Sifuna abashiri Ruto atashindwa hata akiungwa na Raila 2027
SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna amebashiri kwamba, Rais William Ruto atashindwa katika uchaguzi mkuu wa 2027 hata kama ataungwa mkono na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.
Kulingana na Bw Sifuna, ambaye ni katibu mkuu wa chama cha ODM, muungano wa Kenya Kwanza umeonyesha hauna uwezo wa kuongoza na umepoteza umaarufu na imani ya raia na kupunguza uwezekano wa kuchaguliwa tena.
Mwanasiasa huyo alisema hataunga utawala wa Ruto, wanavyofanya baadhi ya wanachama wa ODM.
“Hata kama ODM itaamuunga mkono Ruto, bado atashindwa. Kama chama hatuungi mkono masuala ya ndani au ya nje ya jinsi nchi hii inavyoendeshwa. William Ruto atashindwa katika uchaguzi ujao hata akiungwa mkono na Raila,”Bw Sifuna alisema akizungumza katika runinga ya Citizen TV jana asubuhi.
Seneta huyo anayehudumu muhula wa kwanza alisema kuwa, ODM itashirikiana tu na vyama vyenye maono sawa na vinavyoimarisha utawala ili kuboresha maisha ya Wakenya.
“ODM itashirikiana na vyama vya kisiasa ambavyo vina nia na maono sawa. Hamtatulazimisha tuingie katika muungano na watu wasio na uwezo na imedhihirika kuwa serikali ya Kenya Kwanza ndiyo isiyo na uwezo zaidi tangu uhuru,”aliongeza.
Kauli zake zinajiri huku baadhi ya viongozi wa chama cha ODM wakisisitiza kuwa, chama hicho kimeungana na serikali hasa baada ya kuundwa kwa Serikali Jumuishi.Mwenyekiti wa tawi la Nairobi la chama hicho, George Aladwa, ambaye ni mbunge wa Makadara amekuwa akipuuza Bw Sifuna kwa kukataa ODM inaunga serikali.
Washirika wa karibu wa Bw Odinga katika chama hicho, akiwemo kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed na mwenyekiti wa kitaifa Gladys Wanga wamekuwa wakitoa kauli zinazoashiria wataunga Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, Bw Sifuna alikanusha madai hayo akiunga Gavana wa Kisii Simba Arati ambaye amesisitiza kuwa chama hicho sio sehemu ya serikali ya Kenya Kwanza.