Jamvi La Siasa

Walionja mamlaka na kuporomoka 2024

Na BENSON MATHEKA January 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWAKA wa 2024 ulishuhudia kuporomoka kwa baadhi ya watu waliokuwa na ushawishi serikalini baada ya kuonja mamlaka kwa muda mfupi.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua aliondolewa mamlakani baada ya kuhudumu kwa miaka miwili.

Aidha, aliweka historia kwa kuwa Naibu Rais wa kwanza kabisa kuondolewa afisini. Kuondolewa kwake pia kulimfanya kuwa afisa wa juu zaidi wa umma kuondolewa afisini.

Iwapo hatashinda kesi yake katika Mahakama Kuu huenda akazimwa kushikilia wadhifa wowote wa umma kwa miaka kumi ijayo.

Bw Gachagua amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala ambao alikuwa akitetea akiwa ofisini huku akimlaumu Rais Ruto kwa masaibu yake, kuteka nyara raia, kusimamia utawala uliojaa ufisadi na kubebesha raia mzigo wa ushuru.

Cleophas Malala

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala. Picha|Maktaba

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala aling’atuliwa kutoka wadhifa huo kufuatia ushirika wake na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Kwa kuondolewa kama katibu wa UDA, Malala alipoteza ushawishi aliokuwa nao katika chama tawala.

Sawa na Gachagua, amegeuka kuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa Rais Ruto na utawala wake.

“Inakuwaje wewe, Rais William Ruto, kuwa na uchungu hivyo? Naibu wako ni mgonjwa hospitalini na bado unapambana naye. Rais tulikusaidia na kusimama na wewe, lakini hatukujua ungekuwa mtu asiyejali marafiki zake. Tunamwachia Mungu kila kitu,” Malala alinukuliwa akisema katika mahojiano na gazeti moja la nchini Oktoba 2024.

Dkt Susan Nakhumicha

Aliyekuwa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha akihutubu katika hafla ya awali. Picha|Maktaba

Aliyekuwa Waziri wa Afya wa kwanza katika serikali ya Kenya Kwanza Dkt Susan Nakhumicha ni miongoni mwa wale ambao hawakurejeshwa kazini Rais Ruto alipounda baraza la pili la mawaziri baada ya kutimua la kwanza.

Hajapatiwa wadhifa wowote kufikia sasa.

Tangu kutimuliwa kwake, Nakhumicha amedumisha hadhi ya chini lakini aliwahi kupata umaarufu baada ya video yake kusambazwa akimwambia Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Kenya Jackson Ole Sapit ‘kumuombea,’ akikiri kwamba maisha baada ya kufutwa kazi hayakuwa rahisi.

Bw Mithika Linturi

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi. Picha|Maktaba

Waziri wa zamani wa Kilimo Bw Mithika Linturi alikuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri la kwanza la Rais Ruto alipoingia mamlakani mwaka wa 2022 na hakurudishwa kazini baada ya Rais Ruto kuvunja Baraza lake la Mawaziri kufuatia maandamano ya Gen Z yaliyoshuhudiwa mwaka huu.

Kwa muda alikuwa ametulia lakini mwezi jana alijitokeza kulalamikia kile alichodai kuwa ubaguzi katika uteuzi serikalini.

Bi Aisha Jumwa

Aliyekuwa Waziri wa Jinsia na Utamaduni. Picha|Maktaba

Mbunge wa zamani wa Malindi Bi Aisha Jumwa pia alipoteza wadhifa wa uwaziri na amekuwa nje kwenye baridi tangu wakati huo.

Jumwa alijiunga na serikali ya Rais Ruto kama Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Sanaa lakini akapoteza nafasi yake baada ya Rais kuunda Serikali Jumuishi.

Ameapa hatabanduka kwa Ruto.

 Simon Chelugui

Aliyekuwa Waziri wa Ushirika na biashara ndogo ndogo. Picha|Maktaba

Bw Simon Chelugui alikuwa waziri wa pekee ambaye Rais Ruto alirithi kutoka serikali ya Jubilee na kumteua kusimamia wizara ya Ushirika ambapo alisimamia kuanzishwa kwa Hazina ya Hasla miongoni mwa sera nyingine za Serikali ya Kenya Kwanza.

Hata hivyo, alipovunja baraza lake la mawaziri baada ya maandamano ya Gen Z hakumrejesha kazini.

Japhet Koome

Aliyekuwa Inspekta Jenerali wa kwanza chini ya utawala wa Kenya Kwanza Japhet Koome alilazimika kujiuzulu kufuatia malalamishi ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji waliokuwa na amani.

Koome alihudumu kama mkuu wa polisi kwa chini ya miaka miwili.