Je, ulijua wadudu hawa kando na kuwa chakula cha kuku wanaliwa na binadamu?
WADUDU maalum aina ya BSF, ni miongoni mwa mbinu ambazo wakulima wanakumbatia kupunguza gharama ya ufugaji.
Kwa Kiingereza, wanafahamika kama Black Soldier Flies (BSF) na wafugaji wa kuku na samaki wanawashabikia.
Steji ya viluwiluwi (larvae), ndio inatumika kama chakula cha wanyama.
Hata hivyo, ulifahamu kuwa wadudu hawa pia ni chakula cha binadamu?
Kulingana na wataalamu, wadudu hawa waliosheheni virutubisho vya Protini wanaposagwa, unga wake unatumika kuunda vitafunwa.
BSF wanakadiriwa kuwa na asilimia 40 hadi 50 ya Protini na mafuta yenye afya – asilimia 25 hadi 35.
Timothy Malasi, mwenyekiti Joyful Birds Self-Help Group, kundi linaloendeleza ufugaji wa kuku jijini – eneo la Kayole, Nairobi anasema wadudu hao wamewasaidia kupunguza gharama ya uzalishaji.
“Wanakuwa tayari kugeuzwa kuwa malisho ya kuku kwa muda wa siku 14 pekee,” Malasi anasema, akikadiria kupunguza gharama kwa asilimia 25 kupitia matumizi ya BSF.
Anataja chakula chenye virutubisho vya Protini kama mojawapo ya nguzo kuu kufanikisha ufugaji wa kuku na hivyo BSF wanawafaa pakubwa.
“Tunapowachanganya na Azolla – mmea wenye chanzo cha Protini pia, tukifanya mahesabu gharama jumla inapungua kwa karibu asilimia 50,” anaelezea.
Joyful Birds Self-Help Group hufuga zaidi ya kuku 500, katika kitongoji cha Soweto, Kayole.
Kando na Protini, wadudu hao pia wamesheheni Vitamini, na maganda yake yana madini aina ya Chitini.
Margaret Ruguru, ni mfugaji mwingine wa kuku ambaye amekumbatia matumizi ya BSF.
“Hawana athari zozote zile kwa mazingira,” Margaret anaelezea.
Ufugaji, mkulima huyu amewaundia vizimba kwa kutumia mbao na vyandarua.
Wanasitiriwa kwa kutumia mbao na vipande vya mitungi ya maji iliyogawanywa mara mbili kasha inawekwa masalia ya chakula na mazao mabichi kama makazi ya kutaga mayai na chakula.
“Hukusanya bidhaa za kula kutoka sokoni kama vile matunda na mboga,” Margaret anaambia Taifa Dijitali.
Huwapa kuku na samaki wake asilimia 80 ya BSF anaovuna, kisha anarejesha asilimia 20 kuendeleza uzalishaji.
Kimsingi, gharama kufuga BSF ni ya chini mno.
Kando na kuwa mbinu mbadala na endelevu kufuga kuku, pia ni chakula cha samaki, nguruwe, na wanyama wengine wa nyumbani.