Uhuru ‘amalizana’ na Raila akikumbatia Matiang’i 2027
RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta sasa anaonekana kumtema kabisa Raila Odinga, kisiasa, kwa kuamua kuendeleza kampeni za kumpigia debe azma ya urais ya Waziri wa zamani Fred Matiang’i.
Ijumaa wiki hii Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni, anachoongoza Bw Kenyatta, alianza rasmi kampeni hizo katika kaunti ya Nyamira huku akiahidi kuelekea katika kaunti nyingine.
Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragua, alikutana, na kufanya mashauriano na Gavana wa kaunti hiyo Amos Nyaribo, huku akitangaza kuwa eneo la Mlima Kenya halitadhamini mgombea urais bali litaunga mkono azma ya Dkt Matiang’i.
“Nilifanya mashauriano na Gavana Nyaribo, kujadili mikakati ya kuvumisha mgombeaji wetu wa urais Fred Matiang’i. Ni mjadala muhimu unaohusu mustakabaliwa wa nchi yetu,” Bw Kioni akasema kupitia ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa X.
Katibu huyo Mkuu wa Jubilee aliongeza kuwa kuna jumla ya vyama 20 vya kisiasa ambavyo vimekuwa vikifanya mikutano ya kila wiki kupanga mikakati ya kuvumisha azma ya Dkt Matiang’i.
Mbali na chama cha United Progressive Alliance (UPA) kinachohusishwa na Dkt Matiang’i na Jubilee, Kioni hakufichua majina ya vyama vingine vinavyoshiriki mkakati huo.
Kulingana na wadadisi wa masuala ya siasa, juhudi hizi za Jubilee zimeshika kasi baada ya uamuzi wa Odinga kufanya kazi na Rais William Ruto baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) mwezi uliopita.
“Bila shaka kampeni hizi za Bw Kioni, zinafanywa kutokana na baraka za Bw Kenyatta ambaye ndiye kiongozi wa Jubilee. Ni wazi kwamba rais huyo wa zamani amevunjwa moyo na hatua ya Odinga kuungana na Rais Ruto na sasa ameamua kuendelea na mipango ya kumwandaa Matiang’i kwa uchaguzi wa urais wa 2027,” anasema Bw Martin Andati.
Mnamo Machi 5, siku mbili kabla ya Bw Odinga kutia saini mkataba wa ushirikiano na Rais Ruto, alifanya mkutano wa kisiri na Bw Kenyatta katika kaunti ya Kilifi, na kuibua dukuduku kuhusu uwezekano wake kubadili mpango wa kutia saini mkataba huo.
Bw Odinga alikuwa amezuru eneo la Pwani kushauriana na wafuasi wake kuhusu hatua ya kisiasa aliyopasa kuchukua baada ya azma yake ya kutwaa uenyekiti wa AUC kutibuka.Wawili hao (Odinga na Kenyatta) walionekana pamoja kwenye picha iliyozungushwa katika mitandao ya kijamii.
Waliandamana na Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro na mwandani wa Kenyatta David Murathe, ambaye pia ndiye naibu mwenyekiti wa Jubilee. Japo yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo hayakufichuliwa, wadadisi waliamini kuwa yalikita katika handisheki ambayo Bw Odinga alitarajiwa kufanya na Rais Ruto.
“Kuna uwezekano mkubwa kwamba Uhuru alijaribu kumshawishi Bw Odinga kutokubali kufanya kazi na Ruto. Huenda Uhuru alitaka Raila asalie katika Azimio na waikarabati upya kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2027 lakini Bw Odinga akakataa. Hii ndio maana sasa ameamua kumvumisha Matiang’i baada ya kuvunjwa moyo na msimamo wa Raila,” Bw Andati anaeleza.
Profesa Gitile Naituli anaonekana kukubaliana na kauli hii akisema kuwa Bw Kenyatta hajawahi kuonekana mwenye haja ya kumsaidia Rais Ruto kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
“Bila shaka, Uhuru hajajitolea waziwazi kumkumbatia Rais Ruto kisiasa. Hii ni licha ya kwamba Ruto amekuwa akijaribu kumvuta upande wake kwa kumtembelea nyumbani kwake Ichaweri, Desemba mwaka jana, kisha kuwateua wandani wake kuwa mawaziri,” anaeleza.
“Hii ndiyo maana baada ya kushindwa kumshawishi Raila kutoweka mkataba rasmi na Ruto, ameanza kampeni kamili za kumvumisha Matiang’i, Ruto naye akiamua kuzuru ngome yake ya Mlima Kenya kujaribu kunusuru ushawishi wake uliodorora kabisa,” Profesa Naituli anaeleza.