Tangaza msimamo wako kamili kuhusu Ruto, Kalonzo aambia Raila
KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka amemtaka aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kutangaza wazi msimamo wake kuhusu uhusiano wa chama chake cha ODM na Serikali ya Kenya Kwanza.
Bw Musyoka alisema japo ODM inasisitiza kuwa haina mkataba wa ushirikiano na serikali ya Rais William Ruto, kujumuishwa kwa waliokuwa wake katika baraza la mawaziri kunatoa taswira tofauti.
Washirika wanne wa Bw Odinga walioteuliwa mawaziri ni John Mbadi( Fedha) Opiyo Wandayi( Kawi) Wycliffe Oparanya( Ushirika) na Hassan Joho ambao pamoja na Kiongozi wa Walio Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed ambaye amekuwa wakitetea vikali serikali licha ya kushikilia wadhifa wa upinzani.
Bw Raila amenukuliwa akisema alisaidia Ruto na wataalamu kutoka chama chake kurekebisha nchi huku Bw Junet akitangaza kuwa ndiye kiongozi wa upinzani katika Bunge la Kitaifa.
“Tangazeni msimamo ikiwa mko serikalini au katika upinzani kufuatia handisheki ya Ruto na Raila na uteuzi wa baadhi ya wanachama katika baraza la mawaziri. ODM haiwezi kutumikia mabwana wawili. Lazima iwe serikalini au katika upinzani,” Bw Musyoka alisema huku akidokeza kuhusu muungano mpya mapema mwaka ujao kwa kuunganisha viongozi ‘wenye nia moja na wao’.
Kukosa kutangaza msimamo kwa ODM, kunafanya chama hicho kuwa na tabia ya popo ambaye haeleweki iwapo ni mnyama au ndege huku kikiwa ndani ya serikali na wakati huo huo kudai kiko katika serikali.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna anashikilia kuwa kiko katika upinzani huku wadadisi wakisema kinalenga kudumisha nafasi za uongozi ndani ya mabunge. Alisema hayo akiwa eneo la Karurumo Kaunti ya Embu wakati wa mazishi ya Bi Gertrude Muthoni pamoja na viongozi wengine wa upinzani ambao walikashifu serikali kwa kujikokota katika kuunda upya tume ya uchaguzi.
Viongozi hao walitishia kuongoza maandamano kote nchini dhidi ya serikali kwa kuchelewesha kuunda Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.Waliambia serikali kuwa, nchi inapaswa kuwa na IEBC mpya kufikia Machi 2025 la sivyo wataingia barabarani kushinikiza ifanye hivyo. Viongozi hao walisema kukosekana kwa IEBC kunaweza kutumbukiza nchi katika mzozo wa kikatiba.
“Ikiwa serikali haitaunda IEBC kufikia Machi mwaka ujao, basi tutawaongoza Wakenya kuandamana dhidi yake,” alisema Bw Musyoka. Marehemu Muthoni ni mamake mwanahabari mpekuzi, John Allan Namu.
Wengine waliohudhuria ni kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni na aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ambao walisema kuchelewesha kuunda tume ya uchaguzi kunaweza kuathiri uchaguzi mkuu wa 2027.
Bw Wamalwa alisema wanachotafuta kwa kuunda muungano huo mpya ni kuondoa utawala mbovu Kenya, ufisadi na mikataba inayoshukiwa kuhusishwa na utawala wa UDA.
Naye Bw Kioni alipuuzilia mbali madai ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba, eneo la Mlima Kenya lina deni la kisiasa la Kalonzo kwa kumuunga mkono aliyekuwa rais, marehemu Mwai Kibaki.
Alisema kulipa madeni la kisiasa kumezua siasa za kikabila ambazo zimekuwa na madhara kwa mfumo wa kijamii wa nchi.
“Tunakataa kurejeshwa kwenye siasa za nani anadaiwa na nani. Cha muhimu ni kubadilisha nchi yetu kwa manufaa ya Wakenya wote lakini si kulipa madeni ya kisiasa,” alisema Bw Kioni.