Jinsi faini ya ‘achulla’ katika jamii ya Pokot inavyotumiwa kuzuia waume kuzaa nje ya ndoa
KAPTUYA Limasya, kijana mwenye umri wa miaka 23 ambaye aliomba jina lake kamili kubanwa kwa kuhofia uhusiano wake wa kimapenzi wa sasa kuvunjika ni mtu ambaye anaumia.
Kaptuya ambaye anatoka eneo la Chepareria, Pokot Magharibi anajindaa kuenda kwa kina msichana ambaye wanataka kufanya harusi ya kuoana.
Hata hivyo, kuna changamoto ambazo zimemnyima usingizi na kumrudisha nyuma.
Kaptuya yuko na deni ambalo hajalipa.
Hajalipa faini ya msichana ambaye alimpa mimba miaka minne iliyopita lakini akakosa kumuoa.
Mwanawe mvulana anaishi na mamake mzazi ambaye hajaoleka kwenye kaunti hiyo.
Kaptuya anasema kuwa anafaa kupanga ng’ombe kumi za kulipa mahari ya mpenzi wake wa sasa ambaye anatazamia kuoa Disemba mwaka huu.
“Ninafaa kulipa ng’ombe wawili kwa msichana ambaye nilimpa mimba kabla ya kupanga harusi,” anasema.
Hapa sasa ndio neno ‘achulla’ linapata maana.
Achulla ni mila ya jamii ya Pokot ambayo inahitaji mwanaume kulipa fidia kwa familia kwa kumpa mimba msichana na hujamuoa.
Faini ama fidia hiyo hutumika kudhibiti wanaume ambao huwa hawawajibiki na wana waliozaa nje na mimba za mapema.
Mvulana husemekana kumharibu msichana na hawawezi kuoana.
Malipo ya uharibifu huo hutegemea na vile familia hizo mbili zitaelewana. Kwenye familia zingine, pesa hulipwa na kwa zingine, ng’ombe ama mbuzi hupeanwa ama vyote viwili.
Mara nyingi, ng’ombe sita hulipiwa mtoto mvulana na watatu kwa mtoto msichana aliyezaliwa.
Wakati wa kuzuru boma la msichana kufanya malipo hayo, kijana huenda na pombe ya kienyeji kwa wazee na fedha ndani ya bahasha.
Kijana mwingine ambaye alizungumza na Taifa Leo bila kutaka jina lake kutajwa anakiri kuwa alilipa ng’ombe watatu kwa msichana wake wa kwanza.
Anasema kuwa alichukua msichana wake ambaye anaishi na mamake mzazi huku akisoma.
“Sitaki jina langu kutajwa kwa sababu ni watoto wengi nje ya ndoa na wakisikia kuwa nilipa mmoja, wengine wataanza kusumbua wakitaka kulipwa,” anasema.
Kulingana na mzee William Lopetakou, neno ‘achulla’ linamaanisha kulipia uharibifu kutokana kwamba mwanaume ameharibu mwanamke na itaathiri maisha yake ya baadaye.
Anaeleza kuwa mila hiyo ina umuhimu mkubwa kwa jamii.
Anasema kuwa mwanaume ambaye huwa amefanya makosa huenda kwa kina msichana akiwa ameandamana na wazazi wake kulipia fidia.
Anaeleza kuwa mwanaume hawezi kusema kuwa anaenda kuoa mwanamke tofauti.
“Huwezi kusema kuwa umepata jiko kwingine. Sio lazima kukutana na msichana ambaye ulimpa mimba. Baadhi ya wasichana huwa tayari wameoleka wakati mwenye alimpa mimba anaenda kwao,” anasema.
Anasema kuwa kuna makubaliamo kuhusu penye mtoto ataishi.
“Msichana anaweza kuchukua mtoto kulingana na makubaliano,” anasema.
Anaeleza kuwa bila kulipa ‘achulla’, msichana ambaye alipewa mimba anaweza kuanza kusumbua mwanaume hata kama ameoa msichana mwingine.
Anasema kuwa ikiwa mtu atashindwa kulipa fidia hiyo, wajomba wake ama marafiki watasaidia kulipa.
Bw Lopetakou anaelezea umuhimu wa mila hiyo kwa kutunza ubikira wa mwanamke na jinsi mimba kabla ya ndoa huchukuliwa na maisha ya ndoa ya baadaye.
“Mila hiyo inasalia kuwa muhimu kwa akina dada ambao hawajaoleka,” alisema.
Anasema kuwa mila hiyo huleta uhusiano mwema kati ya familia mbili ambazo wana wao hawajaoana.
Hata hivyo, Gladys Cheyech mkazi wa Sigor anapuzilia mbali suala la ‘achulla’ akisema kuwa limepitwa na wakati.
“Siwezi kuambia mwanaume ambaye alikosa kunioa kulipa. Haifai kulipa mtu ambaye huishi naye. Hiyo inaleta kutothaminiwa, unyanyapaa, msongo wa mawazo, chuki, mzozo na kutengana na baba na mtoto,” anasema.
Anasema kuwa wanawake ambao hujipata na mimba za mapema ambazo hazijapangiwa hukumbwa na changamoto nyingi.
“Huleta misukosuko kwenye ndoa na shida za kiuchumi,” anasema.
Anasema kuwa ni hatua ya kuwanyima wanawake nguvu na kuonekana wasiokuwa wa maana kutokana na msichana kukosa kuhusishwa kwenye mchakato huo ambao husimamiwa zaidi na wanaume.
Kaunti ya Pokot Magharibi ni ya pili nchini kwa mimba za mapema kwa asilimia 36 na ukeketaji kwa asilimia 44 kulingana na ripoti ya afya wa mwaka wa 2022 (KNBS).