UDA ni chama cha uongo, asema Gachagua
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa mara nyingi amewataka wakazi wa Mlima Kenya kutelekeza chama cha United Democratic Alliance (UDA) na wawe tayari kujiunga na chama kipya atakachozindua Mei mwaka huu.
Alipuuzilia mbali chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto akidai ndicho chanzo cha matatizo yanayowakumba wakazi wa eneo hilo.
“UDA ni nyumba iliyojaa shida, inaendeshwa kwa misingi ya uwongo na hivyo watu wetu wanapaswa kuigura,” akawaambia waombolezaji kwa njia ya simu katika kijiji cha Kinyakiiru, kaunti ya Kirinyaga jana.
Ilikuwa ni wakati wa mazishi ya matineja watatu, akiwemo mwanafunzi wa kidato cha tatu, waliokufa katika ajali ya barabarani eneo hilo.
Bw Gachagua aliwaambia wakazi wasiwe na wasiwasi, akiwaahidi kuwa chama hicho kipya kitawaokoa kutoka mateso.
“Miradi yote ya ujenzi wa barabara katika eneo hili zimesimama ilhali bima mpya ya afya ya kijamii (SHIF) haifanyi kazi. Wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka eneo hili wamesalia nyumbani kwa kukosa karo,” Bw Gachagua akaeleza huku akishangiliwa na waumini.
Alisikitika kuwa Mlima Kenya ilishiriki uchaguzi mkuu wa 2022 bila chama chao mahususi na ndio maana wanateseka sasa.
“Tusirudie kosa hilo tena. Tujihadhari tusiingie katika shimo hilo tena,” akaeleza Bw Gachagua. Vile vile, mwanasiasa huyo aliwashambulia wabunge kutoka Mlima Kenya waliunga mkono hoja ya kumtimua afisini, akiapa kwamba wataadhibiwa na wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“Wabunge hao walisaliti eneo la Mlima Kenya ili kutosheleza mahitaji ya tumbo zao,” akaeleza.
Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, Mwakilishi wa Kike Njeri Maina na diwani wa Baragwi David Mathenge waliunga mkono kauli ya Bw Gachagua. Walisema kamwe wakazi wa Mlima Kenya hawatachezewa shere tena.
“Tumebaguliwa na kuteswa kwa sababu hatuna chama cha kisiasa. Tunamtegemea Bw Gachagua atupe mwelekeo,” akasema Bw Murango.
Wanasiasa hao watatu pia walisema kuwa wenzao waliomsaliti Bw Gachagua wawe tayari kuadhibiwa na wapiga kura.
Matineja hao watatu walikufa siku moja kwenye ajali ya barabarani katika kaunti ya Kirinyaga.
Mazishi yao yalihudhuriwa na wanafunzi wenzao, walimu, wanakijiji na viongozi wa kisiasa.
Jamaa za marehemu waliangua kilio majeneza yenye miili ya wavulana hao yalipokuwa yakiteremshwa makaburini.
Wanenaji waliwaombeleza wavalana hao, waliokuwa waraibu wa mchezo wa kandanda, na ambao maisha yao yalikatizwa na ajali mbaya ya barabarani.