Wasiwasi kuhusu mabadiliko serikalini iwapo ‘mwenye hisa’ Gachagua atatimuliwa
WASIWASI umekumba maafisa wakuu katika utawala wa Rais William Ruto kuhusu uwezekano wake kufanywa mabadiliko serikalini baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kutimuliwa.
Duru zinasema kuwa mabadiliko hayo yanaweza kufanyika hata katika uongozi bungeni na uongozi wa kamati mbalimbali.
Mabadiliko bunge yatafanywa kwa misingi ya nafasi ya baadhi ya wabunge katika mchakato wa kuondolewa kwa Gachagua kwani huenda wandani wake wakaathirika pakubwa.
Katika Serikali Kuu, huenda Rais akafanya mabadiliko katika Makatibu wa Wizara ili kuendeleza masilahi ya wandani wapya akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Mnamo Julai mwaka huu, Rais Ruto aliwafuta kazi mawaziri wake 21 kutimiza matakwa ya vijana wa Gen Z waliofanya msururu wa maandamano kupinga serikali yake.
Alishirikisha wandani wa Bw Odinga katika baraza jipya la mawaziri aliloliunda.
Inaaminika kuwa Bw Gachagua alikuwa na ushawishi mkubwa katika teuzi kuu serikali tangu Dkt Ruto alipoingia mamlakani mnamo Septemba 2022.
Baadhi ya wale ambao alishawishi uteuzi wao huenda wangali waaminifu kwake, hali ambayo huenda ikiwagharimu pakubwa endapo Gachagua atatimuliwa.
Katibu Mratibu wa UDA Vincent Musyoka (Mbunge wa Mwala) aliambia Taifa Leo kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa Rais Ruto atafanya mabadiliko serikalini.
Alisema hatua ya kwanza itakuwa ni kumteua yule atakayejaza nafasi ya Gachagua, endapo atatimuliwa.
Hata hivyo, alisema wale wanaoshikilia nyadhifa zingine kuu watawekwa katika mizani kwa misingi ya utendakazai wao sio kwa misingi ya yule aliyewasilisha majina yao ili wateuliwe.
“Mabadiliko serikalini yataanza na kujazwa kwa nafasi ya Gachagua. Nakuambia kuwa Rais ni mtu ambaye anaweza kufanya mambo ya kushtua. Ikiwa wewe ni waziri au katibu wa wizara na unafanya kazi yako vizuri bila kuhujumu serikali kutoka ndani, uhusiano wako na mtu mwingine hauwezi kutumika kama msingi wa kukubadilisha au kukufuta kazi,” akasema Bw Musyoka, almaarufu Kawaya.
“Rais Ruto anawaelewa zaidi maafisa wake. Utashangaa kupata kwamba yule ambaye jina lake liliwasilishwa na mtu mwingine anayo uhusiano wa karibu zaidi naye,” akaeleza Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Kawi.