi, lakini baadaye alijiondoa mwenyewe. Ungetaka nifanye nini?” alihoji Rais.

Prof David Monda, mchambuzi wa siasa anayeishi Amerika, anasema mtindo huu unaathiri vibaya uongozi wa Rais Ruto, hasa kwa kutumia tena maafisa waliotemwa kwa sababu ya utendaji duni.“Mabadiliko haya ya kila mara pia huleta wasiwasi kwa umma kwani huduma kama bima ya afya ya kitaifa (SHA) huishia kutotekelezwa vizuri,” anasema.