Jamvi La Siasa

Waziri aliyegeuka mhubiri baada ya kustaafu siasa

Na N KENYA YEAR BOOK March 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

JAMES Kabingu Muregi alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Nyandarua Kusini mwaka wa 1969 na akashikilia kiti hicho hadi 1979.

Kuanzia 1975, Muregi alikuwa Naibu Spika wa Bunge baada ya kuzuiliwa kwa Jean-Marie Seroney.Seroney alifungwa jela pamoja na Martin Shikuku kwa kudai chama tawala, Kenya African National Union (KANU), kilikuwa kimekufa.

Shikuku alisema Bungeni kuwa chama hicho kilikuwa kimekufa lakini alipotakiwa kuthibitisha madai yake, Seroney, ambaye alikuwa Naibu Spika wakati huo, alisema, “Hakuna haja ya kuthibitisha mambo yaliyo wazi!” Yeye, Shikuku na wengine wachache walikuwa wakosoaji wa mara kwa mara wa utawala wa Rais Jomo Kenyatta.

Muregi alikuwa mtu anayeunga mkono Serikali na mtetezi mkali wa Muungano wa Gikuyu, Embu na Meru (GEMA), vuguvugu la uliokuwa mkoa wa Kati, wakati wa utawala wa Kenyatta.

Mnamo 1979, alipoteza kiti cha Nyandarua Kusini kwa Kimani wa Nyoike, na baada ya hapo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Pareto ya Kenya. Kufikia wakati huo, alikuwa mshirika wa karibu wa Rais Daniel arap Moi, ambaye alimrithi Kenyatta mnamo Agosti 1978.Mnamo 1988, Muregi alikuwa mbunge wa kwanza wa eneobunge la Kipipiri.

Alipoteza kiti chake kwa Laban Muchemi mwaka wa 1992 baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi kufuatia kuondolewa kwa Kifungu cha 2A cha Katiba ya Kenya.

Mnamo Oktoba 1989, wakati wa kilele cha msimu ambao viongozi waliopaza sauti ya ‘nyayo’ walionekana kuwa waaminifu zaidi kwa Rais, serikali yake, na KANU, Muregi aliteuliwa kuwa Waziri Msaidizi wa Mazingira kuchukua nafasi ya Josiah Kimemia, Mbunge wa Kinangop.

Kimemia wakati huo alichukuliwa kukosa uaminifu wa kutosha kwa rais na chama tawala, na hivyo basi akang’olewa madarakani.Vibaraka wa chama kutoka tawi la KANU la Nyandarua, pia walitaka aondolewe kama mwenyekiti wa tawi; nafasi yake ilichukuliwa na Muregi.

Mara baada ya kuteuliwa katika Serikali, Muregi alionyesha uaminifu wake kamili kwa Moi kwa kukosoa vikali wale walioonekana ‘kupinga nyayo.’Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Muregi aliteuliwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo lakini hakudumu kwa vile alipoteza kiti cha eneobunge la Kipipiri kwa Muchemi.

Mara tu baada ya kupoteza kiti hicho, wanasiasa wanachama wa KANU walianza kumezea mate wadhifa wake wa chama. Alibadilishwa kama Mwenyekiti wa Tawi la KANU la Nyandarua na Kimemia, mtu ambaye alikuwa amemwondoa hapo awali.

Mnamo Mei 1994, tawi la chama lilidai kumwondoa kama Mwenyekiti wa Tawi Ndogo ya Kipipiri kwa madai ya kutomuunga mkono Moi na maafisa wakuu wa KANU.

Lakini alisema hakuwa na hatia na kumshutumu Kimemia kwa kujaribu kummaliza kisiasa. Wiki moja baadaye, katika hatua ya kushangaza, baraza kuu la Kanu lilimrudisha kitini. Mwenyekiti wa tawi na hasimu wake wa kisiasa, Kimemia, aliwaambia waandishi wa habari wakati huo kwamba tawi lilimrejesha Muregi ‘kunyima upinzani katika wilaya nafasi ya kusherehekea mzozo katika chama’, kama ilivyoripotiwa katika Daily Nation la Mei 17, 1994.

Muchemi alipofariki mwaka wa 1995, KANU ilitarajia kutwaa tena kiti cha Kipipiri na Serikali ikamfanyia kampeni mgombeaji wake, Joe Maina, na kuwaahidi wakazi umeme katika eneobunge nzima.

Lakini Maina alishindwa na Githiomi Mwangi wa Democratic Party vigingi vilivyokuwa vimetapakaa eneobunge hilo tayari kwa mpango wa kusambaza stima vilirejeshwa mara moja. Hasara ya KANU ilichangiwa na kutengwa kwa vigogo wa tawi la chama waliomjumuisha Muregi.

Waziri huyo wa zamani alianza kuhubiri baada ya kuacha siasa za uchaguzi na leo ni askofu ambaye kanisa lake linahudumu Nyandarua na viunga vyake.

Katika mahojiano ya simu mapema mnamo 2021, mtoto wa kiume wa Muregi, Mchungaji Moses Ndungu, alisema babake alizaliwa Elburgon mwaka wa 1934, ambapo babu yake alifanya kazi katika moja ya mashamba ya walowezi kutoka Ulaya.

Muregi alihudhuria Shule ya Msingi ya Micinda na baadaye akajiunga na taasisi ya afya huko Nyandarua ambako alisomea kozi ya afya ya umma. Aliajiriwa kama afisa wa afya ya umma huko Nyandarua, ambapo miongoni mwa masuala mengine alitoa ufahamu kuhusu matumizi sahihi ya vyoo. Alipokuwa akifanya kazi Nyandarua, Muregi alinunua shamba na kuwahamisha wazazi wake kutoka Elburgon.