Jamvi La Siasa

Ruto na Raila waandaa kikao kuhalalisha ndoa yao

Na  JUSTUS OCHIENG', BENSON MATHEKA August 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Wabunge wa Chama cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto na wale wa ODM cha Raila Odinga wanatarajiwa kukutana kwa mara ya kwanza chini ya paa moja siku ya Jumatatu kwenye kikao cha pamoja cha kundi la wabunge, ambacho, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, kinaweza kuelekeza ajenda ya serikali bungeni na pia mustakabali wa kisiasa wa nchi kuelekea uchaguzi wa 2027.

Kikao hicho cha faragha kinapangwa kufanyika katika Kituo cha Uongozi cha KCB kilichopo Karen, Nairobi, ambapo kitawaleta pamoja wabunge, maseneta na maafisa kutoka muungano mpana wa Kenya Kwanza.

Kwa mujibu wa Kiongozi wa Wachache Bungeni, Junet Mohamed ambaye anaratibu upande wa ODM, barua rasmi za mwaliko zilitumwa Ijumaa.

“Ajenda itahusu makubaliano ya vipengele 10 tulivyotia saini mwezi Machi, fidia kwa waathiriwa wa ghasia za kisiasa, na masuala mengine ya kitaifa,” alisema Mohamed.

Alipoulizwa iwapo mkutano huo utajadili uwezekano wa muungano kati ya ODM na UDA, Mohamed hakuthibitisha wala kukanusha, akisema tu: “Iwapo kuna mtu atapendekeza masuala ya muungano, yatajadiliwa.”

Barua ya mwaliko kwa wabunge wa ODM iliyosainiwa na Mohamed, inasoma kwa sehemu:“Waheshimiwa Wabunge, kulingana na mawasiliano yaliyotolewa na Rais Dkt William Samoei Ruto na Mheshimiwa Raila Odinga mnamo Alhamisi, Agosti,7 2025, napenda kuwafahamisha kuwa kutakuwa na kikao cha pamoja cha wabunge wa muungano wa Kenya Kwanza na ODM siku ya Jumatatu, Agosti 18 2025 saa tatu asubuhi katika Kituo cha Uongozi cha KCB, Karen.”

Odinga alidokeza kuhusu kikao hicho wiki iliyopita, akisema kitatoa mazingira mwafaka ya kujadili mkataba wa pande hizo mbili na namna ya kufidia waathiriwa wa maandamano.

Kikao hicho kinatarajiwa kujadili mswada na sera zinazotokana na makubaliano kati ya ODM na UDA.

Makubaliano hayo yanajumuisha utekelezaji kamili wa ripoti ya Kamati ya Mdahalo ya Kitaifa (NADCO), usawa wa bajeti, kuimarisha ugatuzi, kupambana na ufisadi, kuzuia uporaji wa rasilmali, kulinda uhuru wa kiraia na kukagua deni la taifa.

Aidha, suala la kulipwa fidia kwa waathiriwa wa maandamano na ghasia za kisiasa tangu mwaka 2017, ambalo limekuwa mada ya muda mrefu kwa Odinga, lipo kwenye ajenda kuu.

Wengi wanachukulia mkutano huu kama hatua ya mwanzo ya muungano wa kabla ya uchaguzi kati ya Ruto na Raila.

Rais Ruto na Odinga wamekuwa wakishirikiana kupitia serikali jumuishi, ambapo wandani wa Odinga wamepewa nyadhifa serikalini.

Baadhi ya washirika wa Odinga walioko serikalini ni aliyekuwa naibu wa chama Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Ushirika), aliyekuwa mwenyekiti wa ODM John Mbadi (Fedha), Opiyo Wandayi (Kawi ), na Beatrice Askul (EAC).

Wandayi alifichua kuwa Odinga amewapa maagizo ya wazi kuunga mkono Rais Ruto hadi 2032.
“Nimeelekezwa na kiongozi wetu Raila Amollo Odinga kushirikiana kikamilifu na Rais William Ruto hadi mwisho wa muhula wake – 2032,” alisema Wandayi akiwa Homa Bay.

Wandani wa pande zote mbili wanasema kikao cha Jumatatu kinaweza kuwa hatua rasmi ya kuanzisha muungano wa uchaguzi wa 2027, kama ule wa ‘Pentagon’ wa ODM mwaka 2007.

Naibu Rais Prof Kithure Kindiki pia ameashiria uwezekano wa muungano mpya akisema:“Ukimtazama Ruto, mimi na sasa Raila tukiwa pamoja, je, kuna mtu anaweza kutushinda kwenye uchaguzi?”

Viongozi wengine pia wameonyesha ishara za kushirikiana hadi uchaguzi wa 2027. Wabunge wa ODM kama Sam Atandi na Mark Nyamita wametaja uwezekano wa ‘Ruto-Tosha’ 2027.
Rais tayari ametekeleza baadhi ya matakwa ya ODM, ikiwemo mpango wa fidia – kama ishara ya nia njema kisiasa.

Seneta Oburu Oginga amesema: “Tupo kwenye serikali hii na hatuna nia ya kutoka hadi 2027.”
Gavana Gladys Wanga naye ameonya wakosoaji dhidi ya kupinga mwelekeo wa chama.

Jared Okello, Mbunge wa Nyando na mwanachama wa NEC ya ODM, amesema ODM itadai urais au unaibu rais katika mazungumzo yoyote ya muungano, pamoja na nusu ya wizara na taasisi za umma.

Mbunge wa Gem, Elisha Odhiambo, amesisitiza utekelezaji wa ripoti ya NADCO ili kuhakikisha ushirikishaji wa kisiasa.
“Tupo kwenye mchakato wa kuidhinisha ripoti ya NADCO, ambayo itaweka nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wawili – hili litasaidia kumaliza suala la ushirikishaji wa kisiasa,” alisema.

Mchambuzi wa siasa Dismas Mokua anasema kikao cha Jumatatu huenda ikawa kuzaliwa rasmi kwa ‘Pentagon 2’.
“Kenya huingia kwenye uthabiti wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi wakati Ruto, Raila, na Mudavadi wako pamoja,” alisema Mokua.

Lakini wakati huo huo, kundi jipya la wabunge vijana limeibuka chini ya mwavuli wa ‘Kenya Moja’, wakiahidi kupindua hali ya kisiasa.

Kundi hili linajitambulisha kama “Nguvu ya Tatu” tofauti na Ruto-Odinga upande mmoja, na Kalonzo-Gachagua upande mwingine.

Wanasema wanapigania maslahi ya vijana na makundi yaliyosahaulika, wakilenga kuleta “mabadiliko ya kizazi.”

Viongozi wake ni Edwin Sifuna, Babu Owino, Caleb Amisi na Gathoni Wa Muchomba — kutoka ODM na UDA.
Hadi sasa, kundi hilo lina wabunge 36 na maseneta 7 kutoka vyama tofauti.