JAMVI: Urafiki wa Uhuru na Maraga unavyotisha kuzima uhuru wa mahakama
Na VALENTINE OBARA
UHURU wa mahakama unazidi kutiliwa shaka kufuatia jinsi Jaji Mkuu David Maraga anavyoonekana kuwa karibu sana na Rais Uhuru Kenyatta.
Tukio la wiki mbili zilizopita ambapo Bw Maraga alihudhuria hafla iliyosimamiwa na Rais katika Kaunti ya Kisii ilisababisha malalamishi makali kutoka kwa baadhi ya wananchi na viongozi waliomtaka akome kuandamana na wanasiasa katika misafara yao.
Kilichoshangaza wengi ni kwamba Jaji Mkuu hakuhudhuria tu hafla hiyo ya kuzindua Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii, bali alikuwa miongoni mwa waliomkaribisha Rais Kenyatta na picha zikasambazwa akiwa amesimama kwenye umati kusikiliza hotuba za viongozi wa kisiasa barabarani.
Wachanganuzi wa kisiasa wanasema hali hii ni hatari kwa maamuzi yatakayotolewa katika kesi za miradi ya mabilioni ya pesa ambapo walalamishi wanaamini utekelezaji haukufuata sheria au zabuni kutolewa isivyofaa.
“Hali hii ni hatari kwa kuwa afisi ya rais ikiachwa iingilie uhuru wa mahakama, inamaanisha hata mtu akienda kortini kushtaki serikali kwa mfano kutaka miradi inayofuja pesa za umma isitishwe, serikali inaweza ikapendelewa katika maamuzi,” akasema mtaalamu wa kisiasa, Bw Holo Oiro.
Hakika, ilibainika miradi ya Sh350 bilioni ya serikali kuu imekwama kwa sababu ya kesi zinazoendelea.
Mkutano huo wa Kisii ulioibua ghadhabu kali ulikuwa pia umehudhuriwa na Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga miongoni mwa wengine.
Hii haikuwa mara ya kwanza Bw Maraga kuhudhuria mkutano unaosimamiwa na Rais Kenyatta ambao machoni mwa wakosoaji wake, hakuhitaji kuwepo.
Mikutano mingine ambayo amewahi kuhudhuria ni ule wa Rais na wawakilishi wa Shirikisho la Wawekezaji wa Kibinafsi Kenya (KPSA) uliofanywa katika Ikulu ya Nairobi, na kongamano la wadau mbalimbali kuhusu ufisadi.
Wakosoaji wake hulalamika kwamba Jaji Mkuu anapaswa kuwa na uhuru kimamlaka unaoonekana wazi na hivyo basi kila anapoonekana kuwa karibu au kunyenyekea mbele za Rais, inachukuliwa kuna vile afisi ya rais inaweza kuteka uhuru wake.
“Itakuwa vigumu kwa Jaji Mkuu David Maraga kujinasua kutoka kwa dhana iliyoenea katika umma kwamba ametekwa na afisi ya rais au amejiunga nao kwa hiari yake. Jaji Mkuu hawezi kuwa na mienendo aina hii. Haiwezekani chini ya Katiba ya Kenya ya 2010,” alisema wakili Nelson Havi.
Lakini wiki iliyopita, Bw Maraga alijitokeza kujitetea dhidi ya wanaodai ametekwa na afisi ya rais.
Kulingana naye, kuna umuhimu wa vitengo vyote vya serikali kushirikiana ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo hasa katika lengo la kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.
“Katiba haisisitizi tu kuhusu uhuru wa vitengo vya kitaifa bali pia ushirikiano kati yao. Itakuwa tunaenda kinyume na maazimio ya katiba kama vitengo havitashirikiana kutekeleza majukumu yao,” akasema alipokuwa akizindua ripoti ya utendakazi wa mahakama katika kipindi cha mwaka wa 2017/2018.
Alisisitiza mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa njia huru inayozingatia sheria na ushahidi unaofikishwa mbele ya majaji na mahakimu.
“Kama serikali itawasilisha ushahidi wenye nguvu, tutahitajika kisheria kutoa uamuzi utakaoifurahisha. Kwa upande mwingine, serikali isipowasilisha ushahidi thabiti au ikipatikana kukiuka sheria, vile vile tutahitajika kisheria kutofautiana nayo,” akasema.
Lakini inavyoonekana, wasiwasi wa wakosoaji wake haihusu kuwepo kwa ushirikiano kati ya mahakama na afisi ya rais bali jinsi ushirikiano huo unavyofanywa.
Wachanganuzi wa kisiasa wanaamini Bw Maraga alibanwa na serikali kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu uliofutilia mbali ushindi wa Rais Kenyatta katika uchaguzi wa urais uliofanywa Agosti 8, 2018.
Wakati huo, viongozi wa Chama cha Jubilee wakiongozwa na Rais walisisitiza watalipiza kisasi dhidi ya mahakama.
Kilichofuata ni kuwa mahakama haikupewa kiasi cha kutosha cha fedha kwenye bajeti ya kitaifa, hali ambayo Bw Maraga alilalamika iliathiri vibaya uwezo wa majaji kutekeleza vyema majukumu yao ya utendaji wa haki.
Wiki iliyopita, Bw Maraga alikiri kuwa miradi mingi ya mahakama ilikwama kutokana na jinsi mgao wa fedha ulipunguzwa.
Alitumia muda mwingi kwenye hotuba yake kumwomba Rais Kenyatta azingatie kulegeza msimamo wake hasa kuhusu uzinduzi wa miradi mipya ili angalau mahakama mpya zifadhiliwe na kujengwa kwa manufaa ya wananchi.
Ingawa Rais husisitiza anaheshimu uhuru wa mahakama, huwa hafichi ghadhabu yake kuhusu jinsi kesi za ufisadi zinavyocheleweshwa na hulalamika kwamba milango ya korti imeachwa wazi kwa mtu yeyote kupeleka malalamishi yanayokwamisha miradi ya serikali.
Kulingana na Rais, miradi ya maendeleo inapokwama huwa ni mwananchi wa kawaida anayeteseka kwa kukosa huduma bora na pia kulazimika kulipia madeni yaliyochukuliwa kwa utekelezaji wa miradi hiyo ilhali haikamiliki kwa sababu ya kesi zilizo mahakamani.