Jiji la Nakuru litakavyonufaika na mfumo wa kisasa wa majitaka
SERIKALI ya Kaunti ya Nakuru inajenga mfumo wa kisasa wa majitaka katika mitaa minne ya ya Flamingo, Kivumbini, Kimathi na Paul Machanga.
Maeneo haya yamekuwa yakikumbwa na milipuko ya kipindupindu na magonjwa mengine yanayosababishwa na maji machafu.
Mradi huu wa mamilioni ya pesa ni mpango wa serikali hiyo kuwezesha Nakuru kuwa na mifumo ya majitaka inayoafiki hadhi ya jiji. Mji wa Nakuru ulifanywa jiji miaka mitatu iliyopita.
Miundomsingi ya sasa imedumu kwa zaidi ya miaka 30 na inasaidia asilimia 30 pekee ya makao hayo makuu ya Bonde la Ufa.
Kumekuwa na shinikizo kubwa la matumizi kwa mifumo hii sababu ya ongezeko kubwa la idadi ya watu na ustawishaji wa mji.
Nakuru ina watu 400,000 kutoka 367,183 ambao walinakiliwa katika sensa ya 2019.
Kulingana na wakazi wa mitaa hii, serikali imewasahau kwa muda mrefu.
“Tangu Kenya ipate uhuru, hatujawahi kuwa na mfumo wa majitaka. Sasa tuna kitu cha kufurahia kuhusu ugatuzi. Watoto wetu wamekuwa wakiambukizwa magonjwa,” akalalamika Beatrice Adisa, mkazi wa Flamingo ambapo kuna wakazi 1,000.
Bw James Kiarie, mkazi wa Kivumbini anasema: “Nimeishi hapa kwa zaidi ya miaka 30 ambapo milipuko ya magonjwa imekuwa tukio la kawaida kwa sababu ya uchafu. Mfumo wa majitaka wa kisasa ni afueni kwetu.”
Diwani wa Kivumbini Neto Sakwa anakatilia mkazo matarajio ya wakazi.
“Mradi huu utaimarisha miundomsingi ya maji na usafi katika Jiji la Nakuru. Wakazi wameteseka kwa miaka mingi kutokana na msururu wa maradhi,” akasema Bw Sakwa.
Wakazi wa mtaa mkongwe wa Paul Machanga pia wana matarajio makubwa.
Bw Mohammed Ali ameishi hapa kwa muda mrefu na anaelewa historia yake.
“Mtaa huu una zaidi ya nyumba 200 ambazo zinasimamiwa na serikali ya kaunti. Wakazi watanufaika pakubwa,” Bw Ali aliambia Taifa Leo.
Gavana wa Nakuru Susan Kihika amesifu mradi huu akisema utadhibiti hali ya kuvuja kwa mifereji ya majitaka.
“Nakuru sasa ni jiji na ni lazima iwe kipaumbele ukizingatia kuwa na maji safi na mfumo mzuri wa majitaka,” Bi Kihika alisema.
Gavana Kihika alifichua kuwa mradi huu ni Sh5.6 bilioni na unafadhiliwa na Benki ya Germany Development Bank (KfW).
Kulingana na Bi Kihika, gatuzi hili litashirikiana na washikadau wengine kuimarisha mifumo ya maji katika miji mingine pamoja na Molo na Gilgil.
Kulingana na takwimu za Kaunti ya Nakuru, familia zinazoishi Nakuru hutoa takriban lita 300 za majitaka kwa siku.
Ni wakazi wa mitaa ya hadhi ya juu ambao wananufaika na muunganisho wa mfumo wa majitaka.
Mitaa hiyo inajumuisha Milimami, Langa Langa, London, eneo la katikati ya jiji (CBD), Racecourse na Freehold.
IMETAFSIRIWA NA LABAAN SHABAAN