JAMVI: Wito wa kurekebisha Katiba wazua uhasama wa mbio za Ikulu 2022
Na VALENTINE OBARA
Pendekezo la kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kutoa ili kuwe na mfumo wa utawala ambapo Waziri Mkuu anateua baraza la mawaziri limeibua msisimko mkubwa wa kisiasa kuelekea 2022.
Ingawa haijabainika wazi kiasi kamili cha marekebisho ya katiba yatakayohitaji kufanywa kufuatia muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga, kuna kila ishara na uwezekano mkubwa wa kubuniwa nafasi mpya za mamlaka ya juu serikalini.
Nafasi hizo zinajumuisha Waziri Mkuu mwenye mamlaka na manaibu wake wawili, hatua ambayo inaweza kupunguza ushawishi wa rais.
Hili ni pendekezo ambalo linashinikizwa na viongozi wa upinzani na wa kidini, huku Naibu wa Rais, Bw William Ruto, na wandani wake akiwemo Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale, wakilipinga vikali.
Kwenye mazishi ya aliyekuwa mpiganiaji wa ukombozi kutokana na serikali dhalimu ya Kanu, Kenneth Matiba, Rais Kenyatta aligusia mdahalo huo akionya wale wanaozungumzia kampeni ya 2022. Inatarajiwa kuwa atazungumzia suala hili zaidi atakapotoa hotuba ya Hali ya Taifa mnamo Jumatano wiki hii.
Kulingana na Bw Ruto, marekebisho ya katiba hayifai kwa sababu yatarudisha nchi katika hali ya kisiasa wakati inahitajika viongozi waungane kuimarisha maendeleo ya taifa, mbali na mchakato huo kugharimu mabilioni ya pesa.
“Wale wanaotaka kuturudisha kwa siasa tafadhali tupeni nafasi tufanye maendeleo. Hatuwezi kuzungumzia siasa za ugavi wa mamlaka milele. Lazima tuanzishe mjadala wa siasa za kuwapa wananchi uwezo kimaisha,” akasema wiki iliyopita akiwa Nakuru.
Hii haikuwa mara yake ya kwanza kuelezea hisia zake kuhusu suala hili. Amekuwa akiligusia katika ziara zake nyingi katika pembe tofauti za nchi tangu Rais Kenyatta na Bw Odinga walipotangaza ushirikiano wao mwezi uliopita.
Pingamizi hizo zimefasiriwa na wengine kuashiria mkakati wake wa kujiepushia hasara atakayopata kimamlaka endapo atashinda uchaguzi wa urais 2022.
“Wanadhani wao pekee ndio wana haki kuzungumzia 2022 lakini pia sisi tuna haki ya kuweka mikakati,” akasema Mbunge wa Tiaty, Bw Kassait Kamket, ambaye aliwasilisha bungeni hoja ya kuunda wadhifa wa Waziri Mkuu na manaibu wake. Bw Kamket ni mwandani wa Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi, ambaye pia anaazimia kuwania urais 2022.
Madeni ya kisiasa
Kufikia sasa, Bw Ruto hana deni kubwa la kisiasa kwa yeyote ikilinganishwa na deni ambalo linabebwa na Bw Odinga kwa viongozi mbalimbali, akiwemo Bw Ruto mwenyewe.
Hivyo basi, naibu wa rais ana kila sababu ya kutetea mamlaka ya rais yasalie jinsi yalivyo kwenye katiba ya sasa. Kwa upande mwingine, Bw Odinga ana madeni hasa kwa vinara wenzake katika Muungano wa NASA ambao ni Kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula (Ford Kenya, na Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi.
Wandani wa vinara wenza wa Bw Odinga wamekuwa wakimshinikiza kigogo huyo wa siasa atimize makubaliano yao kwa kumuunga mkono mmoja wao kwenye uchaguzi ujao na asiwanie urais.
Endapo katiba itabadilishwa kuwe na nafasi mpya za uongozi wa taifa na vinara wa NASA waendelee kuwa pamoja, Bw Odinga anaweza kutimiza makubaliano hayo yaliyowekwa kati ya vinara, na wakati huo huo atimize azimio lake la miaka mingi la kuongoza Kenya.
Taswira ya kwanza ni kuwa, Bw Odinga anaweza kukubali kutowania urais na aunge mkono mmoja wa vinara wa NASA, kisha apewe wadhifa wa Waziri Mkuu.
Raila awe Rais
Taswira ya pili ni kuwa, Kiongozi huyo wa Chama cha ODM anaweza kukubaliana na wenzake apewe nafasi ya kutimiza azimio lake la kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, kisha mwingine kati yao apewe wadhifa wa Waziri Mkuu.
Hata hivyo, uwezo wa kuwa Waziri Mkuu utategemea jinsi katiba yenyewe itakavyoundwa kwa kuwa, katika mataifa mengi kwingineko duniani, wadhifa huo hushikiliwa na chama kilicho na wabunge wengi zaidi.
Wiki iliyopita, Bw Odinga alisema mabadiliko ambayo anashughulikia pamoja na Rais Kenyatta yanalenga kusuluhisha changamoto za wizi wa kura, ukabila, ufisadi, ugatuzi na usalama. Baadhi ya masuala haya yatahitaji kura ya maamuzi.
“Nilisalimiana na Uhuru kwa sababu alikubali masharti tuliyoweka. Tumeanza upya kubadilisha mambo Kenya hii. Tusiposuluhisha matatizo ya 2017 hakuna 2022. Ndio maana tumesema lazima turekebishe mambo mapema wakati huu. Uhuru amekubali na Raila amekubali, sasa wewe ni nani unapinga?” akasema mjini Kakamega.
Wazo hili liliungwa mkono na Bw Mudavadi ambaye alisema hivi majuzi kwamba, itakuwa njia mwafaka ya kurekebisha hali ambayo Wakenya wengi wanahisi inaenda mrama tangu 2010 ambapo katiba ya sasa ilipitishwa.