Jamvi La Siasa

Sifuna alivyotolewa pumzi akakubali handisheki ya Raila na Ruto

Na  RUSHDIE OUDIA March 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA walipokuwa wakisubiri kwa hamu kutiwa saini kwa makubaliano kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika Ukumbi wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) Ijumaa, macho yote yalielekezwa kwa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.

Bw Sifuna, Katibu Mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kwa miezi kadhaa alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais William Ruto na alikataa uwezekano wa ushirikiano wowote wa kisiasa kati ya ODM na chama tawala cha UDA.

Lakini Ijumaa, Machi 7 ilikuwa siku maalum kwa Katibu Mkuu huyo wa ODM ambaye pia ni msemaji wake. Alionekana kuwa amejiandaa vyema kwa hafla hiyo pamoja na mwenzake wa UDA, Hassan Omar.

Seneta huyo wa Nairobi alipewa jukumu la kusoma sehemu ya makubaliano 10 ambayo Rais Ruto na Bw Odinga walikubaliana ili kudumisha umoja, uthabiti na maendeleo. Alipopokea kipaza sauti kutoa hotuba yake ya utangulizi kabla ya kusoma sehemu ya kwanza ya makubaliano hayo, Bw. Sifuna alipigiwa makofi na waliohudhuria hafla hiyo KICC na kuibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii.

Katika hafla hiyo, Sifuna alionekana kuchanganya hisia, mara nyingine akionekana kutokuwa na raha na hali hiyo, huku wakati mwingine akikiri uhalisi wa mazingira tata ya kisiasa ya Kenya.

Kama mwanasiasa shupavu, Bw Sifuna alieleza wazi kuwa alikuwa hapo kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kama Katibu Mkuu wa ODM. Alisisitiza kuwa Mkataba wa Maelewano (MoU) hiyo yaliidhinishwa na kamati husika za chama cha ODM na akahakikisha kuwa makubaliano hayo si muungano wa kisiasa.

‘Tuliamua kusoma makubaliano haya ili sote tuelewe wazi maana yake. Kama Katibu Mkuu, nataka kuthibitisha kuwa yameidhinishwa na kama husika za chama,’ alisema Bw Sifuna, huku akiwataka wanachama wa Kamati Kuu ya Usimamizi ya ODM kusimama kama ushahidi.

Kisha aliendelea kusoma sehemu ya kwanza ya hati hiyo kabla ya kuikabidhi kwa Bw Omar.

Katika hafla hiyo, viongozi na Wakenya waliokuwa wakifuatilia kwenye mitandao ya kijamii walitoa maoni yao kuhusu uwepo wa Bw Sifuna katika sherehe ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo.

Wengine walihisi kuwa hakupaswa kushiriki kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya Rais Ruto, huku wengine wakiamini kuwa alifanya jambo la heshima kwa kusimama na kiongozi wake wa chama na kuhakikisha kuwa masuala aliyoyatetea kwa niaba ya chama yalijumuishwa katika makubaliano hayo.

Masuala haya ni pamoja na ushirikiano kati ya UDA na ODM kushughulikia changamoto zilizotajwa katika ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO), kulinda haki mbalimbali, kuongeza mgao wa bajeti kwa kaunti, kuhakikisha uadilifu na kudhibiti madeni miongoni mwa mengine.

Hata hivyo, hatua hiyo haikumuokoa machoni mwa wakosoaji wake waliomlaumu kwa msimamo wake wiki kadha kabla ya hafla hiyo.

Msimamo wake tofauti kuhusu makubaliano ya Ruto-Odinga ulianza kabla ya kuundwa kwa Serikali Jumuishi Julai mwaka jana.

Yeye na wanachama wengine wa ODM walishikilia msimamo mkali wakipinga ushirikiano na Kenya Kwanza, huku kiongozi wa chama na baadhi ya wanachama wakizidi kuwa na uhusiano wa karibu na serikali ya Ruto.

‘Iwapo Raila atasema atamuunga mkono Ruto mwaka 2027, nitaheshimu uamuzi huo, lakini nitamweleza kuwa kwa sababu nina mtazamo mpana wa nchi, wananchi wanasema kuwa ukimuunga mkono, atashindwa. Ndiyo maana nasema haya kwa msimamo thabiti. Binafsi, siwezi kumuunga mkono Ruto,’ alisema katika mahojiano mnamo Februari 20.

Aliposisitizwa kuhusu suala hilo, alisema msimamo wake wa sasa ni gharama ya kisiasa anayokubali kubeba kwa ajili ya nchi, akisisitiza kuwa Dk. Ruto atashindwa hata kwa msaada wa Bw Odinga kwa sababu rais amekosana na wananchi.

Bado haijulikani ikiwa atapunguza ukosoaji wake kwa serikali au ataendelea na msimamo wake mkali licha ya makubaliano mapya yaliyotiwa saini Ijumaa, ambayo yanatarajiwa kupelekea muungano wa vyama hivyo 2027.