Jamvi La Siasa

Uhuru apigwa darubini kwa ukuraba wake na Ruto

Na MWANGI MUIRURI December 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

MKUTANO wa hivi majuzi kati ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Rais William Ruto unaendelea kuibua mjadala kuhusu sababu ya ukuruba kati ya viongozi hao wawili waliokuwa wametofautiana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Hasa, washirika wa aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua wanauliza ni kipi Bw Kenyatta anachoweza kumsaidia nacho aliyekuwa naibu wake ilhali kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, alisema hakuwa ameiva kuongoza na akamuunga mkono kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye hata hivyo alishindwa na Dkt Ruto.

‘Tunataka kuona jinsi rais huyo wa zamani atakavyofanya baada ya mkutano huo. Kila mtu ana hamu ya kuona jinsi Bw Kenyatta atakavyomsaidia Rais Ruto–ambaye alijaribu kila njia ili kuzuia asiingie madarakani– kujifufua mlimani,” akasema Mbunge wa Embakasi Kaskazini, Bw James Gakuya.

Bw Gakuya alishangaa jinsi Bw Kenyatta atakavyojipanga upya ili kufuta upinzani wake dhidi ya Dkt Ruto kati ya 2018 na 2022, ambaye wakati huo alikuwa naibu wake, na kumpigia debe Rais Ruto awanie muhula wa pili, ikiwa huo ndio mpango.

Rais Ruto (kulia) alipomtembelea Rais mstaafu Kenyatta nyumbani kwake Gatundu, Kiambu. PICHA | PCS

Mbunge wa Githunguri, Bi Gathoni wa Muchomba, alisema mkutano wa viongozi hao wawili hauna umuhimu wowote katika Mlima Kenya, akifananisha uhusiano wa Rais Ruto na eneo hilo na ule wa chungu kilichovunjika.

“Kulingana na sisi tumemalizana na utawala huu, tukakubali na kusonga mbele kusubiri wakati 2027,” Bi Wa Muchomba alisema na kuongeza kuwa “mashinani mambo hayajabadilika kuhusu jinsi utawala huu unavyosawiriwa na tunaendelea kujipanga upya kama nguvu mbadala.”

Baada ya kuungana mwaka 2013 katika muungano ambao haukutarajiwa wakiandamwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), wawili hao walishinda urais huku Bw Kenyatta akiwa rais na Bw Ruto naibu wake.

Lakini baada ya uchaguzi wa 2017 na Rais Kenyatta aliporidhiana na aliyekuwa mpinzani wake, Bw Odinga, mnamo 2018, uhusiano kati yake na Dkt Ruto ulidorora. Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022, Rais Kenyatta alikosana na naibu wake na akamfanyia kampeni Bw Odinga. Mlima Kenya ulimkaidi na Dkt Ruto alimshinda Bw Odinga kwa kura chache.

Lakini kufuatia sera zisizopendwa za utawala wake katika miaka miwili iliyopita, chuki dhidi ya Rais Ruto imekuwa ikiongezeka katika Mlima Kenya.

Hatua ya Rais Ruto kuridhiana na Bw Odinga kisha kutea washirika wake katika Baraza la Mawaziri baada ya maandamano yaliyoongozwa na vijana wa Gen Z, ilizidisha mpasuko Mlima Kenya.

Kutimuliwa kwa Bw Gachagua kama naibu rais kumezidisha uasi unaoongezeka katika Mlima Kenya. Uasi ni mkubwa sana hivi kwamba wakazi hao wamekuwa wakielezea kutoridhika kwao na utawala wa Rais Ruto, na na kumkashifu yeye na wafuasi wake katika shughuli za umma.

picha raila ruto

Vile vile, kutimuliwa kwa Bw Gachagua kutoka serikali ya Kenya Kwanza, kumemfanya Bw Kenyatta kuwa mwanasiasa maarufu hasa kutokana na ushauri wake kwa wakazi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 ambao wakazi walikaidi.

“Hali ilivyo sasa imetufanya tuangalie tena hali yetu ya kisiasa hadi sasa. Kuna yale ambayo rais wa zamani Kenyatta alikuwa akituambia kuhusu naibu wake na kwa nini alikuwa akipinga asiingie madarakani. Lakini tulitilia shaka. Sasa tunajua alikuwa sahihi,” Bw Gachagua aliambia runinga ya NTV hivi majuzi kwenye mahojiano.

Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee cha Bw Kenyatta Bw Jeremiah Kioni, amepuuzilia mbali mkutano kati ya viongozi hao wawili, lakini wadadisi wengi wanaamini kuwa huo ni mwanzo wa muungano mpya kabla ya uchaguzi wa 2027.

“Ninaweza kukuambia bila uoga kwamba mkutano kati ya wawili hao haukuwa na nia mbaya. Kiongozi wa chama chetu hana nia ya kujumuishwa serikalini au kusaidia utawala ulio madarakani,” Bw Kioni alisema.

“Unakumbuka kwamba Bw Kenyatta katika urais wake alishauriana na kiongozi wa upinzani kisha Bw Odinga…lakini hakuwahi kumuingiza katika serikali. Huo ndio uhusiano ambao Bw Kenyatta anatamani katika serikali hii. Atoe ushauri, lakini bila nia ya kuingia serikalini,” akaongeza.

Hata hivyo, mshauri wa Rais wa masuala ya uchumi Bw Moses Kuria kwenye taarifa yake kwa umma, aliashiria mkutano kati ya viongozi hao wawili ulikuwa mwanzo wa mwelekeo mwingine wa siasa hasa katika eneo la Mlima Kenya.

Bw Kuria alitaja uwezekano wa mkutano huo kuibua ajenda ya marekebisho ya katiba ambayo huenda ikarejesha Mpango wa Maridhiano ( BBI).Mpango huo ulilenga kuunda maeneo bunge zaidi ikiwa ni pamoja na katika Mlima Kenya, kuanzisha mfumo wa kura moja ya mtu mmoja na kuunda wadhifa wa Waziri Mkuu..

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA