JAMVI: Sababu za Uhuru kuogopa kuitisha kikao Jubilee
Na CHARLES WASONGA
IMEBAINIKA kuwa Rais Uhuru Kenyatta anasita kuitisha mkutano wa kundi la wabunge wa chama cha Jubilee kwa hofu ya kuaibishwa kwa kuelekezewa lawama kuhusu migawanyiko inayotokota ndani ya chama hicho.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa tuliozungumza nao wanasema Rais Kenyatta anawakwepa wabunge wanaegemea mrengo wa naibu wake William Ruto wanataka ufafanuzi kuhusu dhima ya muafaka kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
“Wabunge hao ambao ni wanachama wa ‘Team Tanga Tanga’ pia wamebainisha wazi kwamba wangemtaka Rais Kenyatta awaeleze waziwazi ikiwa ahadi yake ya kumuunga Ruto kama mrithi wake 2022 ingalipo au la. Rais anafahamau mipango hii na ndio maana amekuwa akitumia majukwaa mengine kuwajibu wabunge hao,” akasema Bw Javas Bigambo.
Wiki jana, Rais Kenyatta alionekana akijibu madai ya wabunge hao kwamba muafaka huo, maarufu kama handisheki, unalenga kumsaidia Bw Odinga kuingia Ikulu 2022 akisema hawajawahi kujadili suala hiyo katika mazungumzo yao na kiongozi huyo wa ODM.
Aidha, alipuuzilia mbali dhana kwamba uhusiano huo unalenga kuivunja Jubilee na kudidimiza ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.
“Huyu Raila hajaniambia anataka kuwa Rais 2022; na sijamwambia ninataka kuwa rais 2022. Tumekuwa tu tukijadili masuala yanayowaathiri watu wetu. Ikiwa ni miundo mbinu, tumekuwa tukijadili kile ambacho tunapaswa kufanya kujenga barabara zaidi.
“Tunajadili, tunasaidiana na kukubaliana,” Rais Kenyatta akasema alipohutubu katika mkutano wa kujadili ufadhili wa miradi ya miundo msingi barani Afrika ulioandaliwa katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.
Mwenyeji wa mkutano huo alikuwa Bw Odinga, ambayo ni balozi wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundo Msingi.
“Ikiwa ni masuala ya afya, huwa ananielekeza kuhusu kile ambacho tunapaswa kufanya. Sisi huketi, kujadiliana na kukubaliana. Yeye pia hunipa mawaidha kuhusu jinsi ya kuimarisha kile ambacho tunafanya. Sasa kuna kosa gani hapo? Rais Kenyatta akauliza.
Alisema mustakabali wa wananchi na taifa la Kenya kwa jumla ndio nguzo muhimu inayohimili muafaka kati yake na Bw Odinga.
Lakini siku moja baada ya Rais kutoa kauli hiyo, Dkt Ruto alioenakana kumjibu alipodai kuwa, “kuna watu mahali fulani ambao wanawachukulia Wakenya kama wajinga.”
Watu ambao, alisema, aidha wanadhani Wakenya hawajui kinachoendelea au wanaamini kuwa Wakenya hawajui nani atakuwa rais wao.
“Kuna watu fulani ambao wanadhani Wakenya ni wajinga. Wakenya wanajua ni nani atakuwa rais wao. Koma kutuletea siasa. Kuna uhaba mkubwa wa wajinga nchini,” Ruto akasema alipohutubia hafla ya Kanisa mjini Nyeri.
Bw Bigambo anasema ni hali kama hii ambapo Rais Kenyatta na naibu wake wameonekana kukinzana waziwazi kuhusu suala hilo la handisheki ambayo imeendelea kuzua tumbojoto ndani ya Jubilee na kufifisha juhudi zozote za kuitishwa kwa mkutano wa kundi la wabunge wake (PG).
“Isitoshe, Rais na naibu wake wametofautiana hadharani kuhusu suala nyeti la vita dhidi ya ufisadi. Rais ameonekana kuunga mkono uchunguzi unaoendeshwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuhusu sakata ya wizi wa Sh21 bilioni za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer lakini Dkt Ruto anampiga vita Bw Kinoti kwa kudai anatumiwa na mahasidi wake kuhujumu ndoto yake ya urais 2022 kwa kulenga wandani wake,” anasema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maseno Tom Mboya anayeshilikia kuwa ni hali kama hiyo ambayo imelemaza juhudi za kuitishwa kwa mkutano wa PG wa Jubilee.
Akiguzia shinikizo hizo za kuitisha mkutano wa PG, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju anasema hamna “mgogoro wowote ndani ya chama chetu wa kuhitaji kujadiliwa katika mkutano kama huo.”
“Kiongozi wa Jubilee Bungeni Aden Duale hajawasilisha ombi kama hilo kwa uongozi wa chama. Kwa hivyo, wale wanaoitisha mkutano huo kupitia mikutano ya hadhara au ya mazishi wanafaa kuelekeza maombi yao kwa Duale. Kufikia sasa hamna ombi kama hili limepokewa ishara kwamba hamna mgogoro au masuala ya kujadiliwa,” anasema Bw Tuju ambaye pia ni Waziri asiye na Wizara ya Kusimamia.
Kwa upande wake Bw Duale, ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini, anasema wajibu wa kuitisha mkutano wa PG sio wa Rais Kenyatta.
“Wale wanataka mkutano huo wanafaa kuwasilisha maombi yao kwa afisi yangu… kisha nitawasiliana na kiongozi wetu Rais Kenyatta na naibu wake Dkt Ruto ili tukubaliane kuhusu ajenda ya mkutano kama huo. Kufikia sasa hamna sijapokea ombi rasmi kutoka kwa mbunge yeyote,” Duale akaambia jarida la Jamvi.
Lakini kulingana na wabunge wandani wa Dkt Ruto, kutoitishwa kwa mkutano huo ndio sababu ya uwepo wa mgawanyiko unaoshuhudiwa katika chama hicho wakati.
Wanasema kuwa endapo mkutano huo hautaishwa hivi karibuni huenda hali hiyo ikadidimisha nafasi ya chama hicho tawala kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao mwaka wa 2022.
Mbunge wa Bomet ya Kati Ronald Tonui anasema wabunge wa Jubilee wanakinzana kimawazo kuhusu masuala ya kitaifa kwa sababu mkutano wa PG haujaitishwa ili waweze kuchukua msimamo mmoja kuhusu masuala hayo, hususan utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu ya Serikali.
Bw Tonui na wenzake wanasema kuwa Rais Kenyatta hajawahi kukutana na wabunge wa Jubilee kujadili suala hilo ambalo linavumishwa na serikali katika muhula wake wa pili afisini.
“Tulifanya mkutano wa mashauriano kupanga marudio ya uchaguzi wa urais mnamo Septemba baada ya mahakama ya juu kufutilia mbali ushindi wa raia Kenyatta. Mkutano mwingine ambao tulifanya na Rais ni pale alipokuwa akitaka kuwalazimisha wabunge kupitia Mswada wa Kifedha wa 2018 Novemba mwaka jana,” akasema Tonui.
Kulingana na mbunge huyo, inaonekana Rais Kenyatta anakwepa mkutano wa PG kimakusudi.
“Dhana inayojitokeza ni kwamba Rais ameanza kuwasawiri wabunge kama maadui wake badala ya kuwa washirika katika chama cha Jubilee na katika shughuli za kuendesha serikali.
Naye mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri anasema malumbano baina ya wabunge na Rais kwa upande mmoja na Naibu Rais kwa upande mwingine ni ishara ya kukita kwa migawanyiko ndani ya Jubilee.
“Kutoitishwa kwa mkutano wa PG kumeibua minong’ono na uvumi kuhusu mipango ya chama hiki tawala kuhusu urithi wa kiti cha urais na hatuwezi kunyamaza ikiwa mambo hayaendeshwi sawasawa,” akasema Bw Ngunjiri.
Sawa na wenzake, mbunge huyo anachukulia kuwa muafaka kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga pia umechochea mikinzano zaidi ya kimawazao na kimasilahi kati ya Rais na Naibu wake.