Jenerali Mkunda aonya waandamanaji dhidi ya vurugu
MKUU wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi nchini Tanzania Jenerali Jacob Mkunda, ameonya dhidi ya vurugu na uhalifu vinavyoshuhudiwa kwenye maandamano ya vijana ya kupinga uhalali wa uchaguzi wa Oktoba 29.
Akizungumza mjini Dar-es-Salaam, Jenerali Mkunda alisema Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (TPDF) halitakaa kimya huku makundi ya waandamanaji yakiingia mitaani, kuvuruga amani na kupinga mchakato halali unaoendelea wa uchaguzi.
Amesisitiza kwamba jeshi, kwa kushirikiana na polisi na vyombo vingine vya usalama, liko tayari kufanya kazi yake kwa kuzingatia sheria ili kurejesha utulivu iwapo machafuko yataendelea.
Amesema vitendo vinavyoshuhudiwa kwa sasa ni uhalifu unaopaswa kukomeshwa mara moja.
‘ Ndugu wananchi, ikumbukwe kuwa nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya sheria, ambayo lazima izingatiwe na kuheshimiwa. Kutokana na hali hiyo Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania, linawataka watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha vitendo hivyo mara moja, ili kuepusha madhara kwa ustawi wa jamii na taifa letu. Endapo vitendo vya uhalifu vitaendelea, jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania kwa kushirikia na vyombo vingine vya usalama vitaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria,’ alisema Jenerali Mkunda.
Onyo hilo linakuja huku maelfu wakijitokeza barabarani kuoandamana kuonyesha kutoridhishwa kwao na mchakato wa uchaguzi.
Maandamano yalizuka katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam na miji mingine Jumatano wakati wa upigaji kura, kufuatia kupigwa marufuku kwa wagombea wakuu wawili wa urais waliokuwa wapinzani wa Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na madai ya ongezeko la ukandamizaji wa serikali.
Hata hivyo muda mfupi baada ya maandamano kushuhudiwa, utawala nchini Tanzania ulichukua hatua za kudhibiti maandamano hayo ikiwa ni pamoja na kuwarushia waandamanaji vitoa machozi.
Kulingana na shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International, watu kadhaa wameuwawa na wengine kukamatwa tangu vurugu hizi zilipoanza Oktoba 29.
Serikali bado haijatoa maoni kuhusu idadi ya vifo lakini imesisitiza kuwa uchaguzi uliendeshwa kwa amani na uwazi.
Chama tawala nchini Tanzania (CCM), ambacho kimekuwa madarakani tangu nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru wake 1961, kinatarajiwa kuendelea kukita mizizi. Tayari matokeo ya awali yanaonyesha Samia Suluhu Hassan anaongoza kwa asilimia 94 ya kura dhidi ya wapinzani wake 16 anaochuana nao.
Polisi Alhamisi walitangaza kafyu ya kutotoka nje usiku jijini Dar es Salaam makao ya zaidi ya watu milioni saba baada ya majengo ya serikali na ya kibinafsi kuchomwa moto.
Huduma za intaneti pia zilizokatizwa wakati wa uchaguzi na ilianza kurejea taratibu Alhamisi.